Pages

Tuesday, March 17, 2026

SIKU YA MWISHO YA MWANADAMU

 



BWANA YESU ASIFIWE, Shalom! yatakayotokea kwa kila mwisho wa mwanadamu; uliye hai, aliyekufa, na watakaofwata, ule mwisho wao. Tukijua kwamba kila kitu kina mwanzo na mwisho wake. Walikuwa wengi wameondoka, wamekufa, wanasubiri hukumu ile ya mwisho na unyakuo, na baada ya unyakuo yako mapigo 21 wanadamu kuteseka, mwanaye akishuka kuhukumu.


Ufunuo 20: 11- 15

11 Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na Mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. 13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na mauti na kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 14 Mauti na kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. 15 Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”


Mtu yeyote ambaye hataonekana jina lake katika kile kitabu cha uzima (aliyeokoka) hatakuwa na nafasi ya kwenda Mbinguni. Hakutakuwa na kitabu kilichoandikwa cha ulokole au mlokole! Unapojiita mlokole tayari umepindua wokovu, na mtu anapokuwa mlokole anakuwa wa ajabu, unaweza hisi amechanganyikiwa kwa ajili ya neno la MUNGU, kumbe amekombwa fahamu. Wengine wanapitiliza nakutoa mafundisho ya uongo katika ulokole, na shetani anakuwa nao akiwatala.


Ni dhambi kujiita mlokole, katika ulimwengu wa roho kwa kujua na kutokujua unakuwa umempinga YESU kwa kukiri hayo. Usikubali kuitwa mlokole, ulokole inatabia zake na laana zake, unakuwa kweli unampenda MUNGU, ila kwa hilo jina shetani amekuwekea mashtaka.


Kama nilivyokwisha sema, siku ile ya mwisho ya hukumu atakuja Bwana YESU, siyo MUNGU ni YESU ndiye atakayekuja kuhukumu, itakuwa ni moto usiku na mchana, wataogelea milele baada ya YESU kuhukumu. Kuna kitabu cha uzima wa milele, kitabu cha matendo na kitabu cha mauti, sasa itategemea wewe uko wapi. Atahukumu sawa sawa na matendo ya mtu afanyayo, hakutakuwa na wakati wa kujitetea. Unaweza ukawa unamtumikia MUNGU, ila siku ile ukatupwa katika ziwa la moto, kumbuka hata shetani alimtumikia MUNGU sana lakini bado alitupwa huko, kwa sababu alitenda mabaya na akaendele kutenda mabaya.


Warumi 2: 16

“ 16 Katika siku ile, MUNGU atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo YESU.”


Kutakuwa kuna aibu ya milele ambayo mtu itamtesa maisha yake yote, sasa naposema hata aliyeokoka endapo hataonekana ametenda matendo mazuri, na yeye atatupwa katika ziwa la moto kwasababu kuna watu wanaokoka ila hawataki habari ya matendo mazuri.


Huu ni wakati wa kumrejea MUNGU, hukumu inakuja. MUNGU atamaliza ghadhabu yake na hasira yake kwa wanadamu, mashetani, mapepo, miungu hii mnayoiabudu, majini mnayoyafuga na kuchomea udi, atayahukumu siku hiyo ya ghadhabu na siku hiyo ya mwisho, kila miungu kwa jina lake, hakutakuwa kuna siri hata yaliyofichwa yatafunuliwa.


Na watumishi wa MUNGU wa kweli wanapoifanya kazi ya MUNGU kweli, ujue jina lako lipo katika kitabu cha uzima wa kweli, MUNGU anakutambua na kukujua ‘ Wafilipi 4:3.’


Kwenye yale mapigo 21, watu watauwawa na kuteketea, maana biblia inasema kutakuwa kuna maiti kila mahali, damu robo tatu ya bahari, mito na maziwa. Na ile siku ya mwisho baada ya watu wote kuuwawa, biblia inasema bahari itawatapika, tazama mapigo hayo wamepitia yote wanakuja kufufuka. Ndivyo neno linasema ‘ wataonekana wafu wakubwa kwa wadogo wamesimama katika kiti cha enzi ’ mbele ya kiti cha enzi akikaa YESU, BABA yake akithibitisha uwezo wake, ahadi yake ile siku ya mwisho, utapita kwa jina lako, kutakuwa kuna kitabu cha matendo, kitabu uzima na kitabu cha mauti.


Ufunuo 3:5

5 Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika kitabu cha uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.”


YESU atalikiri jina lako mbele ya BABA yake, wewe ambaye umeng’ang’ania utakatifu, wewe uliyemshinda shetani, YESU atakukiri mbele ya BABA yake.

Kuna watu wamejificha katika njia ya wokovu, ‘ salvation ’ ila bado hawatakwenda Mbinguni. Unakuta mchungaji ni mchawi, anachukuwa kucha na nywele za watu, utatupwa huko kwenye ziwa la moto na wale unaowaongoza watatupwa huko. Hutaweza jitetea, utaonyeshwa picha zako kwa matukio yako mbali mbali.


Ninaposema juu ya habari ya mwisho wa dunia, mwisho wa mateso, ambao ni mwisho wa mwanadamu, ni hivi; Hiyo siku ya hukumu hatakuwepo MUNGU, biblia inasema atahukumu kupitia mwanaye YESU Kristo. Atakuwepo YESU KRISTO, Eliya, Musa pembeni, wazee 24 na Malaika. Watakuwepo malaika wa kitengo cha ‘moto wa jehanamu,’ malaika wa kitengo cha kitabu cha matendo na malaika wa kitabu cha uzima, wakipewa majukumu hayo na Mwenyezi MUNGU. Hivyo, hatahukumu dunia nzima sehemu moja, kila eneo atafika hatua kwa hatua, hakuna atakayeweza kujificha, kuna nguvu itakutoa ulipo.


Sasa hivi ninakusihi mtafute huyu Bwana, anapatikana muda huu, kwa kuwa yanayokuja siyo mazuri ni mabaya, usije kutana na haya mateso ya milele, ila mnaona watumishi wa MUNGU wanakusumbua, wanakupigia kelele. Wakati wa Sodoma na Gomora walidharau, hata wakati wa Nuhu. Mrejee MUNGU wakati huu, mpe Bwana maisha yako na kuziacha dhambi zako ili zikafutwe katika kile kitabu cha matendo mabaya na mauti.


Atashuka YESU muda huo, atakuta ngano na magugu. Ngano ni mtu ambaye hashindani na MUNGU, ametii, amekubali, amekaa katika mafundisho ya kweli. Yamkini na wewe ni ngano endelea kumshikilia MUNGU usilete ubishi. Magugu anaweza akawa; Nabii, Askofu, Mchungaji, mfanyabiashara, mtu wa aina yeyote katika eneo lolote. Akasema ‘ waacheni wakue pamoja ngano na magugu’ na siku ile YESU atasema watoeni kwanza magugu yatenganishwe na ngano. Jikague ujiangalie kama una haya magugu yatoke.


Nasema na mataifa yote, YESU anarudi, tubu na uokoke, huyu MUNGU ni wa rehema, bila wokovu lazima uende Jehanamu. Mtu yeyote anayetaka kwenda Mbinguni, lazima ukiri Bwana ni mwokozi wa maisha yako, ni lazima ukiri, siyo kuamini, hata mashetani wanaamini lakini hayakiri. Acha mafundisho ya uongo, mapokeo ya wanadamu na ukabatizwe kwa maji mengi.


Ile siku ya mwisho, kuzimu itatapikwa, itachomwa, haya mapepo yote dunia nzima ambayo mwanadamu anayafuata, mizimu ya ukoo wenu watachomwa na wewe unayewafwatlia, mtachomwa kwa moto ambao unaishi milele. Mtapasuka kama popcorn ila hamfii milele, asubuh mpaka jion uko kwenye moto wa MUNGU. Mnaotoa kafara, watumishi wachawi, manabii matapeli, vyama vya kishetani, huo moto unaenda kuwachoma, dunia itakwisha, haijalishi una utajiri wa namna gani.


Lazima kusudi la MUNGU likatimie, Mbinguni makao yako tayari, majeshi ya MUNGU yako tayari na nyumba yako iko tayari kwa wewe unayepalilia wokovu wako, unayejitoa kwa kazi ya MUNGU, na ndivyo utakavyolipwa Mbinguni. Anasema asiyefanya kazi na asile, hata MUNGU pia anafanya kazi.


Napenda nikutie moyo na habari hizi usidharau, usipende kuwa Tomaso, mpaka uyaone na kuyasikia, rejea kwake sasa hivi. Injili zimechafuka na zote zilizochafuka ni zakupeleka watu Jehanamu, shetani amepanda magugu yake (watumishi wakipepo, waimbaji wa kipepo) lakini wanaonekana wamesimama imara; ila wanatoa watu kafara na kunyang’anya watu nyota zao. Hii miungu inayowapa nguvu nayo itahukumiwa, itakuwepo kwenye kitabu cha mauti.


Utukufu wa mwisho utakwenda kutikisa hii dunia, kama nilivyokwisha kusema; kiroho tayari na kimwili ni muda wowote. Maneno ya MUNGU ni kweli ni lazima yatimie, hukumu inakuja, uwe umetangulia au umepata neema ya ile siku ya mwisho, badilika sasa!


Wengi waliokufa wanapokwenda hawajui, mtu akishakufa anakutana na hayo, kama ni dhiki kuu au kwenda kuzimu na kama ni mtakatifu anakwenda paradiso mpaka ile siku ya mwisho baada ya hukumu ndipo wataenda Mbinguni. Ila wengi wako kuzimu, wako makaburini wanateseka.


Kuwa makini sana na kuongozwa sala ya toba na mtu humjui, kwa namna hiyo unakamatwa fahamu na kufungwa. Huku kuzimu wametumwa kutafuta kondoo kama mimi nilivyotumwa, Hebron kutafuta kondoo, na shetani ametuma hivyo hivyo kwa wakati wake.


Muombe MUNGU, muulize Roho mtakatifu huyu ni mtumishi wako? Tunza sana wokovu wako, shika sana ulichonacho adui asije kukuibia. Hakikisha uhusiano wako na MUNGU umeujenga na siyo ujenge na mchungaji, wakati ni sasa, YESU hafurahishwi na mtu anamtafuta muda anakata roho.


Hivyo, wewe uliye okoka na utakayeokoka, nakusihi uzidi kufanya matendo mazuri.


SEMA:


Bwana YESU naomba unisamehe dhambi zangu zote, naomba unitenge na hizi dhambi rohoni na mwilini, naomba unipe maisha matakatifu na niweze kusonga mbele. Jina langu naomba uniweke katika kitabu chako cha uzima wa milele, unitoe kwenye maagano yeyote nilioshiriki kwakujua na kutokujua. Mimi mwenye dhambi ninatubu kwako na kubadilika, sitaki kuwa mkristo wa jumapili kwa jumapili, mimi nimeokoka, najua Kristo, wewe chanzo chako ni wokovu, na wewe ni Kristo YESU, siwezi kuwa mkristo, mfuasi wako bila kuokoka. Wanafunzi wako uliwapa kazi, kuendesha dunia nzima kuwaleta kwako, kuwaongoza sala ya toba, nami nimekiri Bwana YESU unisaidie, uniongoze, uniepushe na hili janga la kuchomwa moto.


Eeh YESU nisaidie nisije nikakutana na huu moto, na haya mateso. Amen!


PROPHET HEBRON WILSON KISAMO.