JINSI
YA KUJUA MCHUNGAJI ANAYEONGOZWA NA ROHO WA UONGO
NA
SIYO ROHO WA MBINGUNI
Shalom watu wote wa MUNGU wa mataifa yote, hiki ni kipindi
cha mwisho ambacho tunamsubiria YESU aje kulinyakua kanisa, yaani yeye
aliyeokoka na kuishi katika maisha matakatifu ndiye atakayechukuliwa, kwa
sababu ndivyo alivyosema hata katika Neno lake, na Neno lake ni kweli, hasemi
uongo na wala siyo kigeugeu na habadiliki bado atabakia kuwa MUNGU katika
nafasi yake ile ile. YESU mwenyewe amesema bayana, angalieni watakuja wakitumia
jina langu, watawadanganya wengi wakitumia jina langu. Hao ambao YESU anawataja
watawadanganya watu wengi ni wachungaji au wanaoitwa au wanaojiita kwa jina la
YESU, baadhi yao ni waongo ila imekuwa ni vigumu kwa mataifa kuelewa huu uongo.
Nitaelezea kuhusu uongo wa kutumia Biblia ambacho ni Kitabu Kitakatifu
na jinsi ambavyo watumishi hao ambao ni waongo ambapo aidha kwa kutumia nafasi
zao au madhabahu zao, wanapoamua kuchanganya ukweli na uongo katika huduma za
kiroho wanazozifanya. Kwanza nataka muelewe kwamba MUNGU yeye siyo mwongo, yeye
ni mkweli muda wote, bali shetani yeye ndiye mtengenezaji wa roho za uongo au
nguvu za uongo. Na pia kila mtu aelewe kwamba huyu YESU jina lake ni zuri sana
na mtu akilitaja huwa anaaminika ni mtu safi, sasa wapo waongo wanaolitumia
jina hili pasipo watu kujua Biblia inasema nini juu ya haki zao kutoka kwa
MUNGU, hudanganywa na wachungaji waongo. Nasema waongo kwa sababu mchungaji
utamjua kwa matendo yake anayoyafanya au injili anayoifundisha, je ni kweli
tupu anayofundisha au anachomekea na uongo ili aibie watu mali zao au awapeleke
watu jehanamu! Mchungaji akiwa kipofu hata wewe muumini utakuwa kipofu, labda Neema ya MUNGU ikusaidie utoke kwenye
upofu huo. Ukijua ukweli kama mchungaji au mtumishi anafundisha uongo na ukamweleza
atachukia kwa sababu umejua kwamba yeye ni kipofu, sasa badala ya yeye kukubali
na kuacha uongo atakuchukia kwa sababu yule roho wa ibilisi aliyopo ndani yake
atajua umemjua na hivyo hakupati tena.
Nitaelezea mifano michache ambayo baadhi ya watumishi
wanasema uongo na wamejawa na roho wa shetani, na kama wamejawa na roho ya
uongo basi wanaongozwa na shetani. Wapo wanaojijua na wengine hawajijui na
ndipo ile siku ya mwisho YESU anasema watalia na kusaga meno, naye YESU atasema
sikujui sikujui. Je wewe umeshafikiria ni kina nani hao? Baadhi yao ni
watumishi na wengine wanao fanana na hao. Mfano, MUNGU anasema muwaombee watu
na msiwatoze watu pesa za maombezi, sasa anapotoza watu pesa na kusema eti MUNGU
anawaagiza watoe kiasi Fulani, Je hapo hamuoni huo ni uongo mkubwa uliokithiri na
watu hawalijui hilo! Baadhi wanaziita hizi tozo (charges) sadaka na watu
pasipokujua wanaamini na kumbe unaibiwa na hautapata baraka yeyote toka kwa
MUNGU, bali utaendelea kufilisika na kuangamia wakati huyo mtumishi akiendelea
kufaidi matunda ya unyang’anyi na mwisho atatupwa jehanamu. Huo ndio ukweli
YESU ameniambia kila anayesema uongo kuhusu Yeye tofauti na Neno basi mwisho
wake ni jehanamu, hata mimi Hebron tokea aniite aliniambia usije ukamtoza mtu
pesa ndipo umwombee, ukifanya hivyo utachomwa moto. Nawaeleza watumishi msiojua
hilo na mkaiga wale waliojiunga na muovu, msipo acha sasa, mtachomwa moto
jehanamu, na kila anayetoza watu pesa ajijue anayo ticket ya Jehanamu mkononi mwake, kwanza yeye ni mwizi anawazuia wengine
wasiende mbinguni, yaani ukiongozwa na mtumishi anayewatoza watu pesa uelewe
anakuambukiza na wewe roho ya kukuzuia kwenda mbinguni kwa sababu yeye haendi.
Jinsi alivyo mtumishi na ndivyo alivyo na kondoo, soma Mathayo 23:13.
Jambo jingine ambalo liko wazi kabisa, YESU alisema kila
anayetaka kupona na jehanamu ni lazima aokoke sasa iweje baadhi ya watumishi
katika dunia hii wanawazuia watu wasiokoke bali wajiite wakristo tu bila wokovu,
sasa kama una masikio na usikie, hawa hawaendi mbinguni kabisa na wanawazuia
watu wasiokoke ili nao wasiende mbinguni. Ona basi, wao hawataki kwenda halafu
wanawazuia na wengine wasiende. Sasa muelewe watu mnaotaka kwenda mbinguni, wokovu ndiyo ticket yako ya kwenda mbinguni na kama haujaokoka uelewe unayo ticket ya kwenda jehanamu. Hapo
unafungiwa katika gereza la shetani, unapigwa upofu ili uone upo salama kumbe
tayari umekufa kiroho. YESU anarudi, maneno haya usiyadharau, okoka sasa achana na waongo wanaokuzuia
usionane na MUNGU aliyekuumba, yeye anakuhitaji, mkatae mpinga kristo na uongo
wake. Hata kama mtumishi ameokoka halafu anawatoza watu pesa bado na yeye ni
adui wa MUNGU na shetani ndiye rafiki yake. Dunia, huu ni wakati wa kila mtu
kujua ukweli ili apone roho yake na ndoto zake zije kutimia, kuwa siku moja
ataenda mbinguni na atafika, badala ya kwenda jehanamu.
YESU alibatizwa kwenye mto, Yohana alifanya kama alivyotumwa
na MUNGU, sasa nauliza mataifa yote ni nabii gani alitumwa kutoka mbinguni tuje
kubatizwa na maji ya kikombe, au maji ya kisima au kubatizwa kwa bendera au kwa
jina la mchungaji au kwa vumbi au kubatizwa kwenye beseni? Jibu hakuna, je kama
katika Biblia hakuna sasa huoni hiki ni kipimo cha wazi kuona jinsi uongo
ulivyopokelewa na upo juu ya vichwa vya mamilioni ya watu wakifikiria ndiyo
agizo la MUNGU kumbe siyo na kama siyo basi ni uongo. Watu hawajabatizwa kwa
mpango wa kweli wa MUNGU aliyeumba mbingu na nchi, hivyo yeye hana uhalali na
wewe kwa sababu umepokea kiapo cha mungu asiyejulikana na kukufanya ubakie kwa
huyo asiyejulikana yaani shetani pasipokujua au kwa kujua. Basi ili mpone
mataifa yote ni lazima uokoke, hakuna njia nyingine zaidi ya hiyo, hizo
nyingine zote ni za uongo na zitakuangamiza. Ninapoandika ujumbe huu nasikia
sauti ya YESU ikinieleza haya niyaandikayo kwako wewe kwa taifa lako na kwa
sura yako. Wokovu ni lazima kama unataka
kwenda mbinguni na ubatizwe kama Yeye YESU na siyo tofauti. MUNGU habadiliki (soma
Ufunuo 22: 18-19). Badilikeni sasa
mataifa, okokeni, YESU anawapenda, anajua watu wamedanganywa sana na wanampenda
ila hawajui ukweli kuhusu YESU anavyotaka.
Imeandikwa, kanisani ni mahali patakatifu sasa cha ajabu kwa
baadhi ni sehemu ya masoko, na pia hata sadaka za fungu la kumi la mazao ya
watu imefanywa ni siku ya sherehe, basi wafanye na siku za sherehe za mishahara
wawapige watu upofu na cha kusikitisha zaidi siku za sherehe ya mazao wanakuja
madalali kufanya mnada katika nyumba ya sala wakitumia jina la YESU, huku ni
kumchafua YESU, kumdharau MUNGU na Yeye hakai na watu wa jinsi hiyo.
Zaidi endelea kusoma makala za Nabii Hebron, utajifunza
mengi na utawekwa huru, ila WOKOVU
ni LAZIMA. Tubu sasa, sema, BWANA
YESU naomba unisamehe dhambi zangu zote, unisamehe kufuata uongo kwa kujua au
kutokujua, sitaki tena kushiriki dhambi, uandike jina langu katika kitabu chako
cha uzima wa milele. Amen.
NABII
HEBRON WISLON KISAMO.