INJILI ZA MAPOKEO YA WANADAMU ZINAWAPELEKA WATU JEHANAMU
BWANA YESU WA NAZARETI ASIFIWE! Katika
makala hii nitaelezea zaidi kuhusu mapokeo ya wanadamu yalivyo na madhara kwa
mkristo au mtu yeyote yule unayeyakubali au unayeyafuata ili kumtafuta MUNGU.
Mathayo
15: 5-9 “5Bali
ninyi husema, Atakayemwambia babaye au mamaye, chochote kikupasacho kusaidiwa
na mimi ni wakfu, 6basi asimheshimu baba yake au mama yake.
Mkalitangua neno la MUNGU kwa ajili ya mapokeo yenu 7Enyi wanafiki,
ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, 8watu hawa
huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami, 9Nao waniabudu
bure, Wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu”.
Katika neno hili alilolitamka YESU, ‘Enyi
wanafiki”! Sasa jiulize ni nani anayeitwa mnafiki na YESU? Mnafiki ni mkristo
asiyeyafuata yale aliyoleta MUNGU, huyu ndiye mnafiki anayesemwa na YESU, sasa
wewe jipime, utajijua kwa matendo yako, je wewe ni mnafiki au la!!
NINI
MAANA YA MAPOKEO YA WANADAMU?
Mapokeo ni kitu ambacho sicho halisi bali
ni kitu cha kuchomekewa au kuunganishwa na neno ambalo silo linalostahili
ambalo neno hilo linakuwa limeletwa na wanadamu na siyo MUNGU, utajiuliza kivipi?
Kila mtu anajua Biblia ni kitabu kitakatifu na kitabu hiki amekileta MUNGU,
nikimaanisha yale yote yaliyomo ndani ni Yeye MUNGU kaleta ili wanadamu
tuyafuate na zaidi akasema katika kitabu cha Ufunuo 22: 18-19, kisiongezwe chochote wala kupunguzwa. Sasa basi ikiwa
mkristo ataongezewa mambo ambayo hakuyaagiza Mwenyezi MUNGU basi hapo mtu huyo
atakuwa ameleta mapokeo ya wanadamu na mtu yule ambaye atayafuata na yeye
atakuwa sasa anawafuata wanadamu na siyo MUNGU, na jambo hili watu wengi
hawalifahamu na linawafanya kibiblia kuwa wanafiki kwa YESU pasipokujua na
wengine wakijua kabisa ni wanafiki wenye roho ngumu wasiosikia na kutubu na
kuachana nayo.
Swali, kwa nini YESU anasema mnaofuata
mafundisho ya wanadamu mnaniabudu bure, hili neno lina maana kubwa sana na mimi
Nabii wake nataka nikufunulie hili neno. Ina maana kwamba haijalishi unajiita
ni mkristo au umeokoka au unafunga au ni mtumishi, mfano ni mchungaji, lakini pasipo
kuachana na kazi unayofanya au unachokiabudu, hata sadaka unazozitoa bado YESU
hakuhitaji anakuona wewe ni mnafiki kwake. Sasa ni bora uelewe ili upone na
unafiki uliokuwa haujui ukutoke kabisa.
Kwa wewe ambaye utaguswa na mafundisho haya
ya Nabii Hebron kwa jinsi alivyonifunulia neno hili takatifu ili ulimwengu
upone na usiangamie. Swali jingine la kujiuliza ni kwa nini mapokeo yameletwa
na kuchanganywa na neno la MUNGU? Kama mnavyojua YESU yeye ndie chakula cha
uzima na mtu atakapolila neno lake atakuwa na uzima, hivyo basi kila mtu
anayetaka uzima ni lazima roho yake ipate neno lake kama lilivyo, MUNGU
amelihakikisha ndilo linalofaa kwa wanadamu. Sasa shetani na yeye ili aliharibu
neno lile ambalo mtu akilila atapata uzima shetani akaleta maneno yake akampa
mwanadamu au baadhi ya wanadamu ambao ni waalimu, wachungaji, mitume, manabii,
na wengineo, wale ambao hawakusimama imara katika kweli au wale ambao shetani
amewazaa kiroho wafanye kazi ya mpinga kristo au wale ambao mwanzoni waliitwa
na MUNGU ila baadaye wakamwasi MUNGU wakaingia upande wa mpinga kristo. Sasa
unavyoyapokea na kuyaamini hayo mapokeo ya wanadamu na wewe tayari katika
ulimwengu wa roho umekuwa mwana wa wanadamu badala ya mwana wa MUNGU, kwa
sababu umepokea katika moyo wako ukafanyika uwe mnafiki kwa YESU na kwa MUNGU
pasipokujua au kupenda ukayaamini maneno hayo mkayafanya ndio njia yako ya
kiroho, na unapoyafuata basi na roho yako ndipo ilipo. Hivyo basi, nimendika
ujumbe huu kwa mataifa yote ili ueleweke, kwa sababu YESU anarudi na watu wengi
wapo katika mapokeo pasipo kujua na wanarithishwa na kuwafanya baadhi kuwa
wanafiki mbele za MUNGU wakati wao wanampenda YESU kikweli ila wametegwa na
mtego huu wa mapokeo ya injili ya uongo.
Nitaeleza baadhi ya mapokeo ya kibinadamu
na zaidi hata baadhi ya vyuo vikuu vya injili vimeacha neno la kweli na
wanafundisha kwa kuchanganya na uongo. Ninaposema uongo nataka uelewe ni jambo
lolote ambalo neno halijaagiza lifanywe au mafundisho yanapokuwa ni tofauti na
YESU alivyosema katika kitabu chake, yaani Biblia. Sasa cha ajabu katika Katiba
hii ya MUNGU alivyowapa wanadamu, wametokea waongo katika baadhi ya imani za
kikristo wakabadilisha vipengele kama neno lilivyosema ikawa ni tofauti.
MIFANO:
1. Ubatizo
wa kikombe, ubatizo wa kisima, kubatizwa kwenye tenki, kubatizwa kwa kutumia
bendera au kubatizwa kwa jina la mchungaji. Katika Katiba ya MUNGU hakuna
batizo za jinsi hii japo hata mimi niliwekewa ubatizo wa kikombe hapo awali ila
namshukuru YESU nimebatizwa tena na ubatizo mtakatifu wa maji mengi
yanayotembea na hata hao waliobatizwa hivyo siyo kwamba hawampendi YESU bali
hawajui ukweli wa neno lilivyo! Kitu cha kujiuliza, ubatizo wa Yohana umetokea
wapi? Jibu ni Mbinguni, jiulize sasa ubatizo wa kikombe, kisima na hizo
nyinginezo zimetokea wapi? Jibu kwa mwanadamu basi kama umepokea na kuamini
ubatizo wa wanadamu na wewe utakuwa mfuasi wa wanafiki ambao YESU amewasema kwa
sababu alipo YESU hamtaenda kabisa, kwa sababu mmepokea kiapo cha kibinadamu cha
ubatizo halafu kikachanganywa na Neno la MUNGU, yaani YESU akatajwa, Roho Mtakatifu
atajwa na mengineyo, hapo bado ni unafiki. Shetani anao uhalali kabisa na wewe kwa
sababu mmepindisha, umekubali kufuata ya wanadamu badala ya YESU. Kwa kila mtu
afuataye hayo hiyo ni dhambi inatembea na yeye.
2. Mifano
mingine imeandikwa, ukiombea watu usiwatoze pesa, lakini hili ni tatizo na kero
kubwa katika ulimwengu wote, hili pokeo la shetani linawatesa sana watu
wakifikiri ni Neno la MUNGU kumbe ni neno la pepo kabisa, ambalo linatumika
kuwaibia wakristo na wasio wakristo katika sehemu za ibada. Nataka uelewe mambo
haya kama alivyonieleza YESU haijalishi utachukia au utafurahi, nimetumwa
kueleza ukweli wa Neno lilivyo na kuliondoa giza ili wale wanaopenda kwenda
mbinguni waende, wasipelekwe jehanamu. Kila mtumishi anayewatoza watu pesa kwa
ajili ya maombi, yeye anakuwa ni mnafiki kwa YESU, na wala hawampendi YESU, na
wala hawamheshimu. Ibada hizo zote ni za kinafiki mbele za MUNGU, na zaidi
unaposali hapo wewe muumini unaambukizwa kidogo kidogo roho ya kinafiki na hiyo
roho ikiingia ndani yako unaanza kupinga kweli ya Neno na mwisho wake unakufa
kiroho na hata kimwili. Ukifa kiroho huendi mbinguni kwa sababu shetani anakuwa
anao uhalali kwa sababu haukumwabudu MUNGU ulipokuwa hai. Ila mtashangaa, hao
watumishi wanaotoza watu pesa wao wanaendelea kufanikiwa, hili lisikushangaze kwa
sababu hao hawaendi mbinguni wakifa bali wanaenda moja kwa moja kwa baba yao wa
uongo ambaye ni shetani.
Mapokeo ya wanadamu yapo mengi ila nitaelezea
machache ambayo ni sugu na utaelewa vizuri kwa mifano. Imeandikwa usiabudu
sanamu, lakini sanamu zinaabudiwa, ibada za kumbukumbu za wafu, wakati MUNGU
yeye siyo wa wafu. Kumwomba mtumishi akusamehe dhambi zako na ukaungama kwake
badala ya kuungama kwa YESU anayesamehe dhambi. Harambee makanisani, wakati
YESU alikataa, sasa kanisa limekuwa ni soko, hata hao waliokubali kufanya
harambee wakitumia jina la YESU, hao wanakuwa ni wanafiki, kwa sababu YESU
hataki unafiki, yeye alimpenda BABA yake na Neno lake. Soma Marko 11:15-18, sasa iweje nyie
wanadamu wa leo hufanya kinyume na aliyekuumba? Hivi mnafikiri MUNGU hawaoni?
Nawaeleza na hii siyo siri, MUNGU anawaona na mwisho mtapata fimbo yake. Hivyo
wacha usije ukachomwa moto, tubu na uokoke sasa hivi. Haijalishi unakesha miaka
yote ya ukristo lakini kama unayafuata mapokeo ya wanadamu, YESU anakuona ni
mnafiki tu ukimwabudu yeye bure. Je ni wangapi wanamwabudu bure na wangapi
wanaendelea kumwabudu YESU bure.
Ukristo wa mapokeo ni kama vile mtu
anayefanya kazi na asipate faida yoyote bali ni hasara tupu, au ni sawa na mtu
anayelima shamba heka kwa maheka lakini hapati mazao, anavuna hewa tu. Na
ukumbuke, hata mkulima huyo atatumia gharama nyingi katika shamba hilo na
zitapotelea chini, ndivyo ilivyo na kwa mkristo wenye kufuata mapokeo. Ili
upone, ukoka na wala usishiriki katika nyumba zao za ibada za mapokeo, ndio
sababu imeandikwa tokeni mkatengwe nao. Wewe unayekaza shingo tii neno hili, ni
sauti ya MUNGU kwako na siyo sauti ya mapokeo.
ZIJUE AINA
ZA WATUMISHI WA KANISA
1. Watumishi
wa kweli wakiitwa na MUNGU, hawarudi nyuma kwa kulichanganya NENO na uongo. Ni
lazima MUNGU amtume yeye binafsi.
2. Watumishi
wa kimapokeo: Hawa ni watumishi ambao wamejiita au wametumwa na shetani au
walimwacha MUNGU na bado wanahubiri kwa kupitia roho nyingine ya giza. Wengine
huteuliwa na watu na siyo MUNGU na kaisomea hiyo kazi ya uchungaji. Nataka
muelewe siyo mbaya kwenda bible college lakini je hiyo bible
college haina mapokeo ya wanadamu? Mfano jiulizeni enyi dunia mnaompenda Mwenyezi
MUNGU na mseme kweli je hizo shada (degree/PhD) anazozipata mtu halafu
anakubatiza kwa kikombe au kwenye kisima, je atabisha kwamba hizo siyo PhD za
kibinadamu? Jibu lipo wazi napenda muelewe, mimi sina mipaka katika injili ya
YESU, nasema anachonielekeza hata mimi nilikuwa sijui elimu hii ila ndiyo kweli
hata uombe, na umuulize MUNGU kuhusu elimu za uongo atakwambia siri zake, hizo
ni za mpinga kristo, ni za kimapokeo. Na zaidi ukiwa mnafiki kwa YESU, yaani
ukiona ukweli, hutasema ile kweli ili isimame imara bali utachukia kwa sababu
tayari ulishakuwa mwana wa wanadamu na siyo mwana wa MUNGU, ila asiye mnafiki
kwa YESU atatubu na kuachana na taratibu hizo na atamtukuza MUNGU kwa ajili ya
uponyaji alioupata.
3. Huduma
kuwa na ma-partners, wanachaguliwa na kiongozi wa huduma kwa sababu ni
watu wenye uwezo kifedha, eti hao ndio waliochaguliwa na MUNGU. Hayo ni mapokeo
yake huyo mtumishi. Na zaidi ndani yake anakuwa analo pepo tamaa na uwizi na
pepo la unyang’anyi, akiwa ni mwana wa shetani mwaminifu katika unyang’anyi.
4. Mapokeo
ya shetani ya kuwadai watu pesa makanisani, yaani kila muumini lazima alipe
kiasi fulani cha pesa na asipo lipa mtu huyo akifa hawamziki. Msilipe, huo ni
ushetani kabisa, YESU hajaleta mambo hayo, hayo ni mambo yao ya kitapeli. Huduma
au kanisa likianza mtindo huo tayari linakuwa ni la kitapeli kwa sababu huu ni
utapeli. Tafuta katika Biblia, hairuhusiwi kabisa, sasa hii imetokea wapi?
Mwenye akili na aelewe.
5. Kumwona
mtumishi yeyote haupaswi ulipe pesa kwa secretary
ndio upewe appointment, anatakiwa
awahudumie kwa upendo, hivyo ndivyo watumishi wa YESU walivyo. Kanisa siyo
hospitali, yaani kumwona daktari lazima
kwanza utoe pesa, hayo ni mambo ya kaisari, kaisari hamwangalii MUNGU na MUNGU
haangalii ya Kaisari, na ndiyo maana YESU alisema ya Kaisari mpe Kaisari na ya
MUNGU mpe MUNGU. Sasa kanisa limekuwa Kaisari? Jibu hapana na kama siyo basi
usitegemee kukutana na MUNGU mahali ambapo yamefanyika mambo ya kikaisari.
Angalizo:
Yapo mapokeo mengi ila MUNGU akufunulie
zaidi ili ushinde. Tubu, sema, BWANA YESU, naomba unisamehe dhambi zangu zote,
uniandike jina langu katika kitabu chako cha uzima. Ulitoe jina langu katika
kitabu cha mapokeo ya wanadamu, nahitaji kuwa mwana wa MUNGU na siyo mwana wa
mapokeo ya wanadamu, nikijua kuwa ule mwisho mimi nitaenda mbinguni na siyo
kwenye mapokeo ya wanadamu, nayafuta, najitenga nayo kwa jina la YESU. Amen.
NABII
HEBRON WILSON KISAMO
USISAHAU KUSUBSCRIBE YOUTUBE CHANNEL
YETU YA PROPHET HEBRON KWA KUBONYEZA LINK HII https://www.youtube.com/prophethebron?sub_confirmation=1 KUTAZAMA
VIDEO ZAIDI