YESU
ANASEMA HAMNITAKI MIMI, LAKINI AKIJA MWINGINE MNAMTAKA!
YOHANA 5:37-47
“ 37Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti
yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona. 38Wala Neno
lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwakua ninyi hammwamini yule aliyetumwa na Yeye.
39Mwayachunguza maandiko, kwasababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima
wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. 40Wala hamtaki
kuja kwangu mpate kuwa na uzima. 41Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu.
42Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa MUNGU ndani yenu.
43Mimi nimekuja kwa jina la BABA yangu, wala ninyi hamnipokei;
mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo. 44Mwawezaje
kuaamini ninyi mnaopeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utako kwa
MUNGU aliye wa pekee hamuutafuti? 45Msidhani kwamba mimi
nitawashtaki kwa BABA; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. 46Kwa
maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika
habari zngu. 47Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi
maneno yangu?”
BWANA YESU ASIFIWE watu wa
mataifa yote. Karibuni katika neno hili ili kujifunza zaidi na kumwelewa YESU
vizuri, ambaye ndiye BWANA na mwokozi wa ulimwengu wote na ni mfalme wa
wafalme.
Napenda kila mtu yule
anayempenda YESU aelewe na aangalie asije akampenda yule mwingine ambaye ndiye
adui na kumtaka pasipo kujua au kwa kujua badala ya kumpenda YESU. Katika
ulimwengu huu wa sasa yale yaliyosemwa na YESU sasa yanaonekana na mengine
yanafuatwa na watu pasipo kujua na wengine kwa kujua. Amenituma niwaeleze kwa sababu
yeye ni mwema kwako, anakupenda, ana wivu juu yako na hataki akukose katika
ufalme wake. Anataka kama ukimkubali siku moja ufike mbinguni. Ila kama
ukimkataa na yeye atakukataa, huu ndio wakati wako wa kupanda utakachovuna
katika ile siku ya mwisho ya kutengwa ngano na pumba.
Yamkini wewe ni ngano basi
usigeuke ukawa ni pumba na kama kwa sasa ni pumba basi ugeuke ukawe ngano. Je
kwa msemo huu YESU anamaanisha nini akisema mimi hamnitaki, lakini akija
mwingine huyo mtamtaka? Swali lingine hapa, je huyo mwingine ni nani? Anaitwa
nani? Anatoka wapi? Yukoje? Hili ni fumbo. YESU alimaanisha kuwa huyo mwingine
ni mtu atakaye litumia jina la YESU kwa kuchanganya na mapokeo ya wanadamu au kwa
kuweka sheria zake ambazo sizo za YESU na wala si zile zilizoletwa na MUNGU, kwamba
hizo mtazitaka ila zile alizozileta mwana wa pekee hamzitaki ambazo ni zenye
ukweli na zenye uzima, bali zile zenye uongo na zisizo na uzima wa milele hizo
mnazitaka, hii ni kuhakikisha baadhi hawamtaki YESU kwa kujua na wengine kwa
kutojua wakati nia ya mioyo yao ni kumpenda YESU. Mpaka hapo mtakua mmeelewa
kwa kiasi fulani.
Uthibitisho katika hayo utaupata
kwa mambo aliyoyakataa YESU na yale ambayo yameletwa na huyo mwingine
asiyejulikana au hajatokea mbinguni:
1.
Ubatizo wa maji mengi ya mtoni, ni wachache
wanaukubali (kumkubali YESU);
2.
Ubatizo wa kisima (kumkataa YESU na kumkubali
huyo mwingine anayetumia jina la YESU).
3.
Ubatizo wa kupigwa na fagio, huo sio wa YESU, bali
wapo wanao mkubali huyo mwingine huku wakitumia jina la YESU.
4.
YESU hakubatizwa kwenye maji ya kikombe na wala haijaandikwa
watu wabatizwe hivyo, lakini Neno la YESU limetimia. Akisema mimi hamnitaki
lakini huyo mwingine atakuja mtamtaka, mpaka hapo hakuna ubishi. Haijlishi
unayachunguza maandiko kama vile unao uzima na kumbe kwa kumtamka huyu mwingine
tu unakua unapoteza uzima wako wa milele. Hata ukisoma kitabu cha UFUNUO
22: 18-19, MUNGU ameonya.
5.
Imeandikwa watu waombewe bure bila kutozwa pesa,
utaona hapa baadhi ya wahubiri wanataka vitu vya YESU na jina lake lakini
hawataki Neno lake, wanataka neno la huyo mwingine la kuwatoza watu pesa za
kuombea watu. Hata baadhi ya watumishi katika ulimwengu huu hawamtaki YESU
wanamtaka huyo mwingine na hata kuwafanya mataifa kuingizwa katika ufalme wa
shetani pasipo kujua au kwa kujua, ila baadhi yao ni wakala wa shetani kabisa na
wanajua wanachokifanya, walichotumwa na boss wao shetani au amiri jeshi mkuu wao
wa kuzimu. Kitu cha kujiuliza, je kwa kuwadai pesa za maombezi, si wanamkana
YESU na neno lake na kumkimbilia huyo mwingine ambaye ni mpinga kristo
anayelitumia jina la YESU. Mwenye akili na aelewe, mwenye masikio na asikie.
6.
Watu wanataka miujiza ya kipepo, hawataki ile ya
YESU. Kwa mfano, miujiza ya kutolewa konokono au mawe na mengineyo, hiyo watu
wengi wanaitaka wakati miujiza hii ni ya kichawi na ni ya kipepo. YESU aliomba
roho chafu zikawatoka watu na pia YESU amesema twende kiroho na sio kimwili, sasa
miujiza mingi ni ya kimwili ya yule mwingine. Lakini pia napenda uelewe kwamba MUNGU
anampa mtu uhuru wa kuchagua, aidha kwenda mbingni au jehanamu. Wewe mwenyewe
ndiye mwenye hatima ya maisha yako, isije ikakukuta siku ile mbaya ya hukumu na majuto ya
milele. Isije ukajikuta wewe mwenye
bahati mbaya aliyemtaka huyo mwingine uko mbele ya YESU akikwambia toka hapa
sikujui sikujui na mwingine aliyemtaka YESU apite kwenye mlango wa uzima.
Wengine watasema nilikua
nafunga na kuomba, nalala kanisani, nahubiri, nilitoa pepo kwa jina lako; YESU
atakwambia sikukujua tokea siku hizo kama ilivyo sasa. Yakupasa wewe mwenyewe kujipima
upo katika nafasi gani na kama haujui na sasa umefunguka ufahamu badilika maana
ulidanganywa na huyo mwingine. Inawezekana huyo mwingine ameamuru uabudu
sanamu, abudu wafu, batizwa ukiwa mtoto mdogo, andika jina katika sadaka na
upewe risiti, hayo sio ya YESU. Utashangaa nyumba za ibada zinatumia jina la
YESU lakini baadhi zinamtaka huyo mwingine. Huyo mwingine ni mafundisho ya
uongo au mapokeo ya wanadamu. Shetani anatumia njia hii kuliteka kanisa ili
aliangushe, kama alivyoliangusha katika baadhi ya sehemu huku wakipigwa upofu
wajione wako sawa kumbe wapo vifungoni.
Huyu mwingine ni harambee au
michango katika nyumba za ibada. Huyu mwingine ni kanisa kukopa benki ili
kujenga kanisa. Ukisoma Neno, YESU anasema usijisumbue kwa lolote niulize mimi,
sasa mwataka kusema je ni YESU ndiye
anayewaongoza wachungaji, mitume, walimu, manabii kwenda kumkopea YESU pesa za
ujenzi wa kanisa? Jibu ni hapana na YESU sio masikini, vitu vyote vipo chini
yake , pesa na dhahabu ni zake, sasa iweje aishiwe? Napenda muelewe huyo
mwingine ndiye masikini. Anaongoza kwa kulitumia jina la YESU na ndio sababu
YESU anasema huyo mtamkubali, na ni kweli huyo mwingine anakubaliwa sana na
kumbe pasipo watu kujua au kwa kujua wamemkubali shetani. Huyu mwovu anayo
mitego mingi sana inahitajika neema ya MUNGU kuyajua haya yaliyofichika. Na
zaidi Biblia ambacho ni kitabu kitakatifu, Neno la MUNGU linasema usilipe riba.
Sasa huyu MUNGU anabadilika? Hapa sasa uelewe dunia kwa kiasi kikubwa ipo katika upande wa huyo mwingine ambaye sio
YESU.
ANGALIZO:
Dunia hii katika kipindi hiki cha mwisho cha kuungojea
ujio wa YESU, pamoja na kila mtu kulipwa ujira wake na YESU, haipendi ukweli wa Neno kwa watu wengi, bali wanapenda
kuchanganya uongo na Neno la MUNGU, hii haikubaliki na haifai, utakapokata roho
utaenda kwa uliyempenda kwa sababu MUNGU yeye ni MUNGU wa haki na hata huyu
mshtaki atakushtaki mbele za YESU siku ya hukumu. Badili nia yako na mkatae
huyo mwingine utamjua alivyo tofauti na neon,
mwongozo usiotoka mbinguni. Wewe ni msafiri wa kwenda mbinguni, sasa
haiwezekani upo kwenye njia ya jehanamu ukifikiri unaenda mbinguni, njia ya
jehanamu haiendi mbinguni au kwa lugha nyingine njia ya huyo mwingine sio
salama.
Sema, BWANA
YESU naomba unisamehe dhambi zangu zote ikiwepo na hii ya kumtaka huyo mwingine,
simtaki kuanzia ndani ya roho yangu na nje. Nakuhitaji wewe mwana wa MUNGU wa
kweli uniandike katika kitabu chako cha uzima wa milele, nibadilishe, niponye
fahamu, nifungue nikujue wewe YESU, naomba uniongoze pamoja na Roho Wako Mtakatifu,
AMEN.
YESU akutunze.
Kwa mafundisho zaidi tembelea
website yangu www.prophethebron.org
na YouTube: Prophet Hebron.
NABII HEBRON WILSON KISAMO.