BWANA YESU ASIFIWE, kwa wakristo wote katika ulimwengu wote na hata wale ambao siyo wakristo, wote nawasalimia.
Najua kuwa baadhi ya watu watashangaa maneno haya ninayoueleza ulimwengu, kwa kusema kuwa ipo miungu ya kikristo kwa sababu miungu hiyo ilijificha kwa miaka mingi bila kujulikana na watu na hata kwa wakristo wenyewe. Shetani alijua kabisa kuwa wakristo hawashikiliwi na miungu kwa sababu KRISTO ni Mwana wa MUNGU aliye hai, na mkumbuke kuwa Kristo mwenyewe alishasema “wengi watakuja wakilitumia JINA langu ili kuwapotosha watu yamkini hata wateule” na sasa maneno aliyoyasema YESU yameshatimia. Baadhi ya wakristo kwa sasa, aidha kwa kufahamu au kwa kutokufahamu wanajua fika kuwa wanaabudu miungu ya wakristo badala ya kumwabudu YESU Kristo aliye hai.
Ukisoma katika kitabu cha Kutoka 20:3-5, MUNGU anasema “usiwe na miungu mingine” yeye alijua kuwa miungu ipo kwa kusudi la kuwapoteza wanadamu na ndio sababu alitoa taarifa ya kwamba isiabudiwe tena, na wala si kwa kutumia mfano wa kitu chochote mbinguni au chini ya ya dunia hii.
Miungu hii ya kikristo huwezi kuiona kwa macho ya damu na nyama, bali hizo ni roho za mpinga Kristo, ambazo ndizo zinawaongoza baadhi ya Wakristo kuelekea Jehanam na baadhi yao wanadhani kuwa wanaenda mbinguni na kumbe wameshatekwa na miungu ya kikristo.
JINSI YA KUITAMBUA MIUNGU YA KIKRISTO
Kila mtu anajua kuwa YESU alileta wokovu na sio dini, wala dhehebu lolote lile, cha kushangaza, imeingia hii aina ya miungu ya kikristo iliyoanzisha ukristo ambao ni tofauti na ule ukristo ambao YESU wa Mbinguni aliouanzisha. Miungu hiyo ya kikristo iliwaingizia wanadamu roho zake, na iliwaelekeza na kuwaongoza watumishi wake, na inaendelea kufanya hivyo hata sasa katika ulimwengu wote. Baadhi ya sehemu wakaruhusu mtu awe mkristo lakini asiokoke, miungu hiyo ikaleta aina nyingi za ubatizo ambao YESU wa Mbinguni hakubatizwa kwa namna hizo na kwa njia hiyo. Unapobatizwa tofauti na vile ambavyo YESU alivyobatizwa unakuwa umeingia agano la kiapo cha kuwa mwanafunzi wa miungu ya kikristo na unaitwa ubatizo wa miungu ya kikristo. MUNGU anamjua YESU, na MUNGU ndiye aliyeumba kila kitu, ndiye aliye tuumba sisi wanadamu. Swali, je inakuaje unakubali kubatizwa ubatizo wa yesu asiyejulikana (ubatizo ambao ni tofauti na ule aliobatizwa YESU WA MBINGUNI)? Hii inawafanya wakristo waingie katika agano na mikataba na yesu asiyejulikana, japo wakristo wao wanafikiri kuwa wanamjua au kumwabudu YESU wa Mbinguni, kumbe ukweli wanamwabudu na kumjua yesu wa miungu. Miungu haijulikani na hata hizo aina za ubatizo hazipo katika Biblia. Soma katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 18:19, Neno lake linasema anayefanya tofauti na Neno lake kwa kulipunguza au kwa kuliongeza basi hataenda mbinguni. Nataka pia uelewe ya kuwa Neno linaongelea juu ya wakristo ambao wanasoma Biblia kama Katiba yao na wanapoenda kinyume na Katiba yao yaani Biblia, hapo hakuna kwenda Mbinguni. Hapo ndipo shetani nae anashangilia kwa sababu watu wengi hawajitambui au hawajatambua kuwa wao wanajiita wakristo lakini sio wafuasi wa YESU wa Mbinguni bali wamekuwa wafuasi wa yesu wa miungu, ina maana hii miungu ya kikristo imewashikilia watu wengi sana ila wakati umefika sasa ni lazima iachwe katika Jina la YESU, ili mataifa wamfuate YESU wa Mbinguni na siyo yesu wa miungu.
AINA ZA UBATIZO WA MIUNGU YA KIKRISTO
Ubatizo wa kikombe:
Ukisoma katika Biblia, hutaona mahali YESU wa Mbinguni alibatizwa hivyo, wala hakuna mahali utasoma kwamba YESU alibatizwa akiwa mtoto mdogo na zaidi huu ubatizo wa kikombe mtu humwagiwa maji kichwani tu tena akiwa kanisani katika nchi kavu. YESU alienda mtoni, hivyo basi ubatizo haufanyiki ndani ya kanisa na hivyo ndivyo alivyopanga MUNGU. Ubatizo unafanyika nje na katika mto na maji yanayotiririka wala sio katika bwawa, ziwa au bahari, na zaidi Neno baptized inamaanisha kuzamishwa; Mkristo soma hata katika kamusi inaelekeza hivyo. Elewa kwamba baadhi ya makanisa yanasema uongo, kwa maneno yao, hata wanapobatiza kwa jina la Baba, na la Mwana na Roho Mtakatifu, wakati wanawamwagia maji kichwani, hapo ndipo hii miungu inajiunganisha na akili ya mtu husika tokea hapo awali, miungu hii ilijiimarisha na injili zao za uongo na kutupiga upofu hata katika akili ili tusitambue ya kuwa tumemwagiwa maji kichwani na waliotufanyia hicho kitenda wanasema ni sawa na kuzamishwa. Neno hili au tendo hili ni la uongo; lakini maneno ya YESU wa mbinguni ni ya kweli, sasa kwa nini baadhi ya wachungaji wanasema maneno ya uongo tena madhabahuni! Kama ni mchungaji wa kweli angetakiwa aseme hivi “nakumwagia maji kwa jina la baba, mwana na roho mtakatifu asiyejulikana”, ambao ndio miungu ya kikristo (kwa sababu ubatizo wa kikombe sio wa Mbinguni). Hata mimi Hebron, nilipokuwa mtoto mdogo nilibatizwa na wala sikuzamishwa, walinimwagia hayo maji kichwani wakidai ni ubatizo kumbe sio, ila nashukuru kwani NEEMA ya YESU ilinitoa kwa miungu ya kikristo na sasa naichukia hiyo miungu kabisa. Ipo siri katika ulimwengu ya roho ambayo imefichika kupitia kile kikombe na beseni, unapomwagiwa yale maji ile miungu inachukua maisha yako na kuyapeleka kwenye ufalme wao na kuwapa baraka zako wafuasi wao ambao wamejiingiza katika ufalme wa giza, kama vile freemason, Iluminati na hata mizimu, wachawi na waganga. Hivyo basi, kila mtu asikilize na ajifunze. Soma vitabu nilivyoandika vya ubatizo kama vile YESU alivyoniagiza kwenu na kwa mataifa yote ili mpate kufunguka katika hizo kamba, na hata wengine walishabatizwa kwa kufuata mapokeo ambayo wanajua kuwa ni kazi ya shetani. Siku ile ya mwisho utaulizwa na majibu yake ni kwenda katika ziwa la moto tu. Sasa kubali uokoke na ubatizwe na uachane na miungu ya kikristo, na siyo unaokoka na kurudi huko tena (kwenye miungu), la hasha, utakuwa bado unajipeleka gerezani na utakamatwa tu na hiyo miungu niliyokufundisha.
Ubatizo wa kisima:
Kibinadamu, ukibatizwa kwenye kisima utaona ni sawa kabisa, kwa maana umezamishwa katika maji mengi, swali la kujiuliza, je YESU wa mbinguni alibatizwa katika kisima? Na je MUNGU aliandaa kisima kilichojengwa na mikono ya mwanadamu kwa ajili ya ubatizo? Jibu ni kwamba MUNGU hakuandaa kisima bali yeye aliagiza mtu abatizwe katika mto ambao ni kazi ya mikono ya MUNGU na sio kisima. Endapo umebatizwa katika kisima unakuwa umepokea ubatizo wa maji mengi ya kisima ya miungu ya kikristo na unakuwa bado umepotea.
Ubatizo wa maji mengi lakini unabatizwa kwa jina la Mchungaji:
Naomba nikuulize ni wapi imeandikwa kuwa watu wabatizwe kwa jina la Mchungaji au kwa jina la Nabii na wengineo? Hakuna! Soma Mathayo 28:19-20. Tayari shetani na miungu yake ya kikristo inajiongezea nafasi katika aina hiyo ya ubatizo, na zaidi huyo atendae hivyo anawaunganisha na miungu ya kikristo. Hao wanaoendelea kubatiza kwa majina yao baadhi yao ni wachawi. Mtumishi wa aina hiyo hupewa masharti kama alivyoelekezwa na shetani ambaye ndie anayewasaidia kuendesha hilo kanisa la miungu ya kikristo, ila kanisa hilo huitwa la YESU ili waumini wasikimbie. Mwenye ufahamu usikie, uyajue hayo na utende kama MUNGU atakavyo. Usiishi na kiapo cha miungu ya kikristo bali ishi na kiapo cha YESU wa Mbinguni.
Aina hizo za ubatizo ni tofauti na ubatizo ule ambao YESU alibatizwa. Haijalishi umeokoka na unasali kwenye kanisa la wokovu au lolote lile, bado utakuwa na kiapo cha miungu ya kikristo na watakuwa na uhalali na wewe kwa sababu unalo agano na wao, agano hili huvunjika pale tu ambapo utabatizwa ubatizo wa kweli, na utoke katika hiyo madhabahu, kwa sababu unatenda kazi na miungu ya kikristo na siyo Agano la MUNGU wa Mbinguni.
IMANI ZA MIUNGU YA KIKRISTO
Hizi ni imani ambazo zinafuatwa na wakristo kwa kujua au pasipo kujua, unakua ni mkristo na unaenda kanisani lakini unakuwa umefungwa ufahamu wako ili uamini kile unachoongozwa, ambacho ni tofauti na vile ambavyo MUNGU ameagiza; kwa mfano, unajiita mkristo lakini kanisani mnaabudu sanamu, au kanisani kuna sanamu, na hata wakati mwingine kuzibusu. Mkumbuke kuwa MUNGU alishasema asifananishwe na chochote, soma Kutoka 20:4-5, sasa mkristo kwa nini unaabudu sanamu, halafu unajiaminisha kuwa wewe ni mkristo wa mbinguni, wakati KRISTO aliyeko Mbinguni yeye na Baba yake NENO lao ni moja? Huoni huo ukristo ambao uko nao unakuwa tayari umeshamsaliti KRISTO kwa kufuata miungu ya kikristo? Elewa sasa na hasa kama unataka kwenda Mbinguni, achana na hayo mambo, hata madhabahu zenye sanamu na vinyago, hizo zimekufa, hayo yote MUNGU amekataa, vinyago visiabudiwe, sasa inakuaje kama kweli wewe ni mkristo, kwa nini una abudu kinyago cha sura ya mfano wa mtu fulani kilichotengenezwa na mwanadamu? Tayari ukristo huo unakuwa ni ukristo wa miungu ya kikristo.
Ipo imani ya miungu ya kikristo ya kufanya ibada za wafu. Neno linasema MUNGU yeye sio MUNGU wa wafu, sasa ni nini kinachokusababisha wewe mkristo ufanye ibada za wafu? Endapo unafanya ibada hizo uelewe kuwa ukristo wako ni wa miungu ya wafu na miungu ya kikristo, sasa usidanganyike na kuona tu umekuwa mkristo, jaribu kuchunguza ukristo wako na mafundisho unayopewa, kwa sababu YESU alisema atakuja mpinga Kristo na ndio hao sasa.
Ipo imani ya mafundisho ya uongo, yaani Neno linachanganywa na uongo, halafu mkristo anakubali, kwa mfano unaambiwa utoe pesa ndipo uombewe, sasa uelewe kuwa mtu huyo ndani yake anaongozwa na miungu ya kikristo na siyo MUNGU wa Mbinguni, na ndio sababu ndani ya moyo wake imejaa miungu ya kupenda pesa na alisemalo mtu ndilo lililomjaa moyo wake.
Zipo sadaka za miungu, na sadaka hizo hutolewa kwa njia zifuatazo:
Kuandika majina na kupewa risiti na na hata kupewa vyeti vya hongera, hizi sio sadaka za kupokeliwa na MUNGU wa Mbinguni bali miungu ndio huzipokea sadaka hizo, Soma Mathayo 6:2-4, zikiwemo pia sadaka zile za kupangiwa kiwango cha kutoa aina, hizo za sadaka ndizo ambazo zinaenda kwa miungu ya kikristo.
Sadaka za harambee ndani ya kanisa, ukisoma Marko 11:15-18, wakati huo YESU wa Mbinguni aliwakuta wakifanya harambee na kufanya nyumba ya BABA yake kuwa ni soko, akawafukuza, lakini sasa watu wengi wamesahau na kudhani kwamba wapo kanisani kumbe wako sokoni, wanalea wanyanny’anyi, waongo na miungu ya kikristo, na hii miungu imewapofusha watu na hata hawajui kuwa hii ni dhambi na hata hizi sadaka haziendi mbinguni bali zinakuwa kama zile za Kaini.
YESU wa mbinguni hapokei sadaka ambayo ni tofauti na zile ambazo alituachia maagizo yake. Kila mtu afunguke akili yake. Watu wengi waliotoa kwa jinsi hiyo ikiwamo mimi Hebron, ila siku moja nilipokuwa naongea na YESU akaniambia maneno haya “hata wewe uliwahi kutoa kwa miungu ya kikristo”, niliogapa sana na nilisikia kufa kwa sababu siipendi miungu ila nilitegwa na hiyo miungu kwa kupitia Jina la YESU, pengine ni kama ilivyo kwako na kwa wengine pia.
Watu wote napenda mjue kuhusu hili jina la YESU, kuna baadhi ya watumishi na madhabahu ambazo zinalitumia jina la YESU kutafutia pesa na kuwaibia watu au kuwatapeli, kuwa sadaka wanazotoa zinapokelewa na MUNGU wa Mbinguni, kumbe asilimia kubwa zilipokelewa na miungu ya kikristo.
YESU amenituma niwafakishie ujumbe huu, “anawapenda watu wote, anawaambia mtubu na mrejee kwake muachane na miungu ya kikristo, yeye YESU hajaleta dini yeyote, wala dhehebu lolote bali yeye YESU alileta wokovu kupitia yeye KRISTO. Dini ya kikristo tayari ilikuwa na mapokeo ya wanadamu au ya miungu na hata yeye YESU aliikuta dini, na BABA yake alimtuma yeye YESU kuja hapa duniani kwa sababu dini haimpeleki mtu mbinguni, ila yeye YESU ndiyo njia ya kumuunganisha kila mtu na Mbinguni, utakapomkubali na kuokoka na kuishi maisha matakatifu peke yake”, hata mkisoma katika nyaraka za injili mtaona dini ilikuwa ndio kipingamizi kikubwa cha kumpinga YESU, kupitia mafarisayo yaani watumishi (Masadukayo) kwa lugha za kiyahudi. Alisema, “mimi YESU ninakaribia kuja kuchukua KANISA langu na sio DINI, kwa sababu sijaleta DINI ila wokovu na mtu akikubali na kunifuata na kuamini katika roho na kweli na kubatizwa kama MIMI nilivyobatizwa, na kutimiza haki yote”.
Sema: Bwana YESU, naomba unisamehe dhambi zangu zote, namkataa shetani na miungu ya kikristo kwa majina yake, naomba uandika jina langu katika kitabu chako cha Mungu wa Mbinguni na utoe jina langu katika kitabu cha miungu ya kikristo, kwa sababu nilikukiri, nikaokoka na kumbe jina langu liliandikwa katika kitabu cha wokovu wa miungu ya kikristo. Siitaki tena miungu ya kikristo. Amen.