KUFANYA
SHEREHE ZA MAZAO KANISANI NI KUMKUFURU MUNGU, YESU, ROHO MTAKATIFU NA MBINGU!
BWANA YESU ASIFIWE, MUNGU
anayewapenda watu wake aliowaumba amenituma niwaeleze ili wale watakaopenda
kusikia wapone na watakao kaza shingo watakutana naye kwa mapigo ajuavyo Yeye.
Kama nilivyokwisha kusema awali, YESU alishasema watakuja waongo ili kuwapoteza
hata wale wanaoenda mbinguni ili waende jehanamu pasipo kujua kwa sababu
shetani na yeye anazo mbinu zake na mipango yake ya siri ambayo imefichika
katika nchi zote ambapo jina la YESU na hata jina la MUNGU linakuwa likitumiwa
vibaya, wakati hata MUNGU mwenyewe hasikii. Nataka muelewe unapofanya kitu
ambacho MUNGU amekataa halafu mkamtaja Yeye haji na badala yake shetani ndio
anakuja kwa sababu ndilo lake.
Nataka uelewe kuhusu sherehe za
mavuno zinazofanyika baada ya watu kuvuna mazao yao na kwa nini sherehe hizi hazifanyiki
kipindi cha masika. Katika sherehe hizi wanakuwepo pia madalali (ambao ni wazee
wa kanisa). Kufanya sherehe hiyo ni dhambi kwa sababu mnamnyima mkulima uhuru
wake wa kumtolea MUNGU fungu lake la kumi, na badala yake mnalinadia fungu lake
la kumi. Hii haina tofauti na mfanyakazi au mfanya biashara fungu lako la kumi
unalomtolea MUNGU sadaka ukalipeleka kanisani halafu akaja dalali akaanza
kusema, kwa mfano umetoa 10,000 igombaniwe na atakayeibuka kwa pesa zaidi mfano
hiyo 10,000 ukapanda mpaka 20,000 ikabakia hapo kanisani, hapo bado utakuwa
haujamtolea MUNGU fungu la kumi.
Mkulima anavuna mazao yake na akatenga
kiasi fulani ni cha MUNGU anauza na atapeleka kanisani, sasa ukipeleka hayo
mazao yakafanyiwa mnada uelewe ya kwamba haukumpelekea MUNGU bali ulipeleka
sokoni kwa hiyo usimdai MUNGU. Huo ndio ukweli, neno lifuatwe kama lilivyo,
kanisa halipaswi kufanya mnada kwenye mafungu ya kumi ya watu, ila kama ni
mpinga kristo, wao wataendelea kwa sababu hiyo ni sheria ya roho iwaongozavyo. YESU
alikataa, mbona sasa inafanywa kuwa ni sherehe? Ina maana YESU anapuuzwa (Soma Marko 11:15-18). MUNGU analiangalia Neno
lake, MUNGU anapaona hapo ni sokoni na siyo ibadani, bali mpinga kristo yeye
anapaona ni kanisani.
Angalizo:
Jiulize
tokea lini sadaka ya mtu anayemtolea MUNGU ikaletewa dalali ainadi? Pia zipo
sadaka ambazo ni zakupandia kiwango au dau ambazo wanasema ni sadaka za sanduku
la agano, hizo hutembezwa katika baadhi ya nyumba za watu halafu atakayetoa
sadaka za kiwango au pesa nyingi kama mashindano ndiye anayepewa hicho
kisanduku cha agano ila pesa yote inachukuliwa na mtumishi, huu ni wizi na ni
utapeli, hata mnaotoa mjue ni kama mmetupa kwenye choo. Hizo ni mbinu za baadhi
ya watumishi ambao wapo kinyang’anyi na siyo kwa mapenzi ya MUNGU, wakitumia
jina lake YESU. Kwa wale ambao hawakujua, sasa mpone na uwatumie na wengine
ujumbe huu au elimu hii ya kweli kwa sababu hawajui ukweli. Na sadaka hizo
hutengenezewa visanduku na kila mwisho wa wiki (weekends) hukutanika kwenye nyumba za waumini wakifanya huu utapeli
eti mashindano na atakayetoa kiwango cha juu zaidi yeye atabakia na sanduku la
agano kama lile la wana wa Israeli na eti atafanikiwa kwa kila jambo.
NABII
HEBRON WILSON KISAMO.