Pages

Monday, April 23, 2018


JINSI GANI MTU ANAWEZA KUMPA SHETANI MAISHA YAKE BILA KUJUA WALA KUPENDA?
(KWA KUOKOKA)

BWANA YESU ASIFIWE! Nafikiri wengi watashangaa haya ninayoyaelezea, zipo njia nyingi ambazo mwanadamu anaweza akampa shetani maisha yake huku akijua kabisa, kwa mfano, kujiunga na freemason na mengineyo. Ila hapa naelezea kumpa shetani maisha yako kupitia kutumia jina la YESU. Hata YESU mwenyewe alishasema watakuja watumishi wengi wa uongo na watatumia Jina lake kuwapoteza hata wateule. Hapa nitaelezea jambo moja, japo mengine mengi nitaendelea kuyaelezea jinsi YESU alivyonifundisha na kunijulisha njia zao ili niwaeleze mataifa wakapate kupona.

Njia yenyewe ni hii, shetani na yeye anatumia neno hili hili kuwateka wateule. Wateule ni watu ambao wanapenda kuokoka au wameokoka. Maana ya kuokoka ni kumpa YESU maisha yako awe BWANA na mwokozi wa maisha yako, ukisoma katika kitabu cha Warumi 10: 9-10.

9Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. 10Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.”

Sasa kupitia neno hili hili ndio njia aliyoileta YESU kwa ajili ya mwanadamu kwa kumpa maisha yake kwa kuokoka, na kuokoka huja kwa kikiri kwa kinywa chako yale maneno ya toba unayoongozwa na mtumishi wa MUNGU wa kweli, ikiwa unaongozwa sala hiyo ya toba kikweli na Mtumishi ambaye MUNGU amemchagua na anamtumia, hapo utakuwa unampa YESU maisha yako kuwa BWANA na mwokozi wako. Ila ikiwa umeongozwa sala ya toba na mtumishi freemason kupitia sala ile ambayo ndio kiapo, unakua umemkiri shetani, haijalishi limetumiwa jina la YESU, kimsingi bado utakuwa haujaokoka bali utakua umeokoka ili uende jehanamu au unakuwa umempa shetani maisha yako, na ndio sababu Biblia inasema wengi watalia siku ile wakisema niliokoka na atawaambia siwajui ninyi. Hii ni sababu moja wapo.

Sababu nyingine ni kuongozwa sala ya toba na mtumishi aliyegeuza nyumba ya MUNGU ni sehemu ya biashara, anatoza watu pesa za maombezi, kubatiza kwa kisima au kubatiza kwa maji ya kikombe au kubatiza kwa jina la mchungaji au kubatizwa kwa bendera. Haijalishi hata ukibatizwa na maji mengi kama YESU wakati kanisa linatoza watu pesa na kwenda kinyume na YESU bado hao watu wote watakuwa wameunganishwa maisha yao na shetani, sababu jinsi alivyo kuhani ndivyo muumini alivyo.

Yapo mambo mengi yaliyoingizwa katika kanisa na wanadamu huku wakiyatoa yale au kuyapunguza yale yaliyopigwa muhuri na MUNGU kwa sababu shetani anajua watu wanakimbilia kuokoka ili waende mbinguni. Shetani na yeye amezaa watumishi wengi na kuwapa wokovu wa kupeleka watu jehanamu. Asilimia kubwa ya wahubiri duniani kote wengi wametengenezwa na waganga wa kienyeji kwa njia za masharti. Sasa jiulize toka lini Mtumishi wa MUNGU akatengenezwa na mganga wa kienyeji? Jibu umelipata. Yamkini hata baadhi ya mnaosoma ujumbe huu mnaenda kwa waganga, adhabu ya MUNGU inawasubiri na zile Ole zote. Unaweza ukaongozwa sala hii na mtumishi ambaye labda hapo mwanzoni kweli alikuwa anatumiwa na MUNGU lakini baadaye akaasi akaenda upande wa shetani na bado anashika biblia na anahubiri sasa uelewe hiyo injili yote anayoihubiri hata kuwaongoza watu sala za toba kwa njia hiyo anakuwa anawaunganisha wanadamu kumpa shetani maisha yao sababu roho iliyopo ndani yake siyo ya MUNGU ni roho nyingine itendayo kazi, kama ni hivyo basi watu wote wanaongozwa sala hizo majina yao yanakuwa  yanaandikwa katika kitabu cha uzima na mateso ya milele na mahali jina lako lilipo ndipo utakapoenda.

Jambo hili linauma sana na YESU akiangalia dunia hii anajikuta hana watu wengi wanaoenda mbinguni. Aliponiita mwaka 2010 aliniambia 98% ya watu wote wapo chini ya ufalme wa shetani, ni asilimia mbili (2%) tu ndio watu wake, sasa fikiria mikutano ya injili ilivyo mingi dunia yote, watu wanavyookoka na wanaongozwa sala ya toba, lakini ni asilimia mbili tu. Sasa mwenye akili na ufahamu na uelewe, uwe makini. Sio kila mtu anayekuongoza sala ya toba atafanya jina lako liandikwe mbinguni. Hata kibinadamu, hauwezi kwa mfano ukaenda kukata ticket ya ndege kwenye ofisi ya baiskeli wakati wao wanahusika na baiskeli tu, hiyo ticket ukienda nayo uwanja wa ndege (airport) watakurudisha nje kwa sababu hawamjui huyo wakala na hivyo ndivyo ilivyo, watumishi wengi zaidi kwa kipindi hiki cha mwisho siyo mawakala wa MUNGU na kama siyo mawakala wake basi ni mawakala feki (batili) kwa hivyo kila utakachofundishwa ni feki (batili), hautaupata uhalisia wa MUNGU na badala yake utakuwa mwana wa miungu. Kama ni sadaka utakuwa unawapa miungu na kukufanya uzidi kumkosea MUNGU zaidi pasipo wewe kupenda wala kujua, ndio sababu amenituma Nabii wake niwaeleze mambo haya ambayo najua shetani na kila roho iliyopo ndani ya mawakala wa shetani hawafurahii bali wale mawakala wa MUNGU wanafurahi na kumtukuza MUNGU kwa sababu wanazidi kuujua ukweli. Ukiongozwa sala ya toba na mchungaji ambaye anadai watu pesa za kumwona ofisini, au pesa za kupangiwa sehemu za kukaa mbele, au kutozwa pesa ili uombewe na tena unapangiwa kiasi cha kutoa jua tayari umeunganishwa na safari ya jehanamu. Jamani mataifa, someni Biblia, mawakala wa shetani wamejaa kila mahali. Wenye MUNGU hawatozi pesa kwa ajili ya maombi, atakuombea bure kwa sababu juu yake ipo roho ya MUNGU ina upako wa mafuta, ila wenye kutoza pesa juu yao ipo roho ya miungu, roho ya ulafi, wizi na unyang’anyi, na ndiyo roho itendayo kazi ikitumia jina la YESU kuwapoteza na kuiba mali za watu.

Hivyo basi kama una uelewa, uelewe zaidi na upime, tokea lini roho ya giza ikampeleka mtu mbinguni? Jibu ni kwamba itakupeleka gizani na hata sasa inabidi watu wengi waokoke upya, watafute mchungaji wa kweli ili majina na maisha yao waliyokiri pasipokujua au kupenda walipo ongozwa sala hizo na kumpa shetani maisha yao na miili yao itoke huko la sivyo watabakia katika mahekalu ya mateso na shida badala ya baraka na ushindi. Na hii ndio sababu unakuta mtu ameokoka lakini analogeka au ameporomoka maisha yake na yupo katika wokovu.

Angalizo:
Ujumbe huu na maneno haya aliyonieleza YESU yawasaidie mnaompenda YESU mkawekwe huru. Ikiwa ulitubishwa sala za toba na watumishi wa jinsi hiyo uelewe hauendi mbinguni, ticket yako ni feki. Yakupasa kutubu upya.

Sema, BWANA YESU, naomba unisamehe, dhambi zangu zote, ukiondoa jina langu kwa miungu, uondoe maisha yangu niliyompa shetani pasipokujua au kwa kujua nikaongozwa sala ya toba na mtumishi ambaye wewe unamjua siyo wako akaniapisha kiapo cha wokovu wa shetani, nayafuta maneno yote ya toba hiyo, hivyo naanza upya mimi kwa jina langu­­­­ (taja jina lako), natubu naomba rehema, nakupenda YESU, nakukabidhi maisha yangu na mwili wangu kuanzia sasa na milele, wewe ndiye BWANA na mwokozi wa maisha yangu, uandike jina langu katika kitabu chako cha uzima wa milele, nikae kwako milele. Najitenga na sala za toba za kuniteka niwe mfuasi wa shetani. Asante YESU, Amen.

Ubarikiwe, nakuombea kila mara ufunikwe kwa Damu ya YESU.

NABII HEBRON.



USISAHAU KUSUBSCRIBE YOUTUBE CHANNEL
 YETU YA PROPHET HEBRON KWA KUBONYEZA LINK HII https://www.youtube.com/prophethebron?sub_confirmation=1 KUTAZAMA
 VIDEO ZAIDI