Pages

Tuesday, March 31, 2015

JE UNAJUA KUWA KIBIBLIA AU KWA MUNGU MWANANDOA YEYOTE ANAPOKUWA AMEZAA NA MTU MWINGINE AKIWA KATIKA NDOA TAYARI AMEIVUNJA NDOA YAKE?
TALAKA YA KIKRISTO IPO HIVI…

BWANA YESU ASIFIWE, Nawasalimu watu wote wa mataifa yote na wanandoa na wasio wana ndoa. Ujumbe huu utawasaidia kuzitunza ndoa zenu zisivunjike na hata ambao bado hawajafikia katika ndoa mkifikia wakati huo mjitunze ili kusudi aliloliunganisha MUNGU kwa wanandoa kisivunjwe na shetani. Watu wengi wanafikiri ndoa hazivunjiki zilizounganishwa na MUNGU. Nataka uelewe shetani yupo kwa ajili ya kuvunja au kuharibu kusudi la MUNGU katika ndoa, na jinsi anavyotumia huwa analeta roho ya kutokuwa waaminifu kwa wanandoa pale wanapoanza kuruhusu miili yao iingiliwe na watu tofauti na mwili uliokuwa mmoja yaani mume na mke.

Ukisoma katika kitabu cha Mathayo 5: 31-32
31 Imenenwa pia, mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; 32 lakini mimi nawaambia, kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa  kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.”
Utaona maneno ya YESU anayoongelea kuhusu talaka, na neno linasisitizwa siyo kwa kosa lingine unaruhusu kumwacha mke wako au mume wako, ni endapo atazini na wewe ukipata uhakika kama ukivumilia . Katika  kipengele hiki mimi Hebron nimekuwa nikipigiwa simu na maswali mengi kuhusu ndoa na wengi wamepata majibu yao na wamepona, na sasa wanafurahia maisha yao na wanaziona baraka za MUNGU na hata ambao walikuwa na mpango wa kuzini nje ya ndoa wamepona kwa sababu wameujua ukweli.

Lengo la ujumbe huu, nia yangu; msome ili shetani asiweze kuja kuzivunja ndoa zenu kwa sababu ndoa inapokuwa na uzima shetani hapendi na siku zote shetani hapendi mapenzi ya MUNGU yatimie katika ndoa na yeye alibuni mbinu zake za kuvunja vifungu vya mistari katika biblia; mfano Mathayo 5:32;
32 lakini mimi nawaambia, kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa  kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.” Hapa utaona wazi wazi YESU mwenyewe anasema ni kwa habari ya uasherati tu ndio ndoa inavunjika na siyo makosa mengine. Sasa hapa inahusisha jinsia zote mbili awe ni mwanaume amezaa akiwa ndani ya ndoa tayari yeye kaivunja ndoa yake na yeye ni mzinzi, ndivyo biblia inavyosema kupitia maneno aliyoyasema YESU.  Na ikiwa ni mwanamke na yeye yupo katika ndoa halafu akazaa na mwanaume tofauti na mume wake, hapo tayari ameshaivunja ndoa yake, na endapo katika hizo jinsia mbili yeye ambaye hajasababisha au ni mwaminifu yeye hata akioa au kuolewa tena endapo atapata amani mbele za MUNGU yeye siyo mzinzi na milango yake ya kuolewa au kuoa MUNGU atamfungulia kwa sababu analiangalia neno lake; amtetee yule ambaye ni mwaminifu katika ndoa.

Point ya pili Mathayo 19: 3-11
3 Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? 4 Akakjibu, akawaambia, hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, 5 akasema, kwa sababu hiyo,  mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? 6 hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha MUNGU, mwanadamu asiwatenganishe. 7 wakamwambia, jinsi gani basi, Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha? 8 akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi. 9 Nami nawaambia ninyi, kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. 10 Wanafunzi wake wakamwambia, mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, haifai kuoa. 11 lakini yeye akawaambia, si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.

Hapa utaona Mafarisayo walimuuliza YESU kwa kumtega na yeye aliyajua hayo, akawaeleza je hamkusoma tokea mwanzo MUNGU aliwaumba mume na mke, na sababu hiyo wataambatana pamoja na watakuwa ni mwili mmoja? Mafarisayo wakamuuliza tena swali lingine, basi ni jinsi gani Musa aliruhusu kumpa hati ya talaka na kumwacha? YESU akawajibu, Musa aliyaruhusu hayo ni sababu ya ugumu wa mioyo yenu, ila haikuwa hivyo tangu mwanzo. Hapa utaona YESU anafunua siri hata  ambayo Musa alikuwa na yeye hajafunuliwa, ila YESU hapa ameifunua hiyo siri kuwa tokea mwanzo haikuwa hivi. Verse 8 ; utaona YESU anasema wanakuwa ni wawili tena hapa ni baada ya kufunga ndoa, hivyo aliowaunganisha MUNGU wawe mwili mmoja mwanadamu asiwatenganishe.

Hapa MUNGU anaonya mtu asiwatenganishe; alitoa onyo hili sababu MUNGU anaona mbali kuwa ni mtu ndiye atakaye tumika na shetani tu ili kuitenganisha hiyo ndoa na ikawa tena siyo mwili mmoja, sababu mwili wa wanandoa unaunganishwa na miili miwili, ya kiume na ya kike. Verse 9 YESU akasema 9 Nami nawaambia ninyi, kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini.”  BWANA YESU ASIFIWE, katika mstari huu wa 9 nataka muelewe sababu kuna watu wametekwa au kufanyiwa matendo mabaya katika ndoa kwa jinsi nitakavyoelezea utapata picha na ikifika mtu mmoja wapo iwe ni mwanandoa wa kike au kiume yeye baada ya either mwenzake akiwa katika ndoa yeye akazaa na mwanamke nje ya ndoa au mwanamke akatoka nje ya ndoa akaenda akazaa na mwanaume mwingine na hadi matunda ya uzinzi wakayaona. Yeye hata akiamua kuoa au kuolewa, yeye aliyekuwa mkamilifu yeye anaruhusiwa kabisa na yeye hataitwa mzinzi.

Soma biblia inasema wazi na adhabu ya mwanandoa anapoingia katika ndoa halafu akafanya uasherati tu yeye hana cha kumtetea mbele za MUNGU, na neno halibadiliki kwa sababu ndivyo ilivyo elezwa na adhabu yake iwe ni mwanaume au mwanamke. Katika siku zako zote za maisha yako iwe utaoa au kuolewa utakuwa siku zote wewe unazini tu na hata aliyekuoa au kukuoa, hivyo katika paji lako la uso unabakia na alama hiyo ya jina la mzinzi, kwa sababu mshahara wa dhambi hiyo ndiyo hiyo. Wewe soma utaelewa, verse 11 YESU akawaambia “11 lakini yeye akawaambia, si wote wawezao kulipokea neno hili, ila wale waliojaliwa.”

Hapa YESU alijua kuwa unapojua mmoja wapo katika ndoa siyo mwaminifu hata imefikia hatua iwe ni mume au mke yupo katika ndoa halafu akaenda kuzaa na mtu mwingine, tendo hili ni libaya na la aibu sana na ni la kumkasirisha MUNGU sana kwa sababu mwanandoa ambaye yeye amejaribu  kutokuwa mwaminifu na akawa adui wa MUNGU akazini akiwa katika ndoa, akazaa nje ya ndoa tayari yeye ni adui wa YESU, na pia ni adui wa jamii ambayo yeye alioa au aliolewa na ni adui kati yake na mwana ndoa mwenzake; yaani amemdharau. Ila MUNGU na yeye anayo neema yake kwa wanandoa waminifu wanaotendewa mabaya endapo atataka kuoa au kuolewa yeye anaruhusiwa; talaka atoe na anaruhusiwa kuoa hata atakaye muoa au kuolewa yeye ataitwa mwanandoa safi mfano; mume bora kutoka kwa BWANA au mke bora kutoka kwa BWANA.

Ila walioharibu ndoa zao kwa ajili ya uasherati iwe ni mwanaume au mwanamke; hao siku zote za maisha yao iwe waolewe au waoe, kila wanapokutana tendo lao la ndoa siyo takatifu bali itakuwa ni uzinzi tu, kuvunja amri ya sita. Neema hiyo haipo tena kwao ndivyo neno lisemavyo, hivyo chunga sana ndoa yako, usije ukafanya mchezo wa uasherati halafu ukasema utaoa au utaolewa tena. Sawa utaoa au kuolewa lakini siku zote tendo lako la ndoa itakuwa ni uzinifu na uasherati.

Jambo lingine kwa kuongezea, unaweza ukakuta wanandoa kati yao mmoja wapo yeye alimpata mwenzake kwa kutumia nguvu za giza na hata wakafanikiwa kufunga ndoa kanisani, ndoa hiyo inakuwa haijaunganishwa na MUNGU kwa sababu mwanzilishi ni nguvu za giza na kwa sababu kanisa limepigwa upofu na shetani unakuta watumishi wanafungisha ndoa kupitisha kazi za shetani. Ndoa za jinsi hii hazidumu kabisa  na bado hazijaunganishwa na MUNGU na hazitakaa ziunganishwe na MUNGU, siku zote giza na nuru vinatengana, hivyo ndivyo na alivyo katika ndoa. Wapo wengi ambao wanajua historia ya ndoa zenu kama wewe ulifanya siri ukamteka mwenzako sababu ulitamani vitu vyake au mafanikio yake, ukamloga, akakukubalia; uelewe hauna ndoa mpaka sasa na unayo dhambi kubwa mbele za MUNGU kwa sababu umetumika kuzuia mpango alioupanga MUNGU, mfano; J aolewe na X na wewe ukafanya J aolewe na Y. Ikiwa ni hivyo maisha yenu ni shida na zaidi hautafanikiwa lolote sababu siyo MUNGU kaunganisha ila limetumika jina la MUNGU kwa kumsingizia katika haya makanisa ambayo tayari yamemsaliti YESU baadhi yao.

NOTE:

Watoto wa MUNGU mpaka hapo kwa somo la leo itawafungua wengi na mtakuwa huru na nira zitawaachieni. Yeye MUNGU ndiye ajuaye mioyo ya wanandoa na amenifunulia haya kama Nabii wake Hebron niwaeleze; utakaye yashika hakika ndoa yako itapona na haitavunjika kwa jina la YESU. Wanandoa wengi walizoea kutenda uasherati na kujitetea eti alichokiunganisha MUNGU kisitenganishwe. Sasa umeelewa kumbe biblia inasema ukifanya uasherati na upo katika ndoa siku zote hata ukiachwa au ukaenda kuoa wewe utakuwa unafanya uzinzi tu hata na huyo aliyekuoa au kuolewa tena jambo ni mmoja na umemwambukiza mwingine hiyo dhambi.

Wanaume wengi wapo katika ndoa na wana watoto wanazaa na wanawake ambao hawajawaoa na bado wapo katika ndoa; hao tayari wamezivunja ndoa zao wanaitwa waasherati na biblia ndivyo isemavyo. Na pia wapo wanawake wengi katika nchi mbali mbali wapo katika ndoa na wanzaa na wanaume wengine na wapo katika ndoa na hata kuzaa watoto wa nje na kuwasingizia kuwa ni watoto wa ndoa, hiyo ni dhambi kubwa sana. Familia nyingi zina shida hii; ingekuwa kama wanandoa wangekuwa wanacheki DNA utakuta watoto wengi watu wanasingiziwa na siyo damu zao, hii ni dhambi. Unapokuwa umezaa nje ya ndoa, huyo mtoto anakuwa siyo wa ahadi kutoka kwa BWANA, ni mtoto wa matunda ya uzinzi.

Nawaeleza YESU anazipenda ndoa zenu, mzitunze kwa usafi na utakatifu. Wapo wengine wamezaa na wachungaji, maaskofu, mitume, manabii; hata hao ukizaa nao usifikiri utabarikiwa, unakuwa umejilaani iwe ni mwanamke au mwanaume na kufanyika wote ni waasherati na kujifungia baraka za maisha yako.

Zaidi fuatilia masomo katika vitabu vya Mtume na Nabii Hebron, ingia katika website, ingia katika blog na YouTube, utajifunza mengi na utapona. Karibu pia katika kanisa la YESU NI BWANA NA MWOKOZI WA MATAIFA YOTE. Ndoa yako yenye shida na vifungo mbali mbali vitaombewa na utapona.

Sema BWANA YESU naomba unisamehe dhambi zangu katika maisha yangu na katika ndoa uiponye. Uniandike jina langu katika kitabu chako cha uzima wa milele. Niongoze nisirudi nyuma tena, naacha tabia chafu katika ndoa, nitakuwa mwaminifu, YESU nisaidie. Amen.


NABII HEBRON.