Pages

Monday, May 18, 2026

UNYAKUO NA JINSI UFALME WA MBINGUNI ULIVYO.

 Bwana YESU asifiwe! Habari ya kuja kwa YESU mara ya pili;


1Wathesalonike 4: 13-17

13 Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. 14 Maana, ikiwa twaamini ya kwamba YESU alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye.  15 Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kula mauti.16Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka Mbinguni pamoja na mualiko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya MUNGU; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. ”


Mwisho wa dunia ni pale baada ya YESU atakapokuja kunyakua kanisa lake, kanisa ni wewe uliyempokea. Kisha atakaa miaka saba ndipo atakapokuja kuhukumu, hii inakuwa ni mara ya pili YESU anapokuja ili aruhusu dhiki kuu.

Hivyo, nakukumbusha juu ya habari njema, ili kwamba atakapokuja kunyakua na wewe akuchukue, wakati wako wa furaha ni sasa hivi na kuna neema, mkubali Bwana YESU. Kuwa mkristo tu! siyo chanzo cha wewe kwenda Mbinguni, ni mpaka uokoke, kufa katika YESU, ni kimaanisha umekufa katika utakatifu ukiwa umeokoka, ndipo YESU naye atakunyakua. Ila umekufa hujaokoka ukaambiwa utaombewa, usitegemee YESU atakunyakua. Maana nyingine kama hujaokoka mpaka sasa hivi kibinadamu, ina maana kiroho wewe umekufa, lakini unapompokea YESU, alisema yeye ndiye uzima, unakuwa na uzima.

Wanaotumia jina la YESU makanisani wakisema hakuna kuokoka, ina maana hakuna uhai wanaongoza watu wafe. Unaweza jiona uko karibu na Askofu au Nabii kumbe yeye mwenyewe yupo kwaajili ya kupeleka watu jehanamu. Amesema yaliofanyika gizani yatajwe ‘pyeupe’ na hii dunia imeharibika ! YESU anakuja kwa wewe ambaye bado hujaokoka. Kuokoka siyo kuchanganyikiwa, unatoka kwenye mauti, unakuwa na uzima, hivyo shika sana ulicho nacho.

Kuna unyakuo wa aina mbili, uko wakupelekwa Mbinguni na uko wa kwenda jehanamu; unapofundishwa hakuna kuokoka unakuwa ushanyakuliwa wa kwenda jehanamu.

Katika kujiandaa na unyakuo, MUNGU anatumia watumishi wake; wako manabii/ wainjilisti/ walimu wa ukweli na wa uongo. Watumishi wanapobatiza kwa kisima, anahubiri au kuponya kwa kuchukua pesa, teyari wamekuwa wa uongo. Mtumishi anazuia watu wasiokoke, anapiga harambee za michango, teyari ni waongo, nawe unayekataa kuokoka, unakataa ile kweli teyari umekuwa muongo.


Mathayo 13: 24 -30, 42

24 Akawatolea mfano mwingine, akisema, ufalme wa Mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika bonde lake;  25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. 27Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? 28  Akawaambia, adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? 29Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. 30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusayeni ghalani kwangu.” 42 “ Na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. ”

YESU atakapokuja atachukua ngano; sasa sijui wewe ni ngano au magugu? Katika shamba, magugu ni takataka ila ngano huchukuliwa na kufanywa chakula.

Ngano ni neno la kweli linalopandwa ndani yako lakini magugu ni mafundisho ya uongo yanayopandwa ndani yako, yanakufanya magugu. Anasema yacheni yakuwe pamoja, ila ile siku ya mwisho YESU atachukua ngano na kuchoma magugu. YESU ndiye mwenye ngano, neno la kweli, na shetani ndiye magugu. Unapojiita mkristo lakini hutaki neno la kweli wewe ni magugu.

Ukiangalia katika shamba pakiwa na magugu hakuna mmea unaoweza kustawi, hivyo ndivyo ilivyo, magugu ya kiroho yametawala sana. Unaweza ukawa uko mahali ukahisi ngano kumbe uko madhabahu ya magugu. Magugu hayatoagi ngano (baraka), utavuna nuksi, mikosi, balaa, huoni mema ya nchi. Utabaki sema YESU wa nini, wokovu umechoka; huo ni wokovu wa magugu.

Mtumishi anaweza anza vizuri na MUNGU ila baadaye anakuwa magugu, unakuta watu wako karibu na watumishi, sasa ukiwa karibu na mtumishi ambaye ni magugu naye anakuambukiza gugu, unakuwa husikii wala huelewi. Haya magugu ni roho inayotoka kwa mpinga kristo inaingia ndani yako, na unapoendelea kuomba na kufunga ile mbegu mbaya inaendelea kukuwa, ya umasikini, mikosi, balaa. Tofauti na ukiwa kwa Bwana YESU ambaye ni ngano, unapo omba na kufunga unazidi inuliwa. YESU atakuja chukua ngano, angalia madhabahu uliyopo ina magugu ?

Iko roho ya magugu; utaambiwa barikiwa ila unazidi kukauka, sasa gugu inaponyeshelewa (kubarikiwa) inatoa matunda? Hapana! na ndivyo ilivyo ukiwa na magugu. MUNGU hana ubaguzi ila ukiwa kwenye magugu huwezi muona MUNGU. Wachawi wamejaa kanisani kuliko waganga wa kienyeji wakiwa na irizi mgongoni, injili za kutabiriwa unapokea magugu na siyo ukweli. ‘Tokeni mkatengwe nao,’ gugu linapokusogelea linataka kuharibu usistawi. Unaposikia mtu ameokoka na hali yake inazidi kuwa ngumu, unakuta amekutana na magugu.

Ukijengwa kwenye ufalme wa MUNGU utakapo zubaa na kurudi nyuma, shetani akapanda magugu; utakuwa ni mtu wakuhangaika na maombi kila kituo, kila mkutano. Majengo mengi ni majumba ya shetani, hatuna mahali pa kumuabudu MUNGU, unaweza soma kitabu cha mafundisho au kusikiliza mahubiri ya kwenye redio au TV kumbe unapokea magugu, huoni mabadiliko, unafunga mpaka afya inaporomoka.

YESU akikuita wewe ni mtumishi wake huna mshahara, ila magugu wanaangalia mshahara, wanasahau Bwana YESU anabariki bila mipaka, mtumishi wa MUNGU analipwa na MUNGU. Ila imekuwa kuchangishana, na kunyang’anyana wakidai MUNGU amekuona umfanyie mchungaji kitu, kumbe washakuona fungu la kumi unatoa kiasi gani kwa majina ya bahasha.

Usiogope, na kutia moyo usikate tamaa, okoka na kumpenda YESU. Usiwe mtu wa kumpenda YESU ili akubariki, unaokoka ili usilogwe, unaokoka ili uende Mbingni au uolewe, wala usiseme ushakuwa mkristo unaenda Mbinguni. YESU anakuja mara ya pili kuangalia walio wake, wewe uliyeokoka na una ngano, omba!
 
Na kama bado wewe ni gugu basi mpe YESU maisha yako ili uwe ngano sema;

BWANA YESU naomba unisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya kwa kujua na kutokujua. Naomba unisamehe kwa kuwa nilifuata magugu na siyo ngano mahali ambapo upo wewe YESU. Naomba uandike jina langu kwenye kitabu cha uzima wa milele na kulifuta katika kitabu cha hukumu. Asante Bwana YESU. 

Hongera; mpaka hapo wewe umefanyika kuwa mfuasi wa YESU.

PROPHET HEBRON WILSON KISAMO.