MWENYEZI MUNGU ANAULIZA
DUNIA NZIMA, KWA NINI HAMTAKI WOKOVU?
Mara kwa mara nimekuwa nikisikia
sauti ya MUNGU ikiniambia sema na dunia nzima, na leo hii nasema na dunia nzima,
MWENYEZI MUNGU ANAULIZA DUNIA NZIMA HIVI, KWA NINI HAMTAKI WOKOVU? Anasema na
watu wote, iwe ni raisi, iwe ni mtu tajiri, iwe ni mtu maarufu, iwe ni masikini anawauliza
kwa nini hamtaki wokovu? Kwa nini hamuitaki zawadi aliyowaletea ambayo ni BWANA
YESU? MUNGU anasema na mataifa yote; wazungu, wahindi, wachina, waafrika na
watu wote wa kila rangi KWA NINI HAMTAKI WOKOVU? Je, mnafikiri bila wokovu
mtaenda kwake? Mimi nawaambia hamuwezi kwenda, kusoma Biblia tu bila kuwa na
wokovu hauendi popote hata uwe una shahada (degree) tatu au nne za masomo
ya Biblia lakini bila wokovu mimi nakuambia ni kazi bure.
Tutasoma Neno la MUNGU kutoka
katika kitabu cha MARKO 7:1-3; “1Kisha Mafarisayo, na baadhi
ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake, 2wakaona wengine katika
wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. 3Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi
wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao.”
BWANA YESU asifiwe, hapa utaona mafarisayo
walivyokuwa wakiwashitaki wanafunzi wa YESU, lakini ukumbuke hawa wanafunzi wa
YESU kabla ya hapo nao walikuwa ni waumini wa Mafarisayo. MAFALISAYO NI WATUMISHI
NA WACHUNGAJI AMBAO NI WA DINI. YESU yeye hakuleta DINI ameleta wokovu kwa sababu wokovu umetoka kwa MUNGU, bali Mafarisayo
wao walikuwa na mapokeo ya wanadamu ya masharti-masharti na amri–amri. Biblia
inasema hivi, wao walikuwa na mapokeo ya wazee, haya mapokeo ya wazee
hayakupeleki popote yatakuacha hapa hapa duniani. Katika Dunia hii asilimia
kubwa ya mapokeo haya ya wanadamu wazee ndiyo yamewashika watu wengi sana. Amua
leo na uachane na mapokeo ya wanadamu wazee na uupokee wokovu wa kweli wa BWANA
YESU.
MARKO 7:4-5; “4tena
wakitoka sokoni, wasipotawadha, hawali; na yako mambo mengine waliyopokea
kuyashika, kama kuosha vikombe, na mindu na vyombo vya shaba. 5Basi wale mafarisayo na
waandishi wakamwuliza mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya
wazee bali hula chakula kwa mikono najisi?”Anasema hivi wakitoka sokoni wakiosha vikombe na mindu, maana yake ni madhabahu kwa sasa ndio zinaitwa sokoni, sasa hivi watu wengi wanaenda makanisani wakijua ni makanisa ya kweli kumbe tayari yameshakuwa ni masoko, lakini usiogope mwana wa MUNGU kwa sababu BWANA YESU alikuja ili haya masoko yafe, hili soko la kikanisa limeshika mizizi na kustawi sana duniani kote kwa asilimia kubwa na kama ni hisa (share) basi lina hisa (share) nyingi sana kwa shetani, kwa BWANA YESU ni chache sana.
Wewe unabatizwa kwa ubatizo wa kikombe
wa mapokeo ya wazee, je hayo ndiyo YESU aliyoyaagiza tuyafanye? BWANA YESU ni
zawadi iliyoletwa na MWENYEZI MUNGU, kwa sababu Dunia ilikuwa imeangamia, YESU alipokuja
hiyo ilikua ni zawadi tumeshushishiwa ili kwamba tukaurithi ufalme wa MUNGU,
lakini baadhi ya watu wanalitaka jina lake kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, watu
ambao walioanzisha mambo hayo hata hawawajui. Wengine ni wazungu na wengine ni
waafrika, ndio maana sasa hivi kanisani watu wengi wamekata tamaa na BWANA YESU
kwa sababu ya mapokeo ya wazee, siku hizi kama ni uganga na uchawi ndio umejaa
makanisani, msiseme huko nje ndio kuna uchawi, makanisani ndio uchawi umejaa. Lazima
nikuambie ukweli ili ukapate kupona, usiwe mnafiki kwa MWENYEZI MUNGU, kama
kweli unampenda kwa nini mpaka sasa hautaki kuupokea wokovu aliotuletea kama
zawadi? Jua kwamba, kwa wewe kuupokea wokovu ndio tiketi yako ya wewe kwenda
mbinguni na kuurithi ufalme na BWANA YESU.
MARKO 7:6; “6Akawaambia,
Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, watu hawa
huniheshimu kwa midomo Ila mioyo yao iko mbali name; nao waniabudu bure,
wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu. 7 Nao waniabudu
bure, kwa kuyafuata mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu, 8 Ninyi
mwaiacha amri ya MUNGU, na kuyashika mapokeo wanadamu. 9Akawaambia,
vema! Mwaikataa amri ya MUNGU mpate kuyashika mapokeo yenu”.
Watu hawataki kweli ya MUNGU
aliyoileta YESU, wanataka ya wanadamu, MUNGU anauliza leo, MNATAKA WOKOVU
ALIOULETA MWANAE YESU WA NAZARETI KWA KUJA DUNIANI AU MNATAKA
MAPOKEO YA WANADAMU? Yamkini ulikuwa hujui, fanya maamuzi sasa, kataa mapokeo
ya wanadamu na uokoke, jua kwamba mtu yeyote ambaye hajaokoka huyo amekwisha
kumkataa MUNGU kabisa, kama ulikuwa hujui sasa uelewe.
MUNGU yeye aliamua kumleta mwanae
YESU kwa sababu Dunia yote ilikuwa imeangamia, amua leo na umpokee BWANA YESU,
Mfalme wa ulimwengu huu kwa njia ya utakatifu umpokee na umuamini, kwa sababu
kuna baadhi ya makanisa leo hii wanawafundisha waumini kwamba wamuamini YESU tu
bila wokovu, mimi nakuambia hapo unapoteza muda wako, ondoka ukatengwe nao,
ukristo tu bila wokovu hatakwenda mbinguni.
YESU anasema enyi wanafiki, hii
imeandikwa miaka mingi sana na ikatabiriwa na leo hii ndiyo mambo yalivyo, watu
ni wanafiki, utamkuta mtu anasema yeye ni mkristo safi kwa kwenda kanisani na
kukesha lakini ukimwambia mambo ya sala ya toba hataki, sasa ujue kwamba mtu
huyo ni mnafiki, hata kama ni Mchungaji yeye ni mnafiki tu, awe ni Askofu au ni
Nabii jua kwamba hao wote ni wanafiki, hivi ndiyo tunavyopotezwa na mambo ya
kizee. Haya mambo ya kizee nitayashughulia dunia nzima kwa Jina la YESU ili
watu wakapate kupona. YESU yeye alianzisha huduma tano (5) lakini sasa hivi
kuna baadhi ya makanisa yana huduma sita (6) ya uaskofu, YESU yeye hakuleta
huduma ya uaskofu, askofu ni mtu wa kufagia kanisani mwenye mke mmoja, lakini
leo hii nashangaa kuna baadhi ya maaskofu wanaume hawajaoa hayo mambo yametoka
wapi, soma Biblia inasemaje YESU anawauliza kwa nini hamtaki vitu
alivyovianzisha Yeye? Na kutaka vitu vya wazee na vya masokoni? Tokeni hukona muupokee
wokovu wa kweli.
MARKO 7:13; “13Huku
mkilitangua neno la MUNGU kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo
mengi yaliyo sawasawa na hayo”.
Neno la MUNGU siku hizi linahubiriwa
kwa kuchanganywa na mambo mengine ambayo ni mafundisho yaliyo mapokeo ya wanadamu,
utamkuta Mchungaji anahubiri anatumia Biblia kwa kuchanganya na mambo mengine
yanayofanana na Biblia ambayo ni mapokeo ya wanadamu kwa kuweka michango makanisani, mtu kama huyo ni mnafiki na siyo mtumishi wa MUNGU.
Huyu YESU anawapenda watu sana,
anasema njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo
nitawatua, sasa leo hii ukisikia kuna mahubiri sehemu, badala ya wewe kwenda
kutuliwa mizigo wewe ndiye unayeenda kupewa mizigo. Watu wengi wanahubiri
habari za YESU, mtumishi anakwambia lete pesa au gari ndio uombewe, hapana, tusifanywe
wapumbavu, sadaka ni uamuzi wako wewe mwenyewe kwa utukufu wa MUNGU na siyo
kutengenezewa mazingira ya kukuchukulia pesa, hivi ndiyo Dunia ilivyoharibika. Sehemu kubwa hakuna YESU ni utapeli tu, watu
watasema, BWANA YESU asifiwe tuko na BWANA YESU, lakini utawakuta wanaabudu
sanamu, wanabusu mbao, sasa tunakwenda wapi? Hapana, huo ni unafiki, sasa YESU
anauliza mnamtaka Yeye au mnayataka mapokeo ya wanadamu?
MATENDO 4:10-12; “10Jueni
ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,
ambaye ninyi mlimsulubisha, na MUNGU akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu
anasimama alimzima mbele yenu. 11Yeye
ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu
la pembeni. 12Wala hakuna wokovu kwa mwingine awaye yote, kwa maana
hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi
kuiokolewa kwalo”
Hapa Neno la MUNGU linatuambia
kwamba hakuna jina lingine lililopewa wanadamu, siyo jina langu mimi Hebron, siyo
Musa, siyo Eliya wala siyo Maria. Mimi nashangaa sana mtu akimwabudu Maria,
wakati Maria mwenyewe ukisoma kwenye Biblia anamwambia mwanae YESU kwamba mwokozi
wangu ninakuabudu, sasa wewe ni nani wa kumwabudu Maria? Hayo ni mambo ya wazee wenye kufuata mapokeo
yaliyo ya wanadamu, mtu yeyote hawezi kumwomba MUNGU pasipo kuokoka ili kuweza
kuunganika na yeye, ni wewe mwenyewe kuamua unataka kuangamia au unamtaka MUNGU.
Mheshimiwa BWANA YESU anakuja,
nyakati hizi ni za mwisho, ninakwambia usimame imara na ubadilike sasa, uachane
na hadithi (stories) za mapokeo ya wazee, na pia utoke huko katika kambi
zao, kwa sababu haya mambo ya kizee yameletwa kwa lengo la kuwaharibu wanadamu na
watu wengi kwa sasa wamekuwa ni mavuno ya shetani. YESU alisema watatumia jina
langu kuwapoteza wengi na ndivyo ilivyo kwa sasa. Upo wokovu wa kidunia, na hii
yote ni kuhakikisha kwamba dunia inakukamata na kukufanya wewe usiweze kwenda mbinguni,
sasa ni ajabu sana wokovu huu wa kishetani ndio watu wanautaka kwa kubatizwa
ubatizo wa kisima halafu unajidanganya utaenda mbinguni, mbingu ipi hiyo, ya
ubatizo wa kisima na wa kikombe? Mimi nakuambia huwezi kwenda mbinguni kwa
batizo kama hizo, badili mawazo yako sasa na ukabatizwe upya kama BWANA YESU, kwa
sababu yeye ndiye atakaye tuwezesha sisi tuweze kufika mbinguni.
YESU yeye ni wa mbinguni na sisi
wanadamu wote tunatakiwa kwenda mbinguni, sasa ni lazima tuupokee wokovu wa
mbinguni kwanza ili tuweze kwenda mbinguni, dunia hii baadhi ya watu wengi
wamekuwa ni wanafiki tu wanaenda makanisani asubuhi hadi jioni wakisema BWANA
YESU asifiwe na kusema kuwa wanampenda YESU kwa kutoka kanisani ibada ya kwanza
ya pili au ya tatu lakini wao hawajaokoka, mimi nawaambia watu wote mnaofanya
hivyo hamjamjua MUNGU bado, lazima nikuambie ukweli, haitanifaa mimi nikuone
wewe unaangamia na nisikuambie ukweli, mimi siyo mnafiki nakuambia ukweli
ukubali ukatae hiyo ni shauri yako.
MUNGU yeye hakuleta dini wala
hakuleta dhehebu, na wala si dhehebu au dini itakayoweza kukupeleka wewe
mbinguni ni BWANA YESU tu tena ukiwa umeokoka, kwa sababu dini na dhehebu
halikutoka mbinguni bali kwa wanadamu kwa mipango yao wenyewe ya namna ya
kumtafuta MUNGU kwa njia za utapeli tapeli tu, kuchukulia wana wa MUNGU pesa
zao na kuwaongoza kwenda jehanamu, YESU anasema hivi yeye ndiye njia ya uzima
na kweli. Sasa nakusihi mwana wa MUNGU, mpokee YESU naye atakuonyesha njia ya
kufika mbinguni, kwa njia ya wokovu wake wa kweli.
Hakuna dini au dhehebu hata moja
ambalo MUNGU amelileta kutoka mbinguni, yeye alimleta BWANA YESU TU na YESU
hakuja hapa duniani kusema dini hii au dhehebu lile, YESU alisema yeye ameleta
wokovu, sasa mfuate YESU na umpokee kwa kumkiri yeye akupe wokovu wa
kukufikisha wewe mbinguni. Wokovu maana yake ni kuokolewa. Dini
na dhehebu maaana yake ni wazee wa dunia hii sasa chagua leo uamuzi ni wako.
MUNGU ameniambia, waambie Dunia
nzima je wanamtaka mwanangu YESU KRISTO au wanataka dini na madhehebu? Mimi
ninayekuambia haya mbinguni nimefika na mbinguni hakuna mahali penye tawi la
dini wala dhehebu, yeye ni MUNGU wa watu wote na ili uweze kufika kwake mlango
ni BWANA YESU peke yake. Mtu asikudanganye eti kwamba ukifa mwaka fulani
tutakukumbuka kwa kukuombea, mimi nakwambia huyo anakupoteza, MUNGU wetu yeye
si MUNGU wa wafu ni MUNGU wa walio hai tu, wakati wako ni sasa wa wewe kumpokea
BWANA YESU na wokovu aliouleta.
Lakini pia uelewe kuwa kuna
wokovu wa dini na madhehebu, ya watu kuokoka tu bila kuupokea wokovu wa kweli wa
BWANA YESU. Ukisoma Neno la MUNGU kutoka
katika kitabu cha 1Timotheo 2:5-6,
Neno linaseama “5kwa
sababu MUNGU ni mmoja, na mpatanishi kati ya MUNGU na wanadamu ni mmoja,
mwanadamu KRISTO YESU; 6ambaye
alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira
yake”.
Sasa uelewe kwamba, YESU yeye ni wa
ukombozi wa watu wote, shida ni madhehebu na dini tu. Ufahamu kwamba kuna
madhehebu ya shetani, ya kabila, ya ukoo na mengine mengi yanayofanana na hayo,
sasa jiulize haya yote yametoka wapi? Mwenye akili na aelewe.
MUNGU yeye anasema ni wa watu
wote na ili akukomboe ni wewe kuokoka, yeye hana muda na watu wanaosema ngoja
kwanza nikufikiriefikirie wewe MUNGU kama nitaokoka ama la! Mtu huyo ni mnafiki
na ni rafiki wa shetani na anampenda shetani ndio maana hataki kuokoka. Kuna baadhi ya makanisa ya wazee sasa hivi wanawaambia
waumini kwamba hakuna kuokoka na kama ukiokoka tutakutenga, mimi nakwambia
watumishi kama hao ni watumishi wa shetani achana nao na uondoke mahali hapo. Jua kwamba dunia hii inapita,
vitu vinapita, tulivikuta na tutaviacha, na watu pia tunapita ni bora umkamate
huyu BWANA YESU maana ukiondoka hapa duniani utaenda kwake, dini wala dhehebu
halitakupeleka popote zaidi ya jehanamu.
Lakini mahali pengine unaweza
ukafikiri unakwenda kwa YESU, lakini unakuta watumishi wanahubiri mambo ya
dunia hii ya kuchukua pesa za wana wa MUNGU eti ndio uombewe, mimi nakwambia
huo sio wokovu aliouleta YESU huo ni wokovu wa mashetani. MUNGU yeye alileta wokovu wa
kweli, anasema hivi katika kitabu chake kitakatifu (Biblia), mtumishi wangu
nimekupa bure toa bure huo ndio wokovu wa mbinguni ninaoujua mimi, mtumishi wa
wokovu wa mbinguni yeye siku zote atakuombea bure na hawezi kuchangisha pesa
kanisani wala kufanya harambee.
Mimi nakwambia mkristo yeyote bila
kuokoka ni kazi bure, watu wengi wanapokea wokovu wa kidunia, wako baadhi ya
wachungaji ni waganga, freemason, ni wachawi wakiwadanganya watu kwa
kuwahubiria wokovu wa kidunia kwa sababu wanajua kwamba watu wengi wanapenda wokovu,
sasa wameamua kuwapoteza kabisa. Kanisa ni mahali ambapo MUNGU anatakiwa
aonekane na awaandae watu wote ili aweze kuvuna watoto wake, kwa sababu mwanae anarudi,
lakini Kanisa kwa sasa, asilimia kubwa limekuwa ni mahali pa biashara na
kufanyia miradi tu.
Mkubali BWANA YESU leo, MUNGU ana
kiu na wewe na anakupenda, amenituma kwako sikiliza haya ninayokwambia usifanye
moyo wako kuwa mgumu, najua watu wengi kwa sasa mmekataa kwenda makanisani kwa
sababu ya michango na harambee za makanisani, mimi nakwambaia ni bora usiende kabisa
huko, mwombe MUNGU akuonyeshe mahali sahihi alipo yeye, maana MUNGU wetu yeye
anasema yeyote atakayenitafuta kwa bidii ataniona. Mimi nakwambia ukimpata
MUNGU wa kweli ni kibali tosha kwa kila kitu kwenye maisha yako ya hapa duniani
na ya mbinguni, we endelea kumtafuta na utamwona.
YESU anarudi ninawaeleza uwe ni
rais, mbunge, tajiri au maskini au ni watoto walio ndani ya matumbo yenu,
wasikie wote kwamba YESU anarudi muda na wakati wowote. Dunia nzima, MUNGU anasema watu
wote, wengi hawamtaki YESU na wala hawautaki wokovu wake, wanalitaja jina lake tu kwa
kuufuata wokovu wa kidunia kwa hiyo kwa wewe kuendelea kumkataa YESU na yeye
anasema kwamba siku atakapo rudi na yeye atakukataa.
Ili uupokee wokovu wa BWANA YESU
ni lazima umkiri kwa kinywa chako mwenyewe.
Sema, BWANA YESU ninaipokea
zawadi ya wokovu wa Jina lako, eeh MUNGU wangu naomba rehema, muda mrefu
sikuipokea zawadi uliyoileta hapa duniani, yamkini hata nilipokea zawadi chafu
ya yesu asiyejulikana, simtaki, nakutaka wewe YESU wa kweli ambaye ni zawadi
niliyopewa na MUNGU ili uniokoe, maana muda wangu ni mchache katika Dunia hii,
najua ya kwamba utakuja kulinyakua kanisa lako na utakapokuja utaangalia
aliyekata tiketi yako na ambaye hana hadithi za wazee na aliyezikataa, nami nazikataa
kabisa, ninajitenga nazo, naomba zisinifuate kabisa zipotelee mbali. Jina langu
liwe kwako BWANA YESU sasa na hata milele, Amen.
NABII HEBRON