ADAMU WA
PILI NI YESU WA NAZARETI WALA SIYO MWANADAMU YEYOTE YULE.
(1 WAKORINTHO 15:
45-49).
BWANA YESU ASIFIWE watu wote wa mataifa yote, wakristo,
wapagani na wengineo wote mlioumbwa kama wanadamu, nawasalimu kwa jina la mwana
wa MUNGU wa pekee ambaye ndiye YESU WA NAZARETI aliyekuja duniani akafanyika
kuwa yeye ndiye Adamu wa pili. Nitaelezea kwanza kwa nini YESU anaitwa ndiye
Adamu wa pili? Hii ni sababu MUNGU alikwisha muumba mwanadamu wa kwanza na
akampa jina Adamu huyu ndiye Adamu wa kwanza na ambaye kupitia yeye tunaitwa
wanadamu kwa heshima ya jina lake na kama ndiye mtu wa kwanza kuumbwa na
mwenyezi MUNGU, baada ya Adamu wa kwanza kuanguka katika bustani ya Edeni
akiwemo na mke wake Eva soma katika kitabu cha
Mwanzo 3 yote.
Hivyo basi haikuwezekana tena binadamu ajikomboe tena kutoka
katika mikono ya shetani. Ikabidi sasa MUNGU amlete mtu wa mbinguni mwenye
nafsi yake akiwa na sura ya mbinguni ili aje aukomboe ulimwengu akazaliwa kwa
kupitia Mama Maria ndiye aliyeibeba hii mimba kwa uwezo wa ROHO MTAKATIFU bila
ya kubeba uja uzito wa mwanadamu, ndiyo sababu YESU anaitwa Adamu wa pili
sababu yeye alitoka mbinguni na ndio sababu Mama Maria hata ukisoma biblia
utaona mchumba wake Yusuph akimkuta tayari ana mimba japo ni bikira ila
akaeleweshwa na MUNGU kupitia ndoto akaelewa.
YAFUATAYO
NI MANENO KUTOKA KATIKA BIBLIA YANAYOHAKIKISHA YESU NDIYE ADAMU WA PILI NA SIYO
BINADAMU MWINGINE.
a)
Daniel 7: 13-14: nikaona katika njozi za usiku,
na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu
akamkaribia huyo mzee wa usiku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na
utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote
wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na
ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.
Sasa hapa unaona unabii ambao ulioandikwa kuhusu
mwanadamu atokaye mbinguni na akaja ambaye yeye ndiye aliyepewa mamlaka yote ya
kutawala mataifa yote ni kwa lugha zote na mamlaka yake ni ya milele. Sasa huyu
ndiye Adamu wa pili, sasa cha ajabu wametokea waongo wanaomkufuru MUNGU kwa
kuchukua utukufu wa YESU na kujiita Adamu wa pili, sasa jamani hauoni huu ni
ushetani wa kumchokoza YESU wa kulipindua neno lake? Je anayejiita Adamu wa
pili yeye ndiye anayetawala mataifa yote zaidi kushinda YESU? Jibu, siyo. Swali
lingine je biblia imetuagiza tutumie jina lipi? Jibu ni YESU WA NAZARETI. Sasa mpaka
hapo uelewe ni dhambi na ni ushetani kuingilia cheo cha YESU au kujiita wewe ni
YESU.
b)
1 Wakorintho 15: 45- 49- ndivyo ilivyoandikwa,
mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyohai; Adamu wa mwisho ni roho yenye
kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule
wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili hutoka
mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama
alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama
tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye
aliye wa mbinguni.
Hapa ni mistari ambayo inakuhakikishia kuwa YESU ndiye Adamu
wa pili. Adamu wa pili ametoka mbinguni ambaye ndiye YESU alitoka mbinguni
akazaliwa kwa sura ya mwana wa Adamu, ndiye sababu anaitwa Adamu wa pili na
ilitabiriwa akatokea na akaja hapa ulimwenguni akaifanya kazi yake akaimaliza akarudi
mbinguni. Sasa hivi tunasubiri aje katika unyakuo kulinyakua kanisa.
Mpaka hapa umeshapata picha ya ukweli kuwa YESU ndiye Adamu
wa pili sababu nimekula sifa za kweli za Adamu wa kweli ambaye ndiye YESU WA
NAZARETI na hata katika ulimwengu wote hakuna jina lenye nguvu na mamlaka kama
la YESU WA NAZARETI.
Swali je binadamu akijiita yeye ni Adamu wa pili je hauoni
huyu anavuruga mpango wa MUNGU ili kuwapoteza watu waende Jehanamu kama wenyewe
watakavyo kwenda na wengine tayari wamesha kwenda kusubiri hukumu ya moto? Kila
bara watumishi wa ajabu ajabu wametokea ili kuwapoteza hata wale wateule.
Kila mtu unayoisoma biblia na unayo akili timamu kama haujatekwa
na shetani au fikra zako kufungwa lazima utakubaliana na mimi Nabii Hebron
kuhusu kuwa hakuna Adamu wa pili tena zaidi ya YESU. Kama atatokea ajiite hivyo
au alishatokea muelewe huyo ni muwongo na ni adui wa MUNGU na pia amechukua
utukufu wa MUNGU na kumpinga YESU yeye hajui lolote, au kwa maana nyingine,
niulize swali sababu umeshajua Adamu wa kwanza alitokana na mavumbi na Adamu wa
pili 1 Korintho 15: 47 alitoka mbinguni, sasa hivi inaingia katika akili yako
mtu amezaliwa hapa duniani, ametenda dhambi, wala hajatabiriwa kuwa yeye kwa
jina lake ataumiliki ulimwengu kama YESU? Sasa hauoni wanaojiita hivyo ni
waongo? Na unapokuwa chini yao ina maana unatawaliwa na wao na siyo YESU wala
MUNGU sababu MUNGU hajapanga hivyo ila shetani ili awateke watu fahamu na
awamiliki anawatumia wale watumishi ambao yamkini YESU aliwaita hapo mwanzoni
na wengine wamejiita wakamsaliti yeye sasa shetani anawatumia hao hao ili
kuwapoteza wanadamu kama ilivyo sasa. Hii ni dalili tosha uelewe watumishi
walivyomsaliti YESU mpaka shetani akateka kama 98% ya watu wote wa ulimwengu
huu.
Jambo lingine niwaulize swali je YESU hakuimaliza kazi yake
hapa ulimwenguni? Jibu, alimaliza. Sasa wengine wanakuja kuwadanganya watoto wa
MUNGU eti YESU hakuifanya kazi yote aliyotumwa? Je inakuingia katika akili
yako? Wanaosema YESU hakumaliza kazi yake aliyotumwa na MUNGU hao ni waongo na
ndani yao ni Lusifa anaongea siyo roho wa MUNGU.
Yohana 1:1, 14, Mathayo 11:9-14 SOMA.
NOTE:
Mimi kama mimi Nabii Hebron, nawasihi watu wote huu ni
wakati mbaya na wa hatari sana YESU ambaye ndiye Adamu wa pili, muda wowote
atarudi kulinyakua kanisa lake ila siku na muda hiyo sijui. Utaulizwa wewe je uliliteteaje
jina lake pale lilipochafuliwa? Au kama unampenda kweli YESU kwa nini
usiwaeleze watu ukweli wasidanganyike pale ambapo hata wanadamu wanajifananisha
na yeye wakati tunajua hakuna zaidi ya YESU aliyetoka mbinguni akawa binadamu? Akaishi
na wanadamu kisha akapaa na atakuja kulinyakua kanisa lake!
Na siku moja nilikuwa naongea na YESU 2013 akaniambia
Hebron, hivi mwanadamu ni nani mpaka ajifananishe na MUNGU? Kama YESU mwenyewe
anachukia pia na Malaika wanachukia, je ni nani ajiite yeye ni MUNGU wa majeshi? Sasa kama
yeye ni MUNGU wa majeshi na anaonekana kwa macho ya wanadamu basi kila mtu
angekufa sababu imeandikwa hauwezi ukamuona MUNGU halafu ukaishi. Sasa kama
tunaishi au unaishi na umemuona mtu anajiita yeye ni MUNGU wa majeshi basi hiyo
ni picha halisi yeye ni adui wa MUNGU kama vile shetani alivyotaka kuuchukua
utukufu wa MUNGU akatupwa kuzimu na ndivyo njia ni moja na hata atakayemuamini
mtu wa jinsi hiyo na yeye atafuata njia hiyo hiyo. Tazama hata shetani
alipofukuzwa mbinguni alifukuzwa na wafuasi wake ambao ndio malaika waliomuasi
MUNGU. Najua hata sasa watu wanatengenezewa njia ya kumuasi MUNGU ili wachomwe
moto na wao hawajui wanatekwa fahamu na akili zao.
Sasa mfunguke fahamu na akili watu wote wa mataifa yote
msiamini kabisa mtu yeyote awe ni Nabii, Mtume, Mchungaji, Mwinjilisti au
kiumbe chochote kile. Kitakachojiita chenyewe ndio Adamu wa pili, anayo mapepo
siyo ROHO MTAKATIFU 100% wala hapeleki mtu kwa YESU bali ni kwa shetani. Adamu wa
pili ni YESU WA NAZARETI ndiye tuliyopewa zawadi na MUNGU ili kupitia yeye ndio
njia atufikishe mbinguni na atulinde! Sasa iweje wengine katika nchi mbali
mbali wajiite wao ni Adamu wa pili? Je inakuingia katika akili yako? Nawasihii kama
unapenda usiende Jehanamu epuka na watu wote wanaojiita wao ni YESU au MUNGU wa
majeshi au ROHO MTAKATIFU. Hao ni wapinga Kristo.
Jambo lingine Adamu wa pili anaishi milele na ndiye
atakayekuja kuuhukumu ulimwengu na ndiye atakayekuja kulinyakua kanisa ambaye
ndiye YESU WA NAZARETI. Sasa swali je hawa wanaojiita Adamu wa pili ndio
watakao uhukumu ulimwengu?? Jibu siyo na je wanaishi mbinguni kama YESU au wapo
hapa hapa tu kama wewe? Na pia niulize swali, je YESU anafananishwa na mtu
yeyote? Jibu hakuna. Watoto wa MUNGU ulimwengu umemgeukia shetani, sasa mnaomjua YESU wa kweli mpinge kwa nguvu watu wanaobadilisha biblia na pia
akatokea mtu mwingine ajiite yeye ndiyo Adamu wa kwanza, nawatangazia hao ni
mapepo kutoka kuzimu kwenye asili ya baba yao wa uongo. Akitokea mtu anajiita
yeye ndiye Adamu wa kwanza elewa yeye ni muwongo na ni adui wa MUNGU. Akitokea ajiite
yeye ni Adamu wa pili mjue yeye ni adui wa YESU 100%.
Sema BWANA YESU naomba unisamehe dhambi zangu, unitoe katika
mikono ya watumishi wa jinsi hii ili nisiangamie. Uniandike jina langu upya
katika kitabu chako cha uzima wa milele, najitenga nao kiroho na kimwili
najikabidhi kwako wewe uliye Adamu wa pili kutoka mbinguni ambaye ndiye YESU WA
NAZARETI. Uniongoze, unilinde, mi simtaki shetani tena, nimetambua kwamba
nilikuwa katika upande wa adui yako. Amen.
NABII HEBRON.