Pages

Friday, February 27, 2026

DHIKI KUU NI LINI?


Bwana YESU Asifiwe!


Dhiki kuu, ni jambo ambalo lina muhusu kila mwanadamu. Ni vizuri ujue habari ya dhiki kuu, ni dhiki ya mwisho, dhiki ni mateso, ambapo haya mateso yanaitwa dhiki kuu. Inamaana kwamba, kutakuwa kuna mateso ambayo hayajawahi kuonekana wala kutokea katika dunia hii, ndomaana inaitwa mateso makubwa, dhiki kuu.

MUNGU ameandaa haya mateso kwa ajili ya ile siku ya mwisho, kwa wale ambao wamekataa, wamechezea na kudhihaki wokovu. Kuna wanaotamani hii siku ifike ‘mwisho wa dunia’ kwa kujua na kutokujua, hawajui nini kitakachotokea. Na ni lazima hii siku iwepo, ni lazima itokee, sasa ni vizuri ufahamu juu ya dhiki kuu.


1Wathesalonike 4: 13 – 17

13 Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. 14  Maana, ikiwa twaamini ya kwamba YESU alikufa, akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika YESU, MUNGU atawaleta pamoja naye. 15  Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. 16  Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka Mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya Malaika mkuu na parapanda ya MUNGU; na waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.’’


MUNGU, yeye ni wa haki, aliniambia miaka michache kama kunipa taarifa. Siku ile ya mwisho itakuwa kama kile kipindi cha Nuhu; wakicheka, wakidharau, watanyakuliwa wachache. Sasa isiwe kwako kwa sababu MUNGU hana la kulaumiwa, tayari amekujulisha wewe. Ni wewe mwenyewe uchague, ni wewe mwenyewe ukatae. Wale ambao watakuwa wamekufa kimwili na kuzikwa, watafufuliwa. Wenye dhambi na ambao hawana dhambi, wote watafufuliwa. Lakini, wale watakaonyakuliwa, ni wale wa Bwana YESU. Watakao baki hapa duniani, hata waliofufuliwa, lakini wana dhambi; ni wachawi, wenye mambo ya ajabu, ambao hawajaokoka, watakuwa hai wote hapa duniani, wakibaki kusubiria dhiki kuu.

Ni vizuri sanaa mwana wa MUNGU ukaepuka hii dhiki kuu. Kipindi hiki, ni cha neema ya kutengeneza na Bwana YESU, pakiwa bado hakuna ugomvi, hakuna kuugua kwa upanga wala usumbufu, ni kwa amani. Je, hiko kipindi cha dhiki kuu, utakiweza?

Daniel 9: 27

“ 27 Naye atafanya agano thabiti na watu wengi kwa muda wa juma moja; na kwa nusu ya juma hiyo, aitakomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu.”


Kwa majuma saba, ina maana baada ya unyakuo ndiyo dhiki kuu; Na MUNGU anaondoa wale ambao wameshinda katika wokovu, wasikutane na hiyo hali. Hivyo, kutakuwa na miaka saba ya mateso, lakini mateso hayo, hayataanza siku hiyo hiyo. Na kila mmoja atagundua kabisa YESU amenyakua watu wake. Mtaona wale ambao wamekufa, wako duniani, uliwasahau, utaona wako wamerejea, utawaza wametoka wapi? Hiyo ni dalili ya kwanza. Sasa wewe utakayebaki, utaivumilia hiyo dhiki kuu?
Nachokufundisha, usimcheze MUNGU, usimcheze YESU, ni vizuri kuwa makini na kumshika sana YESU.


Ufunuo 11: 1-3

“ 1 Nikapewa mwanzi kama fimbo; na mmoja akaniambia, inuka, ukalipime hekalu la MUNGU na madhabahu, na hao wasujuduo humo. 2  Na behewa iliyo nje ya hekalu uiache nje wala usiipime, kwa maana mataifa wamepewa hiyo, nao wataukanyaga mji mtakatifu miezi arobaini na miwili. 3  Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia.”


Miezi arobaini na miwili ni siku 1,260 sawa na miaka mitatu na nusu. Siku hizi 1,260 wale waliobaki katika dhiki kuu watakuwa wakitawala kwa raha na amani, lakini baada ya miaka mitatu na nusu ya YESU kulinyakua kanisa, neno la MUNGU linasema, watakuwa wamevaa magunia. Kutatokea sheria ambazo zitabadilishwa kama neno la MUNGU lilivyo badilishwa wakati huu, kwa kupinduliwa. Itawezekana watabadilisha, watasema hakuna kuokoka kabisa, wewe utasema, umeokoka lakini umebaki, unakatwa kidole, unadhuriwa kwa hali yeyote, hakuna serikali ya kukutetea wala huruma, hii siku siyo ya kuitamani!

Amos 5: 18-20

18 Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya BWANA; kwani kuitamani siku ya BWANA? Ni giza, wala si nuru. 19  Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma. 20  Je, siku ya BWANA haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.”


Hiyo siku ya mwisho, watu wanaitamani, YESU atakaporudi ninyakuliwe, lakini umejiaanda? Neno la MUNGU linasema, Ole wenu mnaoitamani! Tumeshapewa taarifa, ili uwe makini, kwasababu utakapo baki kuna mateso ambayo utakwenda kukutana nayo, mabaya saana. Hii dhiki kuu ina mapigo mengi, kuna adhabu 21 ya mapigo ambayo nitakujaelezea. Na MUNGU mwenyewe ataongeza roho ya uovu katika dunia hii, ili kwamba watu wateseke, watu wapigwe, watu waangamie kwasababu alishakuelezea na alikuonya.

Ufunuo 6: 12

“ 12 Nami nikaona, alipoifungua muhuri ya sita, palikuwa na tetemeko kuu la nchi; jua likawa jeusi kama gunia la singa, mwezi wote ukawa kama damu. ”


Hili ni moja ya pigo, ambalo litafanyika baada ya miaka mitatu na nusu ya mwisho, kumbuka miaka ni saba. Sasa YESU akishanyakua kanisa, watu watabaki hapa miaka saba, kuna watu wengine wanafundisha habari za Kristo, wanasema hayo majumba yatakayobaki yatakuwa ya kwao, kwa mipango yao na dini yao, wamesahau kuwa yatabomolewa yote!

Kwenye yale mapigo 21 ya dhiki kuu, nitakayokuja kuelezea, vitu vyote vitakuja kuporomoshwa, moto utachoma, kwasababu kuna hukumu kutoka kwenye kiti cha enzi. Maana neno la MUNGU linasema ‘ kama siku zisingefupishwa, wengi wasinge enda rithi uzima wa milele, wangerudi nyuma.’

2Wathesolanike 2: 3 -11. Inaeleza Kuna mambo ambayo hayajafunguliwa, na baadaye atakuja mpinga kristo kutawala dunia. Kutakuwa kuna sheria moja, kununua kitu kwa namba, sita sita (666). Ukijiunga tu na hii namba sita sita (666), hapo ndipo itakuwa mwisho wako, huendi tena mbinguni, kwa sababu wengi watakao baki watakuwa walisha fahamu habari hii, ila wali idharau, na kama umedharau basi itakuhusu.

Ufunuo 6: 1-9 yafunua kuwa, watu watachinjwa, watu wata katwa katwa. Kwa wewe utakayempenda YESU wakati huo, ndipo sasa utabadilishiwa kibao uitwe “mpinga kristo.”

Sasa hivi tunajua tuna mpinga kristo ambaye hataki wokovu, anataka masanamu, amebadilisha neno la MUNGU, amebadilisha mambo ya ubatizo. Sasa hawa ndiyo watakuita wewe unayetaka wokovu, mpinga kristo katika nyakati hizo. Kipindi hicho, unamtaka YESU, hutaki kusali sala za wafu, unataka ubatizwe kwa maji mengi, watakudhuru sana kwa kutamani njia za YESU katika wakati huo. Na jicho la MUNGU litakuwa linakuangalia, ila utapona mwenyewe, kwa jasho la damu yako.

Sasa hivi unatukanwa, unasemwa vibaya, unarudi nyuma, unachezea wokovu. Baadaye mapigo yatakuwa ni hatari sana, ukiwa ndipo unautaka wokovu katika dhiki kuu. Kuna watu wengi wanasema wameokoka lakini ni washirikina, wako kwenye matambiko, hawataki kuishi katika utakatifu. Wengine wameokoka wokovu wa kidini, wokovu wa mapokeo ya wanadamu. Wote hawa watabaki hapa duniani, YESU hata wachukua. Amenituma niwaeleze habari njema, lakini, hii dhiki kuu kwanini imeandaliwa? Imeandaliwa kwa ajili ya kuwatesa na kuwapiga wale ambao, hawataki kumpokea YESU mwana wa MUNGU.

Warumi 1:18

“ 18 kwa maana ghadhabu ya MUNGU imedhihirishwa kutoka mbinguni juu ya uasi wote na uovu wa wanadamu, waipingao kweli kwa uovu.” Atasababisha uasi zaidi ili watu wazidi kumkosea, na mpinga kristo, na kukoseana wao kwa wao, hali ikizidi kuwa mbaya.


Pale YESU, anapoinyakua kanisa lake, yeye atakuwa kwenye mawingu. Kumbuka anabaki kwenye mawingu, hashuki kwa miguu yake. Wale waliokufa, waliotutangulia ambao wamekaa na BWANA YESU, na majina yao yako katika kitabu cha uzima wa milele, wao watanyanyuliwa kwanza wata paa. Kutakuwa kuna nguvu iliyoko kwa YESU, inawajua, inawavuta, sio unapaa tu mwenyewe. Umekaa na mtoto, kitoto kinaondoka, mama umebaki unalia kiko wapi. Na wale ambao hawakufa katika YESU, watabaki hapa! hapa! mababu, mabibi, na wengine tunaowajua kwa kila taifa na rangi yao. Basi mnaomchezea BWANA YESU, tazama kipindi kile Nuhu walimcheka, ndivyo itakavyo kuwa. Na kusihi na wewe, usiwe hivyo.

Unapokata roho, napenda uelewe, kuna mambo mawili yanakufwata, kuna huzuni na furaha. Ukishakata roho, unakaa pale paradiso, ulivyo wekeza kwa MUNGU, ndivyo hivyo utakavyopokea thawabu. Utapatwa na huzuni kwa sababu utalipwa sawa sawa na ulivyofanya, ulivyomtolea MUNGU sadaka zako, ulivyofanya kazi za MUNGU, ndivyo utakavyo ishi kule. Utashanga umeingia, unaulizwa unaitwa nani? Utasema ‘Yakobo,’ Malaika anakuambia wewe nenda ‘ street no 4, kaskazini ’ nyumba namba 1,400. Ukienda unakuta nyumba yako haina vitu sawa na wengine, unawaza ilikuaje? Unaanza huzuni, uliwekeza duniani na sasa unalipwa kwa matendo yako. Haijalishi ulikuwa tajiri sana, ulikuwa mtu mkubwa sana, MUNGU anakwenda kulipa mtu sawa na thawabu yake.

Wewe huombi, huendi ibadani, thawabu yako inaondoka.! Kama Malaika Gabriel anawaza, ‘sijui Mikaeli atapewa nini siku ya mwisho, kwa kazi aliyoifanya.’ Mimi, nilijifunza kitu, na wewe jifunze kitu. Utafika mbinguni, wenzako watakuwa mabosi zako, kuna kazi kule na utalipwa tofauti, hata malaika wanalipwa, wazee 24 wanalipwa. Usione hawa wanadamu wana akili ya kufanya vitu vyote hivi, msingi wake ni Mbinguni.

Kuna watu wameokoka dakika za mwisho wakiwa ndiyo wanakata roho, hawa watakuwa na huzuni maisha yao milele, kwa sababu hawakuwekeza kwa YESU.

Mathayo 22: 14

“ 14 Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”

MUNGU ameita wengi, lakini wateule watakuwa wachache. Wako ambao wanaichezea hii injili, hawataki kuiheshimu, hawataki kunyenyekea.

Luka 13: 24

“ 24  Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. ”

Ni watu waliookoka, ni mimi na wewe, vaa msuli kwa YESU, usitikisike, usirudi nyuma, songa mbele. Nakukumbusha uamke usilale, amka! amka! kuna mambo mabaya yatakuja huko mbele. Mbinguni unaenda kwa jasho lako, sio kwa ulegevu, ni mtu aliyesimama. Leo hii wangapi wanapenda kwenda Mbinguni? ni wengi sana, angalia usitamani ukashindwa, umeokoka au wewe ni baridi? unatakiwa uwe moto, umesimama. Au umeokoka katika mafundisho ya uongo? Nilifundisha kuna wokovu wa kidunia, wokovu wa kishetani, wapinga kristo wameingia katika wokovu pia. Watu wanasema wameokoka lakini ni wachawi, freemason, viongozi kwa manabii, wote watachomwa.

Nasema na wewe hapo, nafsi yako wewe itakuwa wapi? na ujiangalie. Na kama hujaokoka, dhiki kuu inakuhusu, mapigo yote yanakuhusu. Hii ni kati yako wewe na MUNGU, siyo wewe na rafiki yako, siyo wewe na ndugu zako. Hakutakuwa na msaada wala kanisa halitakuwepo tena, kanisa ni wewe uliyeokoka, utanyakuliwa juu. Na ndiyo maana neno la MUNGU katika biblia halisemi kuna dini A, dini B au C, ambazo zitakupeleka Mbinguni, hapana! Alileta wokovu tuu, ndiyo kanisa la kwake hilo.

Sasa hivi duniani kuna amani kwasababu ya kanisa, lakini kanisa likishaondoka, amani itaondoka yote, kwa kuwa kanisa ni YESU. Hata katika baadhi za nchi mbali mbali ambapo YESU ameondoka, hakuna amani, au wamemkata YESU, hakuna amani. Amani haitafutwi kwa kupigana au kuongea, amani inaletwa na Mwenyezi MUNGU. Ndiyo maana ninasema, baada ya miaka saba, kanisa likiwa limeondoka, MUNGU ataachilia roho za uovu, watu wata hasi, amani haitakuwepo. Serikali zitaondoka, zitabaki za kishetani na zimeruhusiwa. Maana alishakusema kabla ya ujio wangu, utaziona dalili, mataifa wanapigana, kutakuwa na majanga mbali mbali lakini ni siri iliyofichwa na MUNGU.
Utajuta, utakumbuka maneno ya mchungaji, ya nabii, mtume amekuelezea maneno ya kitabu cha MUNGU na uliyadharau. Wengine walicheka, hakuna wokovu, wokovu umepitwa na wakati, wewe dhiki kuu inakuhusu.

Sasa ambao watafanikiwa tena kwenda, ni ambao watashinda kwa damu yao. Wanakuwa wamepitia mateso, kutobolewa, kukatwa katwa, hufi na wala hakuna matibabu, mateso ya kila namna utakaa nayo miaka mitatu na nusu. Ukiumwa uko hoi, njaa, ukikosa chakula tu au maji unatetemeka, huna nguvu hata ukidondoka ukate roho, hufi. Watu waliokufa bila YESU, wako makaburini, huko chini mvua inawanyeshea, ndiyo maana unasikia mizimu inataka pombe, inataka sigara, ni wale walio kufa inawatesa familia. Ulikuwa na ndege, benzi, hutatembea na hiyo benzi huko kaburini, wanapigwa na kuteseka, huko chini na majini. Sasa kwa nini uchezee wokovu uende kwenye mateso? MUNGU anataka yeye akikuambia kitu usitake kujua nitapata nini? Itakuaje? Chukua hatua ondoka, chukua hatua okoka.

YESU hakuwa mlokoloe, neno la MUNGU, linasema YESU alileta wokovu, anaitwa MWOKOZI wa ulimwengu na siyo mlokole wa ulimwengu, hapana! Soma vitabu mbalimbali, alileta wokovu, hakuna mambo ya ulokole, kama umekiri kwa kujua na kutokujua hiyo ni shida na ni tatizo. Muda huu ninakuletea habari njema, dhiki kuu, utakuwepo?

Anakuja sasa, baragumu zinapigwa, nasikia huko juu, farasi wa kiungu wanashuka, makaburi yakifunguka, wachungaji wa MUNGU wanafufuka miili yao. Wateule wengine waliotutangulia wanafufuka, wao na wewe tutakutana huko mawinguni tukimlaki BWANA YESU.
Ninavyohubiri, miti itakuwa shahidi siku ile ya mwisho ya hukumu, majani, milima itaongea, anga litaongea, utajitetea wapi? Picha yako hii, sauti yako hii, ikusaidie uwaze dhiki kuu.

Usione hao manabii wa kipepo, mitume na wachungaji, hao wameandaliwa na baba yao lusifa ya kuja kufanya kazi ya kupumbaza watu, wasiende Mbinguni wakachomwe. Sasa wewe mlevi utalipa ulevi wako, bangi, sigara, uchawi, hivyo hivyo unavyo ving’ang’ania ni vitu vimewekwa na nguvu ya kuwafanya kubaki hapa hapa. Matambiko, masanamu, hapa hapa maana alishakataza.

Habari yakuambiwa kwamba umezikwa na kanisa, hatakama umezikwa na kanisa, je umefufuka? Ulikuwa hujamkubali BWANA YESU, utabaki huko huko. Na kama wokovu uliokoka, ukafutwa utabaki huko huko. Mguu mmoja ndani kwa YESU, mguu mmoja kwa wachawi, mmoja duniani, badilika. Hakutakuwa na cheo chako, hata wenye cheo kama farao, bado watahukumiwa. Hata wakina Hitler, Iddi Amin mtawaona watafufuka wote, watabaki hapa, lakini ambaye ameokoka amempa YESU maisha yake atakutana naye kwenye mawingu.


SALA YA TOBA:

Mpe maisha yako leo, sema BWANA YESU naomba unisamehe dhambi zangu zote, nilizozifanya kwa kujua na kutokujua, naomba ufute jina langu kwenye kitabu cha dhiki kuu na uliandike katika kitabu chako cha uzima wa milele. BWANA YESU naomba uniongoze, unifundishe na ile siku ya mwisho na mimi niwe mmoja wapo kati ya wale watakaokulaki mawinguni. Amen

PROPHET HEBRON WILSON KISAMO.