JE MUNGU ANAHITAJI SADAKA AU MICHANGO?
MATHAYO 6:1-4
BWANA YESU wa Nazareti asifiwe, kutoka
katika kichwa cha somo hili, Je! MUNGU anahitaji sadaka au anahitaji michango
au MUNGU hupokea sadaka tu au MUNGU hupokea na michango pia? Jibu tutalipata
hapa hapa.
MUNGU anayo njia ya kumbariki mtu na
kila unachokitoa kwa hiari yako pasipo kuchangishwa hiyo hupokelewa na MUNGU na
anakubariki. Ukisoma Mathayo 6:1 “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa
watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa
BABA aliye mbinguni.” Hii ni michango inayofanywa makanisani au
unapofanya harambee usitegemee kuwa utapata baraka kwa MUNGU.
MUNGU anataka utoapo iwe ni siri yako
wewe na MUNGU sasa unapoagizwa kutoa michango ya kazi ya MUNGU, kumbuka yeye
hupenda kazi yake ifanywe na sadaka na siyo kwa michango. Michango ni kwa mambo
mengine ya kijamii inaamriwa kabisa, ila MUNGU yeye anajitegemea kwa kupitia
sadaka. MUNGU siyo masikini wala sio omba omba hana shida na akitaka kufanya
jambo lake anauwezo wa kuamuru kusi na kasi imtolee sadaka. Wapo watu wengi
ambao wanalia na kumkumbusha MUNGU sadaka zao kwa kusema, MUNGU kumbuka
nilikuchangia pale kanisani, nikumbuke na mimi? Ninachokueleza usimsumbue MUNGU
tena, acha kabisa, kwa maana ulipokea thawabu toka kwa wale watu uliowatolea
michango, yawezekana wakakusifu ukaona unafaa mbele za MUNGU, kumbe ulifaa
mbele za wanadamu wenzako tu uliowachangia na sio mbele za MUNGU.
MICHANGO KWA MAKANISA: (MICHANGO YA MAKANISA NI UGONJWA MKUBWA)
Michango makanisani ni ugonjwa ulioletwa
na shetani ukaingia na kuliteka kanisa, kanisa likafuata neno lisilo na pumzi
ya MUNGU wakafanya michango ndio sadaka, kumbuka sadaka ambayo MUNGU anahitaji
hataki ijulikane halafu wewe unawajulisha watu, unatangaza na unapigiwa makofi
na vigelegele na wanadamu, wanakutukuza wewe na kwa njia hii watumishi wengi
sana wameachwa na MUNGU kabisa japo wapo baadhi yao ambao walijiita na wengine
wameingia katika serikali ya shetani, ya ufalme wa shetani hao hawana hofu wala
aibu wa kuubomoa mfumo wa sadaka na hufanya mchango. Hata YESU alipoingia
hekaluni alikuta mambo hayo na alileta vurugu kwa kuwa haifai kufanyika katika
nyumba ya BABA yake. Je! Ninyi mataifa hamna hofu ya MUNGU? Tazama YESU yeye
ana hofu ila wewe unayejiita kwa jina lake hauna hofu! Na Je huoni kuwa ndani
yako anakaa roho wa shetani na anasimamia utawala wa shetani uimarike katika
dunia hii?
Bwana YESU amenituma mimi Hebron,
niwaeleze mataifa yote msitumikishwe na watumishi wa michango popote pale, Yeye
siyo masikini, upo ufalme wa mpinga kristo, wenyewe ni maskini na ili kuujenga
ni lazima michango ifanyike sasa usishangae kwa sababu mimi YESU nilisema
watakuja kwa kutumia jina langu na hata kuwapoteza wateule wa MUNGU, sasa
uelewe kuwa wapo wateule wa MUNGU na pia uelewe kuwa wapo wateule wa shetani
ambao wao huendeleza kazi ya baba yao kwa kulitumia jina langu, lakini
mtawajua kwa matendo yao ikiwemo michango, japo wapo baadhi yao ambao wao
waliiga na hata walipoiga walitekwa na shetani sababu MUNGU ni wa haki, tenda
haki upate haki.
Ipo michango ya majimbo, ya matawi, ya
kwaya, ya wachungaji, ya kanda, n.k. Nataka mjue kuwa kwa kuchangia huko
mlipoteza pesa zenu wala hamkuona baraka yeyote ile, MUNGU hupokea sadaka tu,
haijalishi ni ndogo au kubwa na ndipo utakapo barikiwa ila michango ni ujanja
wa kuwaibia waumini pesa, kwa sababu kisaikolojia utaona aibu kutoa mchango
mdogo mbele za watu wengi, kwa kuwa wanajua mwanadamu anapenda atukuzwe na watu
hivyo katika michango atatoa zaidi kwa wanadamu na katika sadaka yake atatoa
kidogo kwa MUNGU aliyemuumba, akidhani MUNGU hamshangai, anawapenda wanadamu
zaidi, mwanadamu anakuwa mchoyo kwa MUNGU.
Na
zaidi mahali kama panafanywa michango na wewe ukatoa sadaka zako ujuavyo ujue
kuwa bado umetupa kwa sababu katika madhabahu hiyo nuru na giza vimechanganywa
na MUNGU hakai mahali kama hapo, kwa sababu huo ni ujangili. Ukitaka kumtolea
MUNGU chochote ufanye kwa siri na kwa furaha, ni siri ndani yako na MUNGU
atakubariki. Ila kuhusu mchango sahau kabisa kabisa hapo MUNGU hayupo, hata
kwenye redio na TV, utasikia na kuona matangazo eti changia na siyo sadaka,
mwenye akili na afahamu hayo yote ni ujangili, asema BWANA MUNGU wa majeshi,
yeye anapokea sadaka na siyo michango au harambee.
Michango
makanisani ni kero kubwa sana kwa waumini, hata baadhi yao wameacha kwenda
kanisani kabisa kwa sababu ya kulazimishwa kutoa pesa kwa njia ya michango
kuanzia Januari hadi Desemba; ni wizi mtupu, waumini wanaibiwa pesa zao kwa
njia hiyo na wezi wa kiroho, usikubali tena kutoa michango, hata madeni
uliyoahidi na unayoendelea kudaiwa usilipe tena na mbinguni utaenda, uokoke
uishi maisha matakatifu.
NABII HEBRON.