Pages

Monday, March 2, 2026

MAPIGO SABA YA BARAGUMU YA DHIKI KUU YA PILI (MIEZI 14).


Bwana YESU asifiwe!

Naendelea tena leo katika mapigo saba ya dhiki kuu, kama nilivyokwisha kusema yamegawanyika mara tatu, katika miaka ile mitatu ya mwisho ambayo ni mwaka mmoja na miezi miwili ( miezi 14). Nitaeleza mapigo saba (7) ya baragumu ya dhiki kuu, hatua kwa hatua. Haya mapigo ninayo elezea, ni ya pili; yatakutana na wale watakao baki hapa duniani. Naposema mapigo ina maana ni MUNGU anapiga kwa hasira zake kama alivyokwisha kusema.

Napenda nikuambie, hakuna jambo lisilo na mwanzo na mwisho, maneno haya yana mwisho wake, na haya mapigo yana mwisho wake. Lakini wako wanaokuambia hakuna mwisho wa dunia, nachojua ni Alpha na Omega pekee, yeye hana mwanzo wala mwisho, alikuwepo na atakuwepo.

Ufunuo 8: 6 -7

“ 6 Na wale Malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari ili wazipige. 7Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya nchi; theluthi ya nchi ikateketea, na theluthi ya miti ikateketea, na majani mabichi yote yakateketea.”


Katika hili pigo itanyesha mvua ya mawe na moto kutoka Mbinguni, ambayo imeambatana na damu. Hii mvua itakuwa ni mvua ya ajabu haina mfano wake, maji yamejaa damu. Kutupwa katika nchi, ikateketeza theluthi (1/3) ya ardhi, theluthi ya miti dunia nzima itateketea, na theluthi (1/3) ya majani itateketea.

Bahari itabadilika kuwa damu iliyooza; mito, maziwa, mifereji, itakuwa ni damu tu. Hii hali itawapata wanadamu waliobaki hapa duniani baada ya unyakuo, ambao sasa hawataki sikiliza habari za YESU na kuichezea wokovu. Kumbuka MUNGU hachezewi, asemalo lipo na lazima litoke.

Miaka 500 iliyopita, kuna watu wangapi wamekufa? Na bado wanazaliwa wapya. Je, hao waliokufa wameenda wapi? Wale waliompokea YESU, wakaokoka, watafufuka wakati YESU ananyakua kanisa lake. Ambao hawakuokoka, watabaki hapa hapa ili wakashinde kwenda mbinguni kwa mateso kama haya watavumilia, lakini endapo hawata ya vumilia itakuwa ndiyo mwisho wao. Hiyo ni kuvuka kwa jasho lako na mateso, kumkubali YESU chini ya mateso ambayo hayajawahi kuonekana katika dunia hii.


Ufunuo 8: 8 -9

“ 8 Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari; theluthi ya bahari ikawa damu. 9 Wakafa theluthi ya viumbe vilivyomo baharini, vyenye uhai; theluthi ya merikebu zikaharibiwa.”


Theluthi (1/3) ya bahari ikawa damu, viumbe vya baharini; samaki wa aina zote na wanyama wa baharini, wateketezwa wote. Na theluthi (1/3) ya merikebu; meli, boti, mangalawa, na usafiri zingine za majini ziliharibiwa. Robo tatu ya dunia nzima yatazama kuteketea na kubaki robo.


Ufunuo 8: 10-11

“ 10 Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka Mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya theluthi ya mito, na juu ya chemchemi za maji. 11Na jina ile nyota yaitwa Pakanga; theluthi ya maji ikawa pakanga, na wanadamu wengi wakafa kwa maji hayo, kwa kuwa yalitiwa uchungu.”

Nyota ‘Pakanga’ ya moto itatupwa chini, itaangamiza na kuteketeza katika bahari; na watu watakao kuwa humo watakutana nayo mateso. Wanyama baharini watakuwa wamekufa, bahari itanuka, mifereji, vyanzo vya maji, itakuwa ni mateso na hewa mbaya.


Ufunuo 8 : 12

“ 12 Malaika wa nne akapiga baragumu, theluthi ya jua ikapigwa, na theluthi ya mwezi, na theluthi ya nyota, ili kwamba ile theluthi itiwe giza, mchana usiangaze theluthi yake, wala usiku vivyo hivyo. ”


Katika dunia nzima ni robo tu ndiyo ina mwanga, na usiku itakuwa ni robo tu ndiyo usiku, kwahiyo ni giza tupu kila wakati. Haya yote ni mateso yameandaliwa kwaajili ya dhiki kuu, kwa wale watakaoyapata.

Nakutia moyo kipindi hiki mpokee Bwana YESU, usichezee wokovu, usimchezee na Bwana YESU. Shetani hapendi kabisa watu wazijue hizi habari; sijui ni wewe utakuwepo, sijui ni nani atakuwepo, hata aliyetangulia atakutana na habari hizi.

YESU alivyokufa alitangulia kaburini, kule kaburini aliwahubiria pia, wale waliomkubali walipona, waliomkataa watabaki hivyo hivyo, maana siku ile YESU hatakuwa wakulaumiwa. Hata waliokuwa kuzimu, waliokufa miaka ya nyuma sanaa, aliniambia aliwahubiria, wako waliompokea na wako waliomkataa, kama ilivyo hapa duniani wako waliompokea na waliomkataa.

Ukisoma maandiko matakatifu, tumeona kipindi kile cha Nuhu, MUNGU aliangamiza kwa maji. Familia ya watu wachache ndiyo ikajaza tena dunia, MUNGU hana hasara! Tumeona kipindi cha Sodoma na Gomora aliangamiza na hii itakuwa haina mfano ambao unafanana na hivyo vilivyopita.

Ninakutia moyo umshike wala usirudi nyuma, wokovu ni kitu cha thamani sana, anaitwa Mwokozi wa ulimwengu. Haya mapigo yasikukute ambapo MUNGU ataachia hasira yake kupiga wanadamu.


Ufunuo 8: 13

“ 13 Kisha nikaona, nikasikia tai mmoja akiruka katikati ya Mbingu, akisema kwa sauti kuu, ole, ole, ole wao wakaao juu ya nchi! Kwasababu ya sauti zisaliazo za baragumu za malaika watatu, walio tayari kupiga.”


Sauti inasema; ole waliosalia huko, hatakama unahubiriwa habari za YESU hapo ulipobaki, je haya mateso yote utaweza kupona? Katika hali ya kihalisia, mtu ukitishiwa maisha usiokoke, unamuacha YESU, ukitishiwa unafukuzwa kazi, mke au mume anakuacha, unamuacha YESU, hayo sio mateso ila bado utamuacha YESU.

Naye shetani amezifunga habari hizi msizielewe, na habari hizi hazitakuwa na nabii, mtume, mwinjilisti, askofu, mwanaume au mwanamke. MUNGU atatenda haki, atakwenda kutimiza neno lake kama alivyosema ‘ iwe usiku ikawa usiku,’ ilitabiriwa YESU atakuja na akaja, atakufaa na atapaa na imekuwa hivyo. Na sasa tuna msubiri kurudi kwa mara ya pili ambapo atalinyakua kanisa.

Mkristo ambaye umekataa kumpokea YESU, unafarijika tu kujiita mkristo na kwenda kanisani, na kuimba nyimbo za MUNGU na kusoma kitabu kitakatifu, hii haitakusaidia, YESU Kristo anakuhitaji uokoke.
 

Ufunuo 9: 15 – 20

“ 15 Wale Malaika wanne wakafunguliwa, waliokuwa wamewekwa tayari kwa ile saa na siku na mwezi na mwaka, ili kwamba waue theluthi ya wanadamu. 16Na hesabu ya majeshi ya wapanda farasi ilikuwa elfu ishirini mara elfu kumi, nilisikia hesabu yao. 17 Hiyo ndivyo nilivyowaona hao farasi katika maono yangu, nao walikaa juu yao, wana dirii kifuani, kama za moto, na za samawi, na za kiberiti; na vichwa vya farasi hao ni kama vichwa vya simba, na katika vinywa vyao hutoka moto na moshi na kiberiti. 18 Theluthi ya wanadamu wakauwawa kwa mapigo matatu hayo, kwa moto huo na moshi huo na kieriti hicho, yaliyotoka katika vinywa vyao. 19  Kwa maana nguvu za hao farasi ni katika vinywa vyao, na katika mikia yao, maana mikia yao ni mfano wa nyoka, ina vichwa nao wanadhuru kwa hivyo. 20  Na wanadamu waliosalia wasiouwawa kwa mapigo hayo, hawakuzitubia zile kazi za mikono yao, hata wasiwasujudie mashetani, na sanamu za dhahabu na za fedha na za shaba na za mawe na za miti, zisizoweza kuona wala kusikia wala kuenenda.”


Theluthi ya wanadamu watauwawa wote (pigo la pili). Na neno la MUNGU linasema; watapona ambao hawakuabudu sanamu kipindi hicho. Lakini sasa hivi kuna wakristo wengi wanaabudu sanamu, ina maana teyari wameangamia. Wanaoabudu sanamu, pesa, wanaoenda kwa waganga, wakristo wanao nunua majini, majini yana waongoza, wamekuwa watumwa wa mashetani. Napenda nikuambie, yeyote mwenye majini, ni mtumwa wa shetani, yana mtuma huku na huku, umemkataa YESU, umetaka kuwa na mashetani.

Haya mapigo hayatakuwa ya kawaida, ni mapigo ya kutesa. Kama alivyokwisha kusema, mvua ya mawe itadondoka kutoka Mbinguni. Mawe yakikukuta, yatakupasua na kuteketeza, kama ni makubwa, manyumba na miundo mbinu itabomoka. Biblia inasema; merikebu, robo tatu ya dunia nzima yatabomoka yote, itabaki robo MUNGU apendavyo. Haitakuwa sehemu moja, ni kwa utukufu wake MUNGU, kila mahali atabakiza robo, robo.

Huyu MUNGU ni waajabu sana, atakavyofanya anajua yeye. Kumbuka wakati ule Nuhu alivyojenga safina, Malaika akaongoza wanyama wawili kwa wawili wakienda, kwahiyo MUNGU anajua namna atakavyowaficha wenyewe. Mifugo tulio nao wote wataangamizwa kwasababu ni mali zake yeye mwenyewe. Sisi pia ni mali zake, yatupasa kumtii, yatupasa kumsikiliza.

MUNGU ameweka mapigo ili kumuadhibu shetani na wale ambao hawamsikii. Na hivi ndivyo wanadamu wataadhibiwa kwa mapigo ambayo aliyaanda Mwenyezi MUNGU. Kila jambo lina wakati wake na muda wake, sasa kuna mwisho wa kuishi wanadamu hapa, na kuna mwisho ambao ni milele. Sasa hakikisha sanaa una shika utakatifu, uwe ni yule mkristo wa kujua neno la MUNGU unasoma, lakini siyo mkristo mtakatifu. Ni kimaanisha mkristo mtakatifu ni yule aliyeokoka na sura ya ukristo wa Mbinguni, MUNGU anakujua na ni mfuasi wa YESU Kristo. Na kama ni mkristo ambaye hujaokoka, wewe ni mkristo wa sura ya duniani, sura ya kuzimu pasipokujua na kujua.

YESU anarudi, sijui siku wala wakati, ila habari hizi, mimi namtengenezea njia ili wewe ukapate kuvuka. Usiwe mtu unaambiwa habari za YESU anaokowa, ila wewe hutaki. Wewe unasema unakwenda zako jumapili kwenye dini yako, dhehebu yako. Napenda nikuambie nilichokiona Mbinguni; hakuna dini iliyosajiliwa Mbinguni, hakuna dhehebu iliyosajiliwa Mbinguni. Haya madhehebu na dini yanasajiliwa hapa duniani kwenye serikali malimbali lakini kule Mbinguni ni wokovu tu.

Unajitia moyo unasema utakufa na dini ya ukoo wako, dini na dhehebu litaandika jina lako kwenye vitabu vya maofisini, vitabu vyao, watatambua wewe ni mwana wa dini lakini siyo mwana wa YESU. Kubali uandikwe na YESU muda huu, anakuhitaji.

Dini zinakuruhusu kunywa pombe, tutaonana jumapili utakuja kutubu, endelea na uganga, ushirikina, tutaonana jumapili, kanisa linakujua wewe ni mfuasi wetu. Hizi zote ni janja za kukuteka wewe mwanadamu, ukristo wa kwenda Mbinguni hauna mambo hayo. Huo ni ukristo wa ‘anti – christ.’

YESU ameleta wokovu, kwanini hutaki? Kwanini unaukataa? Wakristo wengi waliookoka wanarudi nyuma, wanarudi kwenye udini, Roho Mtakatifu hana dhehebu. Hizi dini na madhehebu ndizo zilimpinga YESU, yeye alileta wokovu na kujenga kanisa lake.

Imempendeza MUNGU majira haya kukujuza juu ya mapigo saba ya baragumu, ambayo sijui kama utaweza vumilia. Neno la MUNGU linasema robo tatu kati ya wale waliobaki watauliwa, watakuwa ni mizoga. Kila mahali ni miozo, sijui kama utaweza vumilia, maana kipindi kile unaambiwa busu sanamu, ukibusu unabaki, ukisema unampenda YESU unateswa. Yamkini umesikia habari za YESU na ukazijua, ukazubaa, kipindi kile hutasikia mtu akisema tena.

Baada ya ile miaka mitatu na nusu ndipo mapigo yatanza. Leo nimeongelea pigo la pili baada ya miezi 14 ya kwanza, ndipo inakuja pigo lingine. Hapo inakuwa ni miaka minne na miezi miwili, ni mapigo tu, mateso kwa mateso. Jicho la MUNGU litakuwa linakuangalia, utamuomba MUNGU akusaidie, YESU akusaidie, na utaita Roho Mtakatifu, hutapata msaada. Utabaki na neno ambalo lipo kwenye akili na kwamba unampenda YESU.

Kwanini usisimame imara sasa hivi? Unasema bado, bado, hujui umebakiza siku moja au masaa machache ukate roho. Na pale unapokata roho tu, ndipo hatima yako imekwisha, haijalishi sanduku lako litaenda kanisani, litaombewa, litafanyiwa sala za kila namna, utamwagiwa ubani, haikusaidii. Utatolewa sadaka, utatamkiwa umetoka kwa udongo, kwa Kristo utafufuka, hatawasingekutamkia bado ungefufuka na kubaki hapa kwajili ya mateso kama hukumpokea YESU.

Hutaona ukoo wako uliokuwa unawachinjia mbuzi, mababu uliokuwa unawapelekea pombe ili wakusaidie. Sasa huwezi acha dhambi? Yatakayokuja yatakuwa magumu, ubani wa uvumba unaochoma huwezi kukusaidia, haiwezi fukuza mapepo, shetani hawezi fukuza shetani mwenzake, ni jina la YESU tu. Iko dhambi imetawala sasa hivi sana; kubadilisha uumbaji wa MUNGU.

1Timotheo 1: 10

“ 10 Na wazinifu , na wafiraji, na waibao watu, na waongo, nao waapao kwa uongo, na likiwapo neno lolote linginelo lisilopatana na mafundisho ya uzima.”


Dhambi hii inahusu wanawake na wanaume, uwe umeokoka au hujaokoka. Nikiongea habari ya uzinzi, imekuwa kitu cha kawaida bila hofu, kama enzi za Sodoma na Gomora, dhambi imekuwa kawaida katika dunia hii ya sasa hivi. Kama neno linavyosema, wafiraji; ni kufanya tendo la kujamiana kinyume katika sehemu MUNGU ameanda ya kutoa kinyesi. Ule ubikra, MUNGU aliumba katika sehemu ya kutolea mbolea haipo, na jambo aliloruhusu MUNGU hatakama ni wana ndoa akalibariki, limekuwa halitumiki. Kataa hilo jambo litakufanya usiende Mbinguni, ni watu wachache wenye ubikra katika sehemu ya kutolea kinyesi. MUNGU atakuuliza kila kiungo nilikiumba kwa kazi yake, je hiyo ndiyo kazi yake?

Naongea habari hizi kwa mataifa yote, wewe unayefira na wewe unayekubali, mna dhambi wote mmeshiriki. Aliye wa MUNGU atashuka na kurejea, usiwe wa MUNGU utakaza kichwa. Hayo mapigo yatakayokuja ni ya kutisha sanaa, naeleza kwa namna kidogo sana lakini hiyo siyo uhalisia wake. Bado ni mambo ya kutisha.

Rejeeni kwa YESU, MUNGU ana hasira, na hasira yake ni mbaya. Achana na masanamu, acha kusajiliwa kwenye mavitabu ya ukristo. Mpe YESU maisha yako, anakuhitaji wewe.


SALA YA TOBA:


SEMA; BWANA YESU, NINAKUOMBA UNISAMEHE DHAMBI ZANGU ZOTE NILIZOFANYA. NINA MKATAA SHETANI NA MIPANGO YAKE YOTE, NA UKRISTO WA DINI SIUTAKI NA WA KIMADHEHEBU. NINATAKA WOKOVU WAKO, ROHO MTAKATIFU, EEH MUNGU, UNIONGOZE NI KAZIDI KUSIMAMA IMARA, NIKIKUSHUKRU WEWE NA KUKUTUKUZA WEWE, SIKU ZOTE ZA MAISHA YANGU. JINA LANGU ULIANDIKE KATIKA KITABU CHAKO CHA UZIMA WA MILELE, SIKU ZOTE NA UNIONGOZE BWANA KWA UTUKUFU WAKO.


Mpaka hapo umeokoka, Mbingu ikikushangilia, wokovu na utakatifu ukatembee katika maisha yako. Ukaangaze, ukutoe katika giza, ukuonyeshe mahali alipo Bwana YESU Kristo. Hatua baada ya hapo, ubatizwe kama vile atakavyo Bwana, maana ubatizo wa kikombe hujatoka Mbinguni wala hauta kupeleka Mbinguni. Mambo yote yatapita lakini neno litabaki pale pale, AMEN!


PROPHET HEBRON WILSON KISAMO.