Pages

Monday, December 1, 2014

MAELEZO YA YOUTUBE: Nabii Hebron amtaja Baba yake wa kiroho aliyemzaa na kumbariki ni Moses Kulola.

MUNGU WA IBRAHIM, MUNGU WA ISAKA, MUNGU WA YAKOBO anawapenda wote, anahitaji watu wamrudie. Kisa kikubwa cha yeye kuniita katika utumishi ni kwa ajili kanisa limemuacha, imebakia ni pesa tu. Na nilipita katika mambo mengi mpaka nimefika hapa kama nilipo, mpaka nikaweza kufanya kazi ya MUNGU, lakini haya yote alikuja kunieleza MUNGU alikuwa kwamba ananipitisha, alinificha kama Musa alivyomficha kwa Farao na mimi nilikaa kwa Farao, yaani watumishi ambao hawakuwa baba zangu wa kiroho, lakini pasipo wao kujua. Walinipiga sana, waliniumiza, walinikatisha tamaa lakini MUNGU alikuwa pamoja na mimi.

Na uzuri kila walilokuwa wanakifanya MUNGU alikuwa ananijulisha na niliendelea kumtii. Lakini ilipofika 2009 mwezi wa nne, aliniambia niondoke katika kanisa nilipokuwa nasali kwa mara ya mwisho japo nilisali katika makanisa mengi, lakini kokote nilikokuwa ninasali nilikuwa ninashangaa kwa nini watumishi walikuwa wananichukia na waumini wananipenda, na sababu kubwa ya kuchukiwa ni sababu nilikuwa nawaombea, wanafunguliwa pale ambapo watumishi wanashindwa mimi nikiwa bado ni kondoo. Mimi nilifikiri wangenipenda na kuniombea, lakini walinipiga na kunipiga wakaniita kila majina, lakini sikupungukiwa na chochote MUNGU alikuwa pamoja nami.

Mwaka huo wa 2009 katika kanisa niliokuwa nasali jumapili moja wapo YESU alishuka katika kanisa ile akasema na mimi peke yangu, pembeni yangu alikuwa muumini wa kanisa hilo ambaye anaitwa Charles, BWANA akaniambia nisikuone tena katika kanisa hili ondoka, mimi sipo. Nilijiuliza, lakini nikatii, nilivyokuwa njiani nikamwambia Charles, YESU ameniambia nisirudi katika kanisa hili tena, nikajiuliza lakini hayo mengine sikumfunulia, nikaondoka. Baada ya wiki kama tatu akaja Malaika Gabriel, akaniambia, pale umeambiwa usirudi tena, hata sisi Malaika tumewekewa X tusikanyage ni kanisa lote kwa jina hilo ambalo silitaji, akaniambia MUNGU ameshaondoka, sasa ondoka, tutakuongoza, tupo na wewe serikali yote ya mbinguni.
Sikuenda kanisa nilizuiliwa nikakaa, nilizuiliwa kama miaka miwili, siendi popote, nafanya kazi yangu ya utalii ninaenda ninarudi, ninaenda ninarudi, sina makao wala sina baba wa kiroho wa kimwili.  Na akaniambia hakuna baba yako wa kiroho
Nikajiuliza sana sasa huko nilipokuwa ninasali ni nini? Lakini alinificha kwa kuwa hata angenieleza nisingemuelewa. Unajua hata mtoto jinsi anavyokuwa unazidi kumfundisha taratibu taratibu. Basi nikamtii yale alikuwa ameniambia ambayo siwezi kuyaeleza hapa, BWANA YESU ASIFIWE. Nikaendelea, nikaja nikaanzisha huduma kama alivyoniambia ambayo akanipa jina liitwe YESU NI BWANA NA MWOKOZI WA MATAIFA YOTE.

Akaniambia wewe kabla ya kuumbwa misingi wala kuingia kwenye tumbo la mama yako, tulikupa utumishi toka mbinguni, sasa tumekupitisha katika tumbo la mama yako tu ili kwamba uzaliwe kazi iende. Kama vile mimi nilivyokuja nikazaliwa hapa, wewe siyo mtumishi wa hapa duniani, hata mafundisho utakayofundisha ni ya juu, kwa sababu alikuwa anajua muda wake ukifika atanitumia, na ndio muda ndio huu sasa.

Nikaendelea, nikaendelea na kazi ya MUNGU kama ilivyo sasa hivi ili kumuona MUNGU zaidi na zaidi, ikafika 9.11.2011 akaniambia sasa Hebron nakuonyesha baba yako wa kiroho nikashtuka, nikaogopa, ni yupi tena wakati ameshaniambia hayupo. Akanimabia baba yako wa kiroho amekuwa akiomba kwa muda wa miaka mitatu, na mimi nimemuahidi kwamba ninakutengeneza na wakati wake ukifika nitakupeleka, nenda kamuone nami nikachukua hatua, nilivyokwenda alikuwa anajua sura ila jina alikuwa halijui, na MUNGU alimuambia mwisho wako wa kulia akamuambia mbariki, akanibariki. Baba yangu wa kiroho aliniambia ni Moses Kulola ndio alikuzaa, na YESU akasema naye tukiwa pamoja naye na mtoto wake anaitwa Willy.

Akamuambia, wewe mwenyewe umebaki wako wapi wenzako walikuwa na wewe? Wameniacha umebakia mwenyewe, hata uliowazaa baadhi yao wamekuwa wachawi, tazama hata na mguu wako huu, wakati huo alikuwa anaumwa na mguu, ni mmoja wa watoto wake ambaye amemzaa kiroho ndio alikuwa amemwekea kile kilema atembee na fimbo, ili amtoe kafara lakini ikashindikana, wanadamu wanabadilika.

Akamuambia hautalia tena, basi ilikuwa furaha na mimi wakati huo wa kumjua baba yangu wa kiroho. Alinifurahia sana, aliniombea, japo sasa hivi ni marehemu, lakini pia nilimuona mbinguni, tayari amepumzika kabisa wala msilie, kwa hiyo nina amani maanake nililia, sijawahi kupendwa na baba wa kiroho, walikuwa wananipenda kwa sababu ya pesa yangu.

Wengine sasa hivi baada ya mimi kuinuliwa wanasema mimi ni mtoto wao wa kiroho NO!  siyo, nilipitishwa huko kama mzururaji, baba yangu yuko mbinguni, ametulia, na sasa hivi ni YESU peke yake ndio ananilea, wala sihitaji mwanadamu yeyote kunilea kiroho, nalelewa na BABA yangu tu. Nilipigwa na watumishi niliangamizwa, na nyie watumishi mnaona mnashindwa kukua au kondoo makanisani mnaagamizwa na watumishi ujue huyo ni baba yako wa kiroho wa kambo. Ni bora baba wa kambo wa kimwili au mama wa kambo wa kimwili anahuruma kuliko baba wa kiroho, anakuua kabisa, anakumaliza kila kitu kwa sababu ya wivu, BWANA YESU ASIFIWE.

Basi ndio ikawa ni furaha yangu toka wakati huo mpaka sasa kwa hiyo nikawa namshukuru MUNGU sana. Na mimi ninawaeleza, muendelee kumwangalia MUNGU, mambo yameharibika, na cha ajabu 14.6.2010 nilipelekwa mbinguni, cha ajabu nilivyopelekwa mbinguni, nilionyeshwa katika watumishi wa Tanzania nilionyeshwa Kulola peke yake, Moses Kulola ndio yuko mbinguni, lakini sikuelewa kwa nini maana yake, akaniambia Hebron huyu ndio amenifurahisha moyo wangu, na huyu ndio alianzisha injili Tanzania, lakini sasa hivi injili imekufa amebaki mwenyewe. Akanionyesha majina mengine yote sikuyaona ya watumishi wakubwa hapa Tanzania, kabisa kabisa hakuna hata mmoja hata na madhehebu hakuna hakuna, na hii ninawaambia ukweli na kama yeye hayupo ina maana hamna kitu chochote 98% shetani ameshikilia.

Akamuambia katika Afrika BWANA YESU tukiwa na Moses Kulola wakati huo bado yuko hai, katika Afrika amebakia yeye peke yake, sasa hebu jiulize ndugu msomaji, kuna watumishi wangapi? Halafu anaambiwa amebaki Moses Kulola, halafu ameondoka, ni nini kipo? Manabii ni waongo, wauza madawa ya kulevya, waizi, wana mazingaumbwe, kweli imeondoka ni uovu mtupu. Ninachowasihi, mnaotaka kupona muokoke kikamilifu tena muishi maisha matakatifu yakumpendeza MUNGU na kama ni kazi ya MUNGU fanya ya kumpendeza MUNGU na siyo kunyang’anya nyang’anya watu hela na siyo kubatiza watu kwa maji ya kikombe huendi, kubariki watu wazima huendi. Hata kuchukua pesa za watu makanisani, mnamfanya MUNGU anakuwa nyang’anya nyang’anya, lakini wakati umefika sasa ulimwengu lazima ubadilike na hii anaifanya MUNGU mwenyewe wala hakuna atakayemsaidia, wala haitaji nchi yeyote wala nini, huo ndio ukweli, kama unaweza shindana na Eliya au unaweza shindana na Musa, shindana naye, hao ndio wamepewa kazi sasa ya kuangalia BWANA YESU ASIFIWE.

Jambo lingine pia katika kanisa nilikuwa nimepita, MUNGU ambalo alinifukuza huko, akaniambia huyu sasa hivi yeye waumini ndio wanamuita MUNGU, halafu sasa hivi anabatiza watu kwa jina lake. Mfano mimi nakubatiza kwa jina la BABA, na la MWANA, na la ROHO MTAKATIFU halafu nakuwekea kwa jina la Hebron, hivi, tafuta kwenye biblia ipo hiyo? Haipo. BWANA YESU ASIFIWE, kwa hiyo mambo yameharibika, ni kuchunguza na kuwa waaminifu, kuangalia, kuwa makini sana. Mashetani pia wanaamini YESU ni mwana wa MUNGU, sawa, ndio, hata watu wanaamini kuna mwana wa MUNGU lakini hawana neno, watu wanahangaika na Zaburi 23 zimekaa kichwani lakini mapepo yamejaa, mjiulize shida iko wapi?

Zaidi soma katika mafundisho ya vitabu vya Nabii Hebron ambavyo MUNGU alinipa mimi, na mimi ninakueleza tena hayo ni madogo tu, kwa sababu nikitoa makubwa zaidi, ufahamu wako unaweza pasuka. Sasa hivi watumishi wanapaa kuliko mwewe au njiwa angani, usiku wanapaa, wa kweli ni wachache sana. Nchi zimelaanika, haya makanisa yachunguzwe ni wauzaji wa madawa ya kulevya, yaani kanisa linaingiza madawa ya kulevya halafu wanadamu wanavuta, inamaana YESU ameingiza madawa ya kulevya.

Enyi wa Galatia imeandikwa, nani aliyewaloga? Enyi nchi zote za dunia nzima, viongozi na serikali nani aliyewaloga? Nawafungua fahamu zenu na MUNGU awainue maana anawapenda sana. Mfanye kazi yake vizuri, mlinde raia wenu, watumishi sasa hivi ndio wanakuwa wanaharibu nchi zenu na siyo nchi zenu ni za MUNGU. Ulikuja uchi utarudi uchi, ni wakati wa kutengeneza nchi, haujui leo upo, kesho haupo, sasa hivi watumishi ni kujinadi kwenye TV namba za benki, Mpesa, MWIZI! Kama MUNGU angemtuma yeye, angemuandalia njia, ameniambia yeye siyo omba omba, na kwa nini wanaomba, ni kwa sababu hawajaitwa.

Mimi YESU aliponiita ameniambia Hebron nimekuita, ndio neno, kwa hiyo kila kitu kitanyooka. Maharambee harambee harambee uwizi mtupu, mnaibiwa, mnazidi kumchukiza MUNGU kwa hiyo mbadilike, mumrejee MUNGU na muokoke, bila wokovu hakuna kwenda mbinguni. Kazi ya MUNGU wana wa MUNGU imekuwa ni biashara sasa hivi, hakuna ukweli, hili jina kwa sababu ni la thamani kila mtu analikimbilia.

Usitishwe na mtu ananena. Sasa hivi watumishi wanatoa watu huku machuma, huku machungwa wanatoa huku mawe, hayo ni mazingaumbwe uwongo. Kila mtu afunguke, BWANA YESU ASIFIWE, itafika mahali watu wanatoa watu maembe kichwani, hivi mnaona mazingaumbwe haya? 98% kanisa limekwenda, na kanisa lililokwenda haliko na YESU maana likiwa na YESU haliendi halitekwi. Na watumishi wanachukiana sana. Ukisema ukweli tu unachukiwa, mimi sijali, hata BABA yangu YESU alichukiwa lakini si alishinda. Mimi hata kukohoa sitakaa nikohoe, hata hakuna atakayekaa mbele yangu, wameshasimama wengi, hata kunisemea kwa kiongozi wa nchi mimi najua lakini imeruhusiwa mkachorwe huko uwovu wenu, BWANA YESU ASIFIWE, na mengine mengi muendelee kusoma vitabu, msiogope, ninawaombea wote kwa jinsia yote, sina ubaguzi, naombea nchi zenu zifunguliwe, na nchi ya Tanzania imeshanyanyuliwa ni Edeni.

Habari ya kuloga loga viongozi hakuna tena kuzoea kuloga viongozi na kuwalaumu. Ukishakuta serikali inalaumu viongozi hawaendi vizuri kanisa linashida, wako wapi wawaombee? Sasa wenyewe wanamazingaumbwe, MUNGU anasikiliza wana mazingaumbwe?

BWANA YESU ASIFIWE. MUNGU awainue, MUNGU awaokoe. Endelea kufuatilia vipindi vya Mtume na Nabii Hebron, ninaachilia moto ubomoe kila nguvu zinazokusumbua ndani yako kwa jina la YESU, kwa damu ya YESU. Amen!


NABII HEBRON.