Pages

Thursday, May 3, 2018


KWA NINI WATU WANABATIZWA KWA KUTUMIA BENDERA?

BWANA YESU ASIFIWE, hapa tutajifunza siri ya ufalme wa shetani ambayo baadhi wakristo wanabatizwa kwa kutumia bendera. Ukisoma Biblia, ubatizo uliopo na unaotambulika ni wa Yohana tu, japo zikaja batizo nyingine ambazo zote ni tofauti na Yohana alivyobatiza, ambazo hizi zote ni za uongo. Ninaposema ni za uongo nataka uelewe kwamba batizo hizo ni za mapokeo ya wanadamu. Hivyo basi yakupasa uelewe ya kwamba hata ukibatizwa kwa jinsi hiyo, bado YESU hakutambui kama umebatizwa, haijalishi lilitumika jina lake. Soma Mathayo 15: 5-9, mnaniabudu bure, ni wanafiki; haya maneno YESU aliyasema ili watu wajue unapofuata mapokeo, hata uombeje ni kazi bure, hata kama umeokoka yeye hakutambui, zaidi unabakia kuwa kama mnafiki kwake japo wewe unakua haujui ukweli; au unajijua umetekwa na shetani au mpinga kristo pasipo kupenda au kujua.

UBATIZO WA BENDERA (FLAG)
Huu ni ubatizo ambao umeshaingia katika dunia hii, haujatokea mbinguni kabisa, kwanza hawatumii maji yoyote hata tone, bali inawekwa bendera mbele yako na mchungaji (pastor) anayekubatiza anaitwa captain. Kitu cha ajabu jiulize, YESU hakuleta captain ndiyo liwe jina la mchungaji, bali mchungaji ni mchungaji. Hapo tayari si sahihi (it’s wrong). Pia nataka mjue kwamba kazi ya bendera ni kwa ajili ya ufalme wa kidunia, ndiyo hutumia bendera kimwili, ila kiroho kanisa halipaswi kuwa na bendera yoyote ile, na kanisa linapokuwa na bendera uwe makini sana na bendera hiyo, kwa sababu inakujulisha ni huduma ambayo mwanzilishi wake alipewa afanye hivyo kama agano na anapoweka bendera basi shetani anaimarisha hilo kanisa na mapepo na majeshi yake.

Sasa watu wanashindwa kuelewa na kujiuliza, mbona Biblia inatumika na jina la YESU linatajwa mahali hapo? YESU mwenyewe alishasema, tena watawateka hata wateule wakitumia jina langu; wateule ni watu wanaopenda kuokoka, wengi wameshatekwa na shetani wasiende mbinguni ila kiongozi au mwanzilishi yeye anajua anachokifanya. Mtu anapobatizwa kwa kutumia bendera na anayeitwa captain (mchungaji) hushika bendera na anayebatizwa hupita mbele ya bendera na kusimama na kupiga saluti akiangalia bendera, na mengineyo; eti hapo tayari anakuwa amebatizwa, naomba usicheke, hivi ni vituko au masaibu ya kumchezea YESU. Inasikitisha na mimi nawaeleza kila aliyebatizwa kwa kiapo cha bendera hataenda mbinguni bali anaenda jehanamu na zaidi ameshajiingiza katika maagano asiyoyajua ambayo yatamtesa maisha yake kwa sababu ametii kiapo cha miungu na miungu inakua na uhalali naye. Hivyo basi, ili upone ubatizwe haraka ubatizo wa Yohana na achana na madhabahu hizo kabisa.

Ujumbe huu ni YESU ndiye aliyenipa ruhusa niulete kwa mataifa yote na wewe unapoupata utume kwa wengine ili wasije wakapelekwa jehanamu kwa sababu hata wanaobatizwa hivyo baadhi yao wamefundishwa kuamini hivyo na wala hawajui kuwa kilicho mbeleni ni jehanamu, na siku ile ya mwisho hakuna cha kujitetea. Toka sasa utubu, upate neema ya kuokolewa na ujitenge na huu ubatizo, ubatizwe kama YESU kwa maji mengi yanayotembea, zaidi soma kitabu cha “Ubatizo wa Kweli kwa Ulimwengu Wote”. Fungua www.prophethebron.or.tz na ingia katika blog na YouTube ujifunze mengi.

Sema; BWANA YESU, naomba unisamehe, dhambi zangu zote nilizozitenda, unisamehe na dhambi hii ya kubatizwa kwa bendera ambayo nimejidanganya kabisa, kwa sababu neno ubatizo ni kuzamishwa na mimi hata sijazamishwa ninakuwa mpinzani, nilisimama kama askari akipiga saluti pasipokujua au kwa kujua. Uandike jina langu, katika kitabu chako cha uzima wa milele, ulitoe kabisa kweye jina la mapokeo ya wanadamu. Uniongoze nikabatizwe kama wewe ili niwe mwanafunzi wako ambaye si mnafiki. Amen.

NABII HEBRON.