Kuwa Mkristo tu siyo kwamba shetani atakuchukia, anakupenda, hana hofu na wewe anajua wewe uko naye tu wakati wowote ila nitakufundisha ni kwa nini shetani huyu huyu ana ugomvi na mtu ambaye ni Mkristo wa aina nyingine.
Mathayo 24:23-24
"Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule."
Point; kuwapoteza hata walio wateule. Wateule ni Wakristo waliookoka, wamemkiri BWANA YESU lakini YESU anasema, tazama watakuja Makristo. Nitaelezea kwa vipengele tofauti ili upate kuelewa.
1. MAKRISTO:
Makristo ndo haya mashetani ambao ni wanadamu waliompokea Krista wa uongo ambao wapo kwenye viwango vya juu sana; hao wanaojiita Freemason, Mpinga Kristo wanaobadilisha neno hao ndo biblia wanaita Makristo na hata YESU kwa kinywa chake aliwaita Makristo. Duniani ukiskia mtu anaanza na jina "Ma" ina maana ni mabaya. Inawezekana mwanadamu wewe ni mmoja wa Makristo pasipokujua au kujua. YESU alisema Makristo, aliongeza neno kama la chuki pale yaani hapendi. Hao Makristo wakawapoteza hata Wateule na wamegawanyika. Wamegawanikanyaje? Kuna Makristu na kuna Mkristo na kuna Mkristo aliyezaliwa kwa roho siyo kwa damu. BWANA YESU ASIFIWE! Katila wote hawa shetani haogopi Makristo, haogopi Mkristo wote anaona ni watu wake tu hana shida nao na ndio maana kuna watu wanakuambia kabla ya kuokoka mambo yao yalikuwa yanaenda vizuri, waombe, wasiombe mambo yananyooka tu na vitu vinakwenda hakuna vita wala vikwazo, ni kwa nini? Shetani anakujua wewe ni mali yake.
2. MKRISTO MTEULE
Hawa ni wale Wakristo waliozaliwa mara ya pili na wamemkiri YESU na waliozaliwa katika roho. BWANA YESU ASIFIWE!
Warumi 10: 9-10
"Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu."
Ninaposema kwamba shetani hawaogopi Makristo wala hana shida nao, ni kwa sababu anajua tayari ameshawateka, ameshawamaliza, na dunia hii Wakristo wengi wamekaa wakijua ya kwamba watakwenda mbinguni, wakati hawatakwenda mbinguni. BWANA YESU ASIFIWE! Hii ni kwa sababu Makristo wamewadanganya wasiwe wateule tukijua ya kwamba YESU mwenyewe alikuja ili aonyeshe njia yake ili uwe Mkristo uzaliwe,uokoke. Tujiulize sasa huu Ukristo unagawanyikaje mara nyingi? Wengine ni Wakristo na wanasema hakuna kuokoka na mbinguni tunakwenda hao shetani hana shida nao anajua ni wake iwe ni mchungaji au ni askofu anajua wewe ni mali yake nakuambia mimi Nabii Hebron huo ndo ukweli, haijalishi unabidii siku ya saba unawahi kanisani kwenye timetable wewe ni Mkristo msafi ratiba zote unahudhuri; ila jiulize wewe ni Mkristo ambaye shetani hakuogopi na hana muda na wewe anajua wewe ni mali yake tayari na dunia hii watu wengi wametekwa kwa kujua na kutokujua, wengi ni mateka wa shetani. Kuwa Mkristo tu haimaanishi utakwenda mbinguni, na kuwa Mkristo siyo kuwa mwana wa MUNGU. Ili uwe mwana wa MUNGU ni lazima umkiri, uzaliwe mara ya pili kwa roho kwa kumkiri.
Yohana 1: 12-13
"Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."
Watu wote waliumbwa na MUNGU lakini MUNGU anataka uwe mwanae, amekupa nafasi umpokee mwanae YESU KRISTO, umkiri siyo ubaki tu wewe ni Mkristo na ukafundishwa ubaki tu kuwa mkristo na kumwamini, napenda nikuambie hata mashetani wanaamini kuwa YESU ni mwana wa MUNGU lakini hawamkiri! Na mambo haya shetani ameleta katika dunia hii, mamilioni wa watu wamekuwa ni Wakristo lakini walete sasa kuja kuwa wana wa MUNGU hapo ni ugomvi, hapo watafungua biblia, hapo watachambua na kuchambua, nakuambia huwezi mfananisha MUNGU na ukoo wako, kazi yako, gari lako, mke wako, na mtoto wako hata na elimu yako. MUNGU ni yeye yule, hata neno la MUNGU halibadilishwi kwa nini mnalibadilisha kama nguo, kama magari? Neno la MUNGU ni lile lile jana leo na hata milele.
YESU alikuwa akipambana na hao Mafarisayo na Masadukayo kwa lugha ya Kiswahili au lugha zetu ndio watumishi wa kanisani; Wachungaji, Wainjilisti, Waalimu BWANA YESU ASIFIWE! Biblia imeshatabiri ya kwamba atazaliwa; yeye akajisema ndiye yeye lakini walimkataa na sikatai maana biblia inasema Nabii hapati heshima nyumbani kwake, hata YESU alipotoka Nazareti badae ndipo wakasema laiti tungelijua. Angalia kina Musa na kina Yeremia. Sasa napenda kuwaambia, MUNGU yeye alimleta YESU ili watu wamwamini kama njia. Atulete kwake kama njia atulete kwake tufanyike kuwa wana, tuwe wateule lasivyo kama isingekuwa hivyo, MUNGU kupitia manabii wake wa zamani angesema muwe Wakristo tu mtafika mbinguni.
Mathayo 24: 23-26
"Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. Tazama nimekwisha kuwaonya mbele. Basi wakiwaambia, Yuko Jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki"
Mimi nilikaa kwenye kambi ya Makristo, nikaamiwa wakiwaambia yuko kule msiokoke, yaani wananifunga tena mimi, walinilisha na kunichunga nisiokoke lakini kwa neema ya Bwana nilitoka nilikuwa siyo Mkristo ambaye shetani ananiona rafiki, nikazaliwa mara ya pili kama kiumbe chake. Na la kujiuliza huu Ukristo mbona una matatizo mengi, wengine wanasema tuokoke tumkiri, wengine wanampinga hakuna kuokoka. Hawa wanaosema hakuna kuokoka hawa ndo Makristo. BWANA YESU ASIFIWE, Ukisoma neno anasema atakuambia sikujui sikujui, utasema ulikuwa kanisani nahubiri yeye atasema sikujui. Na isidhaniwe kuwa hili linawahusu wahubiri tu, hapana, inakuhusu hata wewe ambaye ni mfuasi wa Mhubiri ambaye Ni Makristo yeye ni dreva anakuongoza, unamwamini anakuachia hiyo roho ya Makristo, anakupeleka katika shimo, BWANA YESU ASIFIWE!
Leo kuna Makristo wangapi wanabatiza kwa kikombe, kisima, kwa jina la mchungaji? hao ndo Makristo wanawapoteza. Kuna Makristo pia leo hii ambao hawataki huduma tano za YESU hawataki huduma ya Nabii, hawataki huduma ya Mtume hawa ndio Makristo, ni jina baya sana Makristo. Aliyeanza kusema maneno haya ni BWANA YESU mwenyewe ndo maana baadhi ya watumishi walikuwa watoto wake wengine wakabadilika; haijalishi wanahubiri injili ya namna gani hata Makristo wanahubiri sana mafudisho mengi sana hata kupitia neno la MUNGU lakini roho na msingi itendayo kazi ni ya Makristo. Wakiambiwa wabatizwe ubatizo kama wa YESU hawataki, kuokoka hawataki, sasa shetani haokokagi, sasa kwa nini wewe mwanadamu usiokoke?! Wana wa Israel walifika mahali wakapewa maelekezo; walipotii hata kuweka damu ya kondoo kwenye milango walipona na sasa hivi sisi tumeambiwa tumpokee BWANA YESU ASIFIWE! (Soma Warumi 10: 9-10).
Yohana 14:6
" YESU akamwambia, mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi."
Mtu haendi mbinguni kwa BABA pasipokupitia kwa YESU; hakuna! Anakujaje kwa BABA ni kwa kumkiri, kumpokea BWANA YESU. Mbinguni huendi kwa Ukristo unaenda kwa wokovu; huendi kwa dhehebu, huendi kwa taasisi ni kwa matendo yako kwa imani kusimama na BWANA YESU umpokee leo tena yawezekana ulishampokea BWANA YESU ulishakuwa wewe ni mteule, ukarudi nyuma ukamwacha BWANA YESU wewe ndo unaitwa Makristo pasipokujua na kujua. YESU aliingia kanisani akasema hata mambo ya kanisa kuwa soko, sasa hivi makanisa mengi yamekuwa ni michango ni harambee haya ndio makanisa yanaitwa ya Makristo YESU alikataa lakini leo yamerudishwa halafu unaambiwa MUNGU atakubariki, ninachokuambia siyo MUNGU anakubariki, unabarikiwa na miungu ya Makristo, unabarikiwa na majini ya Makristo. BWANA YESU ASIFIWE. Mtoto mdogo hajaandikiwa kubatizwa, YESU yeye ambaye ndiye njia ambaye ndiye nuru ameachwa. Watu wanaacha nuru ya YESU wanaenda kwenye giza na matokeo yake Makristo wengi wapo kwenye orodha ya kuchomwa moto na watalia na kusaga meno. Kwa maneno yao wanamtaja ila kwa matendo yao hawamtaki. Neno la MUNGU leo hii limebadilishwa na Makristo na watu wengi wanafuata hayo yaliyobadilsihwa kwa kujua au kwa kutokujua na wanaupenda Ukristo ila bado hawajaokoka. Kama bado hujaokoka mimi Nabii Hebron mtumishi wake YESU nakuambia hili neno linakuhusu wewe ni Makristo, unaweza ukachukia lakini acha nikuambie, umedanganywa.
MUNGU ana nguvu, MUNGU ana uwezo sana, anawaangalia wanadamu lakini wakati umefika ambaye napenda niwaambie dunia na mtubu mrejee, dunia nzima watubu tena wafuate sala ya toba, kilichotokea Sodoma na Gomora kisije kikatokea dunia hii. MUNGU akiangalia, wako wapi watakatifu?? Akawaambia Ibrahim hakuna hata mmoja, hakuna hata wawili, hakuna hata watano, hakuna hata ngapi? Angalieni kwenye mataifa makanisa mangapi ni Makristo kwa kujua na kutokujua na wengine wamerithi mafundisho ya uongo, ukisema ukweli wanachukia wanakuloga unamloga YESU. Siku mmoja niliwaambia watu anayetaka kushindana na mimi amuue MUNGU mbinguni, amuue YESU ndipo wataniweza mimi lakini kama unataka faida kalime mchicha, mimi nimetumwa na MUNGU huo ndo ukweli na injili yake siipindishi japokuwa Makristo hawafurahii. MUNGU ameita watumishi wengine wamerudi nyuma, wengine wamekuwa wanafikii, wamekuwa kama masanamu, simama na Bwana, itetee injili, MUNGU akikaa mbinguni akuone. BWANA YESU ASIFIWE! Kwa nini MUNGU alimpenda Ayubu? Kwa nini alimpenda Yusufu? Kwa nini YESU aliwapenda wale wanafunzi wake waliomsikiliza? Na yule aliyemsaliti YESU akawa kwenye Makristo ni Mkristo na alikufa akiwa Makristo. Huyu Kristo YESU, BABA yake amesema tusiabudu sanamu, leo hii Wakristo wanaabudu sanamu. Huyu Kristo BABA yake siyo MUNGU wa wafu, leo hii Wakristo baadhi wanakumbuka waliokufa na kuombea sala za toba na rehema. MUNGU anasema siyo wa wafu kwa hiyo katika ulimwengu wa roho kwa kujua na kutokujua unakua uko kwenye miungu na miungu imevuna sana. MUNGU anavuta, shetani anavuta. Alimwambia Petro kuanzia leo utakuwa mvuvi wa watu na mimi leo hii na mimi amenituma nakuvua wewe uje kwa YESU. Shetani pia anamakristo wake wanakuvua uende kwa shetani na Makristo, wanakutisha ukifa hawatakuzika, hutapata huduma za kiroho. BWANA YESU ASIFIWE!
Napenda ufahamu kuwa siyo mambo yote ya kiroho ni matakatifu; uchawi ni mambo ya kiroho, mazingaumbwe pia ni mambo ya kiroho katika giza. Tulivyoona wakati ule Musa alifanya miujiza yake ni mambo ya kiroho ambao MUNGU alikuwa anafanya kupitia Musa na wakati ule ule, Farao aliwaita wachawi wake wakafanya mambo yao ya kiroho katika giza vile vile. Sasa hapa ninachosema ni mwanadamu amepewa uhuru, democrasia na siku zote MUNGU amempa mwanadamu uhuru; unampenda MUNGU sawa, humpendi sawa lakini anakukumbusha maana anajua umedanganywa Ameniambia "Hebron waambie habari hii ili wakapone maana wengine wamedanganywa na wengine hawajijui" BWANA YESU ASIFIWE! Mbinguni hapatakuwa na dini A,B,C,D na hakuna mtu mwingine aliyeandaliwa kama njia ya kwenda mbinguni ni YESU peke yake. Inakuaje unapokuwa Mkristo mpokee, nenda kwa wateule; ukishaanza kwenda kwa wateule utasikia watu wanapiga kelele wakisema umeikana imani, sema umeikana mapepo katika jina la YESU. Mambo mengine yanatokea MUNGU anaiangalia imani yako, na jaribu la mtu ni tofauti na jaribu la mtu mwingine, lakini napenda ujue kwamba kila jaribu linalokuja ni lazima ulishinde, kuna kitu MUNGU anakuwekea ili ushinde kama ukitii na kumsikiliza.
MUNGU yeye atawachukua wateule, watu ambao wamempokea mwanae kama njia, maana yeye wana umoja MUNGU BABA, mwana na roho mtakatifu siyo kigeugeu, wengine waokoke wengine wasiokoke halafu tutakutana huko, haijalishi unasema sala ya Baba yetu uliye mbinguni, unaweza ukawa unaisema katika Makristo au hata katika miungu. YESU kipindi kile hakufundisha makanisani alifundisha wanafunzi wake waliompokea kama Bwana na mwokozi, alipokuwa anawauliza wanafunzi wake kuwa yeye ni nani, walikuwa wakimjibu wewe ni mwalimu; bwana na mwokozi wangu. Mama yake YESU mwenyewe alikuwa anasema Bwana wangu, Mwokozi wangu; leo hii Maria anaombwa asamehe, asaidie watu, lakini sasa Maria ni mama mtakatifu mzuri sana amefanya kazi kubwa na MUNGU amemteua kiumbe chake. Yeye mwenyewe anamwita YESU Mwokozi wangu; wakati anaenda kumwangalia YESU amefufuka au pale alipokuwa anatesa. Zaidi mimi nilikwisha ongea na Maria uso kwa uso, akasema kwa nini wanadamu wananiabudu mimi? Mimi sina nafasi hiyo, mimi sistahili. Mimi mwenyewe Hebron ninamwambudu YESU mwanangu ninamsujudu, mimi ni nani? wamepotea. Nimeshawaeleza kwenye makala mbali mbali na kazi aliyoianzisha MUNGU mwanadamu asiipinge. Huyu MUNGU ni MUNGU wa maonyo ni MUNGU wa marejesho lakini kuna ambao hata waambiwe kitu hawatakaa wabadilike maana wametoka kuzimu na ni wanadamu na wanaroho mbaya sana ni wauaji kiroho sababu mtu anayekufundisha uongo kiroho tayari ameiua roho yako isiwe na uzima wa mwenyezi MUNGU pasipokujua na kujua.
Kuna wengine wanaona msalaba ndo Ukristo hapana. Msalaba ni kitu ambacho siyo ishara ya Kristo maana YESU hafanani na msalaba. Msalaba toka zamani ilikuwa ni kitu cha kuwaulia wahalifu; aliuliwa pale ili damu yake idondoke na sisi tusihukumiwe maana dunia ilishachafuka, kupitia yeye tukombolewe. Mslaba ingekuwa ni Kristo isingeliwa na mchwa na makaburi yasingeingilika na wachawi. BWANA YESU ASIFIWE! Sasa fahamu shetani hahangaiki na Mkristo bali anahangaika na mteule. Sasa leo karibu uwe mteule na wewe pia katika kumkiri na kumpokea BWANA YESU kama Mwokozi wa maisha yako.
SALA YA TOBA:
SEMA BWANA YESU NAOMBA UNISAMEHE DHAMBI ZANGU ZOTE NILIZOZIFANYA KWA KUJUA NA KUTOKUJUA, ULIANDIKE JINA LANGU KATIKA KITABU CHAKO CHA UZIMA WA MILELE. NAMKATAA SHETANI NA MAMBO YAKE YOTE, BWANA YESU NIMEJIKABIDHI KWAKO. AMEN.
Baada ya hayo maneno anashuka roho mtakatifu na unaanza kuwa kiumbe kipya. Hatua inayofuatia unaenda kufa na YESU na kufufuka na YESU kwa njia ya ubatizo unakuwa kiumbe kipya; mizimu inakufa, majini, mapepo unaanza kusonga mbele. Tunza sana Ukristo wako wa uteule na kukataa roho za Makristo.
PROPHET HEBRON WILSON KISAMO.