Pages

Wednesday, November 8, 2017

JE NI KWA NINI UNAPOACHA UOVU BAADHI YA WATU WANAKUDHARAU?

Napenda kuwatia moyo watu wote mnaompenda YESU na mmeamua kuokoka, songa mbele katika utakatifu na kukaa katika sheria zake MUNGU. Hili si jambo geni, naishangaa dunia hii pamoja na watu wake na wewe pia msomaji wa Blog hii ya Nabii Hebron nadhani unashangaa. Tukianzia kwa kuhani wetu mkuu YESU, yeye alichukiwa na wale ambao walikuwa hawataki mazuri bali wanapenda uovu udumu katika maisha yao na akapendwa na watu waliopenda mema. Sasa hivi kanisa lina matabaka mengi ila nitaongelea matabaka matatu:
1.     Wapo wanaofurahi mtu anapoacha uovu akaokoka;
2.     Lipo kanisa ambalo linafurahia uovu halitaki watu waache dhambi na wampokee YESU linapenda watu waendelee na matendo maovu, hili siyo kanisa lenye kumpenda YESU ni kanisa lenye mfumo wa mpinga kristo.
3.     Lipo kanisa ambalo halitaki watumishi waseme kweli ya Neno la MUNGU kama lilivyo na ukisema ukweli wanakuchukia kwa sababu ndani yao ipo hiyo roho ya muovu na siyo Roho Mtakatifu katika mioyo yao, limtokalo mtu ndilo lililomjaa mtu katika moyo wake ikiwemo mafundisho ya uongo, ujue roho wa uongo ndie amejaa ndani yake.

Sasa cha kujiuliza ndugu msomaji na mtoto wa MUNGU, kwa nini unapoamua kuacha uovu, badala ya jamii ya kikristo kufurahia, wanaanza kukusema, watakudharau, na hata mara nyingine kukutemea mate kwa sababu umekataa uovu. Nataka uelewe kwamba ipo roho ya uovu ndani ya hao wanaokuchukia kwa sababu umekata mawasiliano na ushirika na hizo roho, hivyo wewe siyo mwenzao na hizo roho zinaona moto na Roho Mtakatifu ndani yako, wewe usisubiri kutiwa moyo na dunia, BWANA YESU atakukumbatia ile siku ya mwisho na kuvikwa taji lako kwa jina lako endapo utashinda uovu. Tambua siyo kwa kuokoka tu ndio kwenda mbinguni, uokoke na matendo yako yawe mema.

Wapo walioacha uzinzi, ulevi, umalaya; utaona marafiki wanawasema vibaya, sasa ninachotaka kuuliza, je mbele za watu wote ni bora kutenda mema au mabaya? Sasa mtu unapoamua kwenda kwa MUNGU mbona watu wengi wanawacheka? Je mbona mtu akiwa mchawi, mlevi, mzinzi na mengineyo anaonekana anafaa sana na baadhi ya watu. Hii inaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu ipo kwa shetani, kuanzia kanisa mpaka kwa watu. Baadhi yao wapo upande wa shetani na hawapendi utakatifu kabisa. Hata katika baadhi ya makanisa ukiokoka wanakutenga, wala usishangae ni lazima wakutenge kwa sababu wapo katika njia ya uovu ambayo wewe umeikataa katika imani, umeitaka njia takatifu, hivyo hiyo roho haiwezi kukutaka kwa sababu umekuwa ni moto katika roho na siyo giza.
Nawatia moyo muokoke msiogope kuchukiwa, mbele yako yapo maisha mazuri ya milele na ya kifalme na hao wanaong’ang’ania uovu na kusema eti uovu ni mtindo (fashion). Unapotenda uovu na kumkataa YESU, na yeye atakukataa, wakati ni sasa, okoka.

Sema, BWANA YESU, naomba unisamehe dhambi zangu zote, ulifute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na kuliandika katika kitabu chako cha uzima wa milele, mimi sitaki tena maisha ya uovu, nisaidie niweze kuishi maisha matakatifu yanayokupendeza wewe na ule mwisho nivikwe taji la milele, Amen.
Wanaokucheka ipo siku watalia na kusaga meno katika moto wa milele, wewe tengeneza maisha yako sasa.

NABII HEBRON.