JE! MUME AU MKE
ANAYEPATIKANA KWA NJIA YA UCHAWI NA NDOA HIYO KUFUNGWA KANISANI, JE NI MUNGU
NDIYE ANAWAUNGANISHA WAWE MWILI MMOJA?
Bwana YESU asifiwe! Watoto
wote wa MUNGU, napenda mjue kuwa Mwenyezi MUNGU ana mpango mzuri kwa ajili ya
kila mmoja ila umefika wakati wake wa kuwafundisha wanandoa wapate kuwa
mwili mmoja kwa kusudi lake. Lipo tatizo kwa baadhi ya watu, wanazidi kumkosea
MUNGU wengine kwa kujua na wengine bila kujua. Wengine wanaamua kwenda kutafuta
mke au mume wa kuoa kwenye malango ya kuzimu, yaani wachawi. Watu
hawa wakisha fanikisha kumloga mwenzake ili awe mke au mume wake, kisha wanakwenda
kanisani kufunga ndoa, wakifikiri kuwa MUNGU atawaunganisha wawe mwili mmoja
kama mke na mume na atatambua kuwa ni ndoa takatifu na kumbe hiyo ni ndoa ya
giza (nyeusi).
Napenda
muelewe kuwa watu wengi wanateseka na wengine wanafikiria kwenda kwa
waganga ili wapate wenzi wao, nawaeleza hata kama mtu atafanikiwa kumloga
mwenzake, bado MUNGU hata itambua ndoa hiyo, haijalishi anayefungisha ndoa hiyo
ni mtumishi wa aina gani, ila mwenye macho ya rohoni ataomba na ataona hapo
hapo tatizo na uchumba utasambaratika, ila ikiwa mtumishi hana macho ya
rohoni atakua amedanganywa na atafungisha ndoa kwa akili yake na ibada
ikafanyika, ila kwa MUNGU ibada hiyo ni uchafu mbele zake, kwa sababu siri
imefichwa machoni mwa wanadamu ila MUNGU yeye hafichiki, ndoa hiyo itakuwa
imeunganishwa na shetani kwa sababu asili yake ilianzia kwa wachawi, wakatuma
majini ya kike na ya kiume ndani yao wakakubaliana kupitia nguvu za
majini na majini hayo ndiyo yaliyofanikisha. Sasa kwa nini umshirikishe Mwenyezi
MUNGU ushetani? Hapo utakua umeelewa, kama uliyatenda hayo, unayo
dhambi ikiwemo ya kudhulumu haki ya mwenzako ya ndoa ya mpango
aliyopangiwa na MUNGU, na kati ya wanandoa mmoja wenu ambaye amemdhulumu mwenzake
haki hiyo na kisha unampatanisha na haki ya shetani uliyoipanga kichawi, tambua
kwamba umebeba dhambi hiyo.
Hata ukisoma Biblia, Waebrania
13:14, imeandikwa ndoa na iheshimiwe na watu wote, hapa tayari agizo la
MUNGU litakuwa limedharauliwa. Nafundisha ili wengi wapate kujua kuacha kupenda
kutafuta wake/waume kwa wachawi, waje kwa YESU kwa sababu hata ukimpata mke au
mume kwa njia ya kichawi na ukafunga ndoa kanisani au kuibariki bado
haiwezekani MUNGU kuitambui milele kwa sababu hapana ushiriikiano kati ya giza
na nuru. Kwa hiyo ndoa inakuwa ya shetani na majini siku zote labda mpaka neema
ya MUNGU imkute aliyedhulumiwa na kumtoa hapo.
Hata wale wenye miaka 50
katika ndoa, endapo walitumia uchawi, hata iwe ni mwezi mmoja au mwaka mmoja
bado nataka uelewe kuwa MUNGU haitambui ndoa hiyo kabisa, hata kama mtaishi
milele mpaka kufa, bado hautakuwa na ndoa inayotambulika mbele za MUNGU, bali utakuwa
na ndoa inayotambulika mbele ya shetani. Hivyo basi watoto wa MUNGU kwa kuyajua
hayo yote msipende kutafuta mke au mume kwa njia hizo, hata kama utatumia
mamilioni ya gharama za harusi kubwa bado itakuwa sio harusi inayotambulika
mbele ya MUNGU na pia bado mtakuwa ni wazinzi milele kwa
sababu chanzo cha ndoa hiyo sio MUNGU. Katika ndoa hiyo ni vigumu kuelewa ni nani aliye
enda kwa mganga ndipo akampata mwenzake, kwa sababu endapo ni kijana
hatasema na endapo ni binti hataweza kumweleza mwenzake kwa kuogopa kuachwa au
kutokuaminiwa na kama ikitokea kutoa siri hii ni mara chache sana, ila kumbuka
MUNGU anaona kila kitu.
Penda kumtegemea Mwenyezi
MUNGU katika kila jambo, na yeye atakufundisha, yeye ni MUNGU wa mafanikio yako
na usitegemee tena malango ya kuzimu na waganga wakienyeji, wachawi, wasoma
dua, wasoma nyota, ramli na zaidi kila mtu amshike YESU na kuishi maisha matakatifu,
hao waganga na wachawi hawatakuweza kwa Jina la YESU.
Tubu, sema, BWANA YESU,
naomba unisamehe dhambi zangu zote, sitashiriki kutafuta mume au mke kwa njia
ya kichawi na sitaki dhambi tena, naomba uandike jina langu katika Kitabu chako
cha uzima wa milele. Alichokiunganisha MUNGU ni cha MUNGU na
alichokiunganisha shetani ni cha shetani.
Angalizo:
Usije ukamlazimisha MUNGU kupokea kazi za shetani ili azikubali kwa sababu
MUNGU na shetani hawana uhusiano. Shetani na wafuasi wake ni maadui wa MUNGU na
hawana ushirika wowote. Natumaini watu wengi wamepona na wataacha kwenda kwa
wachawi, ukifanya hivyo ujue kuwa utakuwa wa shetani, hii ni sawa na kutafuta
mtoto kwa mganga wa kienyeji halafu ukizidiwa unamleta kwa MUNGU ili
ampokee (kuwekwa wakfu). Mtoto huyo hatapokelewa na MUNGU, kwa sababu atakuwa
amepatikana kupitia malango ya kuzimu, na mwisho mtoto huyo atakuwa na maisha
ya ajabu ajabu na hatafanikiwa mapema, hataishi maisha marefu na baada ya muda
mfupi shetani atachukua mtoto wake. Wengi nikiwaombea naona baadhi yao
wamepatikana kwa njia hizo na MUNGU hawapokei kama watoto wake, mbingu inakua
imenyamaza kimya.
NABII HEBRON.