Pages

Saturday, May 2, 2026

YESU ALISHINDA KIKOMBE CHAKE, JE WEWE UTAKISHINDA KIKOMBE CHAKO?

 Bwana YESU asifiwe! Kikombe cha YESU alichopitia hapa duniani kinafundisha mambo mengi, ila napenda ujue na wewe unacho kikombe chako; kikombe cha kiroho.


Yohana 18:10 – 11

10 Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa kuhani mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. 11 Basi YESU akamwambia Petro, rudisha upanga alani mwake, je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee? ”


Kikombe cha YESU maana yake; ni majukumu aliyopewa na makusudi ya MUNGU ambayo YESU aliyakubali, alipoyakubali ni kanywa katika roho. Hiki kikombe kina mateso, mapito, na maelekezo yake.YESU aliandikwa kwenye vitabu vingi na kutabiriwa na manabii atakufa, yote haya yalikuwa katika kile kikombe.


Mathayo 26:36 – 42

36 Kisha YESU akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, ketini hapa, hata niende kule nikaombe. 37 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. 38  Ndipo akawaambia, roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. 39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. 40 Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.  42Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yakatimzwe.”


Ilifika mahali, YESU akaona haya mateso yamezidi katika ule mwili wa kibinadamu. Akiwa Gethsemane; akamwambia Baba yake ‘ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke,’ lakini akakumbuka mapenzi ya BABA yake lazima yatimie, akawambia wanafunzi wake; ‘kwanini ni kizuie kikombe cha MUNGU kisitimie?’


Leo hii katika dunia hii, watu kwakujua na kutokujua wameshindwa vumilia mapenzi ya MUNGU yatimie na kurudi nyuma. YESU alikataa kurudi nyuma, alihakikisha kile kikombe amekinywea. Nawatia moyo watoto wa MUNGU, kuna mambo unaweza kuwa unayapitia, ni Gethsemane yako; kila siku wewe ni madeni tu, hata YESU alikuwa anapita mahali hana pesa, siyo kuwa MUNGU alishindwa mpa, ilikuwa ni Gethsemane yake. Kila mwanadamu ana kikombe chake hapa duniani, na kikombe chako ni tofauti na cha mwingine, ila hakuna jaribu litakalokuja ambalo siyo kiwango chako.


Shetani pia ana vikombe vyake vya maagano, na wengine kwa kujua na kutokujua hawajui wako katika kikombe gani: Kuna kikombe cha wachawi, mizimu, uganga na ufalme wa giza, ambacho mtu anapambana ahakikishe yale aliyopanga yakatimie kupitia majini, mapepo, kulala makaburini, kuuwa; vyote hivi vinakuwa ni vikombe vya maagano mtu amepewa.


Kikombe cha kifamilia; baba anakuwa kichwa cha familia na mama anakuwa ni msaidizi, mlezi wa familia, lakini kuna watu hawawezi angalia familia, kikombe hicho kinakuwa hakipo. Kikombe cha dhambi, hiki kikombe hakitaki wokovu, na YESU moja ya jukumu kwenye kikombe chake; ni Wokovu, ambao sisi tunatakiwa tuupate, ila watu wako na wokovu wa kutamkiwa, wa kikombe cha mapokeo, kikombe cha maagano, kikombe cha dini na miungu.


Leo hii wokovu umefananishwa na mapokeo, YESU hakuleta mapokeo. Unapokuwa kwenye mapokeo ina maana siyo kikombe cha MUNGU, vitu vyote utakavyofanya siyo mapenzi ya MUNGU, mtumishi anaweza kuwa ni wa shetani ila anasema wa MUNGU akiwa na kikombe cha shetani, dini, miungu na malango ya ibilisi.


Na jinsi mtu atendavyo kama ni mtumishi wa MUNGU ni kile kikombe alichopewa ndicho kinafanya kazi. Kile kipindi YESU anahubiri habari za MUNGU, wale Mafarisayo na Masadukayo walikuwa wanampinga YESU kwasababu walikuwa na kikombe cha chini, kikombe cha mpinga kristo, wanaijua kweli lakini hawataki kuikiri, ni ile roho waliokunywa, waliopewa kikombe katika roho.


Katika kila kikombe, kuna wakati wa raha na kuna wakati wa mateso au mapito, ila siyo kwamba unapopita katika mapito ina maana MUNGU amekukataa, Hapana! Jambo ambalo MUNGU amepanga kukupa, ni lazima ameweka katika kikombe uwezo wa kuvushwa na kupita. Kinachotakiwa ni wewe usikate tamaa, omba mapenzi ya MUNGU yatimie katika kikombe alichokupa.


Ufunuo 10: 9-10

“ 9 Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. 10 Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mikono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamukama asali kinywani mwangu, na nilipokisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.”


Watu hawataki kuambiwa ukweli, hawataki kukemewa, wanataka maneno ya MUNGU yaliyo matamu kama asali, yanayo fariji na kufurahisha, hawataki ya kuhukumu, maneno makali, hawataki kurejeshwa, wanachukia ukweli, wanataka asali tu.


Ndio maana watu wanasema dini yangu au kanisani kwetu inaniruhusu kila kitu, pombe sawa, uchawi sawa, hamna shida, hata mchungaji wangu nakunywa naye; hivyo ni vikombe vya uovu yaliopo hapa duniani. Kule kwa adui kwenye mapokeo, hawakemei, hawasemi ukweli, wanazidi wapumbaza, wanachanganya uongo na ukweli, na kwa kujua na kutokujua watu wengi wanazidi kupotezwa kwenye mafundisho. Hawafundishi watu kikombe cha YESU, watu wamrudie MUNGU wapate kufika Mbinguni, wanakikombe cha mchanganiko, na huyu MUNGU siyo wa mchanganyiko.


YESU alileta vikombe (5) vya huduma; Nabii, Mtume, Mwalimu, Mchungaji na Mwinjilisti, ila leo hii kimekuja kikombe cha sita, kinaitwa ‘ Askofu’ kimetoka wapi? Hiko ni cha mapokeo ya wanadamu, hakiwezi kuingiliana na kazi ya MUNGU, kwasababu MUNGU hakitambui.


Katika vikombe vya aina mbalimbali: Kuna mchungaji aliyeitwa, ana kikombe cha kuitwa, ila anawezakuwa ameitwa na shetani, akasema ameitwa na MUNGU, na aliyeitwa na MUNGU atasema ni MUNGU. Kuna mchungaji aliyejituma, kikombe cha kujituma, hiko hakijulikani kwa MUNGU, kinajulikana kwa shetani. Kuna kikombe cha kutamani kazi ya MUNGU, hicho ni chako na shetani, MUNGU hayuko hivyo, MUNGU kazi zake zote amezihakikisha. Ndio maana wachawi, wana kikombe hicho katika roho ambacho kinawaongoza waishi na majini na mapepo na kuyatunza.


Katika wokovu huu, kuna kikombe cha wokovu wa kishetani, ndio maana watu wana miujiza ya kishetani, wanaponya kwa; mafuta, kwa udongo, kwa bendera, mishumaa, miti, kikombe cha babu wa loliondo, vyote hivyo ni vikombe vya kishetani lakini vinamsingizia Bwana YESU, na neno la MUNGU linasema; ‘ vitu hivi wanavifanya kwa kifuniko cha jina langu lakini roho ile siyo ya kwangu. ’


Zaburi 75: 7 -8 

7 Bali Mungu ndiye ahukumuye; Humdhili huyu na kumwinua huyu. 8 Maana mkononi mwa Bwana mna kikombe, na mvinyo yake inatoka povu; kumejaa mchanganyiko; naye huyamimina. Na sira zake wasio haki wa dunia watazifyonza na kuzinywa.”


Gethsemane yako yaweza ikawa ni ngumu, ila muangalie MUNGU, unapokutana na mambo magumu unawaza MUNGU amekuacha, hapana! usikaribishe kukataa tamaa, wala usiige kikombe cha mtu alichopewa, MUNGU, yeye ndiye anajua kwa utukufu wake na mamlaka yake. Kuna mahali unaweza fika, ukazani yule uliyemtegemea ataweza kukusaidia, ila asikusaidie ukabaki mwenyewe. Watu wengi wakifika hatua hiyo, ndipo wanapomuacha MUNGU, kwa kumuacha MUNGU ni kukataa tamaa, unapokata tamaa unakikataa kikombe chako.


Ni biashara umeanza, kikombe chako cha kufanya biashara ni cha shetani, kuna mambo lazima utapitia katika hiko kikombe, na ukikosea tu unakuta mambo yanaharibika. Vile vile watu wa MUNGU waliyookoka, kikombe ulichopewa na MUNGU utakapo kikataa lazima utaporomoka. Leo hii wachungaji wamekata hiki kikombe cha Wokovu, wamebaki wachungaji jina hapa duniani, wachungaji wa miungu, wakapewa vikombe vingine na wakaendelea kutenda. Watu wakiona miujiza wanadhani ni MUNGU, ni kweli MUNGU anatenda lakini kwa kikombe gani? MUNGU ni MUNGU mwenye wivu, utukufu wake, haushirikiani na yeyote!


Kuna watu wanapewa kikombe cha utawala na MUNGU, labda ni wafalme, tumeona wakina Daudi na Sulemani, walipewa kikombe cha utawala. Ila kuna watu wanatafuta utawala kwa shetani, itafika mahali lazima aue, ni kikombe hiko na kina nguvu, kina uwezo, na kitafanya.


Mnaogopa kufa kimiwili! kuna kufa na kutokwenda Mbinguni, na MUNGU hana kikombe cha watu waliokufa, wakati wako ni sasa, hata ukizikwa kanisani, kama wewe ni wakuchomwa moto, utachomwa tu! Katika YESU kuna kikombe cha uzima na mauti (kila mtu atakufa na kufufuka); hiko ni kikombe katika roho, na kuna kikombe cha hukumu ambacho kila mmoja ameshakunywa, haki itaenda kama utakwenda Mbinguni au utabaki kwenye moto.


YESU anakuitaji, anarudi, hujui umebakiza siku ngapi, masaa mangapi, maisha sasa hivi watu ni kulogana, ila ngáng’ana na YESU wewe uliyeokoka. YESU alikukubali kikombe chake, mapenzi ya MUNGU yakatimia, je na wewe umekubali kikombe chako cha wokovu? au una kikombe cha dini, kikombe cha miungu, kikombe cha maagano na mapokeo?


SALA YA TOBA:

Bwana YESU, naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya kwakujua na kutokujua, uandike jina langu kwenye kitabu cha uzima wa milele. Natapika vikombe vyote nilivyovinywa; vya mizimu, vya majini, vya mapepo, katika ulimwengu wa roho, hata vile vya kulishwa katika ndoto navikataa na muunganiko wao kwa namna zao nazikataa. Bwana YESU, naomba unitakase, na malaika wako waingie ndani yangu wakanikague, wakavunje kila aina ya vikombe. Mapenzi yako yakatimie kwangu mimi, siyo ya yule mganga, siyo ya yule mtu anayetaka mimi niangamie, anayetaka mimi niteketee, anayetaka familia yangu iwe hivi; wewe MUNGU unajua, naomba mapenzi yako yatimie kwangu mimi kama mimi, katika jina la YESU.

AMEN.

PROPHET HEBRON WILSON KISAMO.