JE
MUNGU ANAPOKEA SADAKA ZA KUDAIWA KWA KUFUATWA MPAKA NYUMBANI NA KUKUSANYWA NA
WAZEE WA KANISA?
BWANA YESU ASIFIWE, Watu wote wa mataifa
yote mnaompenda YESU na kulitetea Neno lake na Jina lake. Hapa ninaongelea sadaka ambazo hazitolewi kanisani na badala
yake uongozi wa kanisa unakuwa na orodha ya majina ya waumini wake wanaofuatiliwa
mtaa kwa mtaa au mji kwa mji. Ukisoma katika Mathayo 6:4, inaelezea jinsi ya kumtolea MUNGU sadaka, SADAKA iwe ni siri yako wewe na MUNGU
na wala asijue mtu mwingine kuwa umemtolea nini MUNGU ibada yako.
Jambo la kwanza, hao wanaotumwa katika
nyumba za waumini kuchukua sadaka kwa lazima kwa kutishiwa usipotoa hiyo fedha
siku unapopata tatizo kanisa halitahusika na wewe, nataka mfunguke akili na
ufahamu wenu, ndiyo maana hata Timotheo
akasema ni nani aliyewaloga nyie Waebrania
hata mdanganyike na mkasahau Neno linavyosema. Nikuulize swali, je sadaka
hutolewa kanisani au nyumbani kwako? Jibu ni kanisani na je ni wapi Katiba ya MUNGU inaruhusu kuandika
majina ya waumini na baadae akishalipa kuandika kiasi alichopangiwa na
binadamu? Nasema huyo siyo MUNGU bali ni binadamu. Swali linguine, jiulize wewe
unamtolea MUNGU sadaka au unamtolea binadamu? Kwa sababu mwanadamu anaweka kumbukumbu
(records) zako za mapato yako ili
siku ukifariki ndio ile pesa uliyolipa kwake huyo mungu binadamu na watu wake waje
wakuzike.
Nilipokuwa naongea na YESU nilisikia sauti
Yake akihuzunika sana juu ya wizi na unyang’anyi huu. Watu wanafikiri
wanamtolea YESU, kumbe ni mapepo ya kamari, haijalishi limetjwa Jina lake.
akaniambia hao ni wanyang’anyi na hao wote iwe ni wazee wa kanisa, mwinjilisti,
askofu, nabii na wengineo wote, sehemu yao ni katika ziwa la moto na huo ndio ukweli na mie sipunguzi
wala siongezi.
Ujumbe huu ni wa kwako wewe popote ulipo, YESU
akaniambia, “wanajipangia pesa zao na kuwapangia waumini jinsi ya kuwalipia
madeni yao”, akaniambia, “waeleze mimi sipo kabisa katika madhabahu hizo,
haijalishi wanalitaja Jina langu, nilishasema watakuja na watatumia Jina langu
na nyie ni mashahidi mnayaona ni wizi wa kitalaam kupitia shetani tena zaidi
wanawafuata watu majumbani kwao nyakati za saa 11 alfajiri, kabla hawajafungua
milango wao wapo nje na msalaba wa mti wakiutumia kana kwamba ni YESU wakati ni
mbao tu tena ya Cyprus, na watu huogopa na kutoa pesa wakielezwa ni YESU”.
Amenituma niwaeleze, YESU hajawatuma na wala
hatakaa awatume, tazama hata Mathayo
alikuwa mtoza ushuru, akamwambia “acha nifuate mimi ukanitumikie” sasa hamuoni
ni ajabu baadhi ya makanisa ya leo yamejengwa na pepo Mathayo, yanatumia jina la YESU kuwaibia watu pesa na mali zao
na wengine kwa njia ya kuchezesha kamari makanisani. YESU hachezi kamari
kabisa.
Sadaka inatakiwa itolewe kanisani kwa kuamua
katika moyo wako mwenyewe, tena kwa kumtolea MUNGU kwa furaha, kwa sababu ile
ni ibada kati yako wewe na MUNGU, ikiwa inafuatiliwa na watumishi au wazee wa
kanisa katika nyumba zenu wakidai tumekuja kuchukua pesa ya BWANA wewe usiwape,
tena uwaeleze kuwa unatoa kanisani, na ukristo wako wasiufanye kama mdaiwa sugu,
kwa MUNGU hakuna mambo hayo, waeleze tafadhali ondokeni kwangu katika jina la
YESU, waeleze sadaka yangu au pesa yangu siwapi kabisa. Kama nyie ni kaisari
labda mnidai ankara (bill) ya maji nitalipa
au ya umeme nitalipa au kodi ya nyumba uliyopanga hiyo lipa, kwa sababu
yakupasa kulipa deni, ila kwa MUNGU ni tofauti.
MUNGU unamtolea kanisani kwa amani yako.
YESU hakuwazii mabaya eti ukipata shida aone utapata msaada wapi, Yeye
anatuwazia mema kila siku na Damu yake YESU inanena mema juu yetu. Sasa cha
ajabu jiulize kama kanisa ni la YESU kwa nini wanakwambia “ngoja tuangalie akipata
shida nani atamsaidia”, unachotakiwa hapo kujua ni kwamba hilo siyo kanisa la
MUNGU ni kanisa jina tu, ni jengo la biashara na malengo yake ni ya kibinadamu
kupitia siri zao za unyang’anyi.
Jinsi baadhi ya makanisa katika ulimwengu
wote yalivyo acha njia ya MUNGU mpaka inakuwa ni aibu, kwa sababu makanisa mengi
pia yameanzishwa na shetani ila yanatumia jina la YESU, na jinsi ya kuyajua ni
kupitia matendo ya jinsi ya kuziendesha hizo huduma ikiwemo na hii ya kufanya
makusanyo kwa kumwinda muumini nyumbani kwake asubuhi na mapema kabla hata hajaamka
au siku za sikukuu (holidays), kwa
sababu wanajua mtu amepumzika na watamkuta ili awape pesa.
MUNGU hapendezwi kabisa na hao wakusanyaji
pesa, iwe ni mzee wa kanisa au yeyote yule, mbele za MUNGU au mbele za huyo
muumini wewe ni mwizi kama vile kibaka anayevunja nyumba ila tofauti yako wewe
unatumia kivuli cha jina la YESU kuiba na kunyang’anya kwa wepesi.
YESU ameniambia niwaeleze kuwa, pesa hizo mnaibiwa
tu. Wapo waumini wanao omba na kumwambia MUNGU kumbuka sadaka zangu nilizotoa kwa
kanisa lako asubuhi ulipowatuma watumishi wako nyumbani. Hao waliokuja asubuhi
kwako na ukawapa sadaka, wote ni wezi tu na ukiona kanisa linakwambia ukipata
tatizo hawatahusika kwa sababu umekataa kutoa mchango, uelewe kwamba hapo ni
kwa mapepo, hata ukichukulia kibinadamu, mchango ni hiari yako na siyo
kulazimishwa, tena hata huko duniani unatoa kwa uhuru wako lakini makanisani
unalazimishwa kutoa kwa ubabe yaani ni lazima. Jiulizeni, je bado mpo Misri kwa
Farao au mpo huru kwa YESU?
Mwenye akili na aelewe ujumbe huu. Msitoe
sadaka zenu kwa wazururaji na wasumbufu wanaodai watu pesa. Wameleta mbinu za Kaisari
za kukusanya mapato kwa kutumia jina la YESU. Kanisa siyo Kaisari, ya Kaisari
mpe Kaisari na ya MUNGU mpe MUNGU. Watu wote msije mkafikiri mtapata baraka
yeyote kwa MUNGU kwa kumtolea kwa njia hiyo, hizo zote mmetupa na mnaoendelea kutoa
kwa njia hiyo bado mtakuwa mmetupa kwa shetani na kuangamia. Wajulishe na
wengine.
MUNGU Awabariki!
NABII HEBRON.