HIKI
NDICHO KIPINDI ANACHOTUMIA SHETANI NA WATUMISHI WAKE KUPIMA MAENDELEO YA KIROHO
YA MUUMINI AMBAYO MWISHO WAKE NI JEHANAMU
Katika nyakati hizi baadhi ya makanisa
au watumishi wengi hupenda kujua taarifa za watoaji, njia zao wanazotolea na
viwango vyao wanavyovitoa tofauti na Mwenyezi MUNGU anavyoelekeza, ambaye Yeye
anasema kumtolea ni siri kati Yake na mtu anayemtolea.
Soma Mathayo 6: 2-4; 2 Kwa sababu hiyo wakati unapotoa zawadi za
rehema, usipige tarumbeta mbele yako, kama vile wanafiki wanavyofanya
katika masinagogi na barabarani, ili watukuzwe na watu. Kwa kweli ninawaambia
ninyi, Wanapata thawabu yao kwa ukamili. 3 Lakini wewe, unapotoa zawadi za rehema, usiache mkono wako wa
kushoto ujue lile ambalo mkono wako wa kuume unafanya, 4 ili zawadi zako za rehema zitolewe katika siri; ndipo
Baba yako anayetazama akiwa mahali pa siri atakulipa.
Ni lazima ujiulize ni kwa nini
watu katika baadhi ya makanisa na sehemu za ibada wanaambiwa waandike majina na
kiasi walichotoa, wakati MUNGU ameeleza bayana unapomtolea iwe siri, sasa hao
watumishi wanaowaeleza waumini waandike majina na kiasi walichotoa, je wao ni
zaidi ya MUNGU au wao ndio wanamfundisha MUNGU njia yao wanayoitaka? Jibu analo
afanyayo hayo. Mtu huyo imeivunja sheria ya MUNGU hadharani na ikawekwa sheria ya
shetani ndani ya kanisa, huko ndiko
kumfukuza MUNGU katika ibada. Na jambo hili limeanzishwa na baadhi ya
watumishi waliotokea kuzimu au wenye asili ya uchawi ili kuibia watu pesa zao na
nguvu zake siyo Roho Mtakatifu.
Cha kujiuliza, kama Kamanda
mwaminifu kwa Jemedari wake ameteuliwa kufanya kazi fulani na amepewa maelekezo,
Kamanda huyo mwaminifu hufanya hivyo hivyo kwa uaminifu kama alivyoelekezwa, lakini
cha ajabu baadhi ya makamanda wa kanisa siyo waaminifu kwa Jemedari wao ambaye
ni YESU, wengi ni waasi na wanyang’anyi kwa kutumia jina la YESU.
Mimi nimetumwa na aliyeumba
kila kitu niyaseme haya na mengineyo ili ukweli ujulikane katika yeye. Hii siyo
njia ya kumpima muumini kiroho kwa kuangalia vipato vyake kwa njia ya sadaka na
kumpa risiti, na pale asipotoa mchungaji huangalia taarifa (report) yake na akiona anachokipata
kimepungua hivyo anarudi kwenye daftari au computer
zilipoandikwa taarifa (reports) za
sadaka akikuta watu hawajatoa viwango vilivyozoeleka unapigiwa simu au kufuatiliwa
na hatimaye utaelezwa eti roho anaumia kwa nini haumtolei, kumbe anakua ameshaangalia
taarifa zako na matoleo ya jinsi hiyo. Napenda muelewe hizo zote siyo sadaka na
wala hazipokelewi na MUNGU, Yeye anaangalia Neno lake, haijalishi Biblia
itasomwa. Hizo siyo sadaka tena, soma Neno linaeleza bayana.
Katika hizi theolojia yapo mambo mengine ni mabaya ambayo
watumishi wanafundishwa na kuyapokea ili yazidi kuwafanya waangamie wakifuata mapokeo
ya wanadamu. Soma Biblia, YESU ameshatoa sheria ili ifuatwe kwa nini haifuatwi?
Elewa kwamba hizo ni roho nyingine. Na sehemu nyingine ukiacha kutoa mwezi
mmoja wanaangalia ripoti yako unaambiwa umezimia kiroho na usipotoa tena mwezi wa
pili fungu la kumi hapo unaambiwa umekufa na sasa wewe ni maiti na watu wanaamini
hayo ni kweli kwa sababu Biblia inasomwa na YESU anatajwa. Sasa pasipo kujua au
kuelewa wanadanganywa na wanafanyika kama vitega uchumi vya mtumishi kwa sababu
yeye anayo maagano yake ya nguvu ya kishetani hivyo ili kanisa liendelee ni lazima
ijulikane na mchungaji umetoa ngapi.
Napenda muelewe hakuna mtumishi
yeyote anapaswa kukufuatilia umetoa kiasi gani, sadaka ni ibada yako na ni siri
yako kati yako na MUNGU tu. Ukitoa kwa jinsi hiyo bado umetupa kwa shetani na
hata kama umetoa bila kuandika jina katika madhabahu hiyo bado utakuwa unampa
shetani kwa sababu hiyo ni madhabahu yenye roho ya kumpinga MUNGU kwa kupindua
Neno lake au kwa lugha nyingine ni madhabahu ya kumpinga MUNGU atakavyo Yeye,
hivyo MUNGU hana uhusiano kabisa na sehemu hiyo. Zaidi fuatilia masomo ya Nabii
Hebron katika blog yangu ufunguliwe
zaidi na utakuwa huru. Sasa unafunguka, ubarikiwe na YESU.
NABII
HEBRON WILSON KISAMO.