YESU
AMESEMA YEYE SIYO MWIZI (MNYANG’ANYI), SASA JIULIZE INAKUWAJE TENA ANAWAIBIA
WATU PESA ZAO KANISANI?
BWANA YESU ASIFIWE! YEYE ALIYE
HAI NA AMBAYE SIYO MNYANG’ANYI. Nimeandika waraka huu ili kuwaelimisha mataifa
yote ya kuwa YESU siyo mnyang’anyi wala siyo mwizi lakini nataka kuelezea
kupitia jina hili. YESU alishasema wengi watatekwa na kudanganywa kwa kutumia Jina
lake na ndivyo ilivyo katika ulimwengu wote, kwa sehemu kubwa wamekuwepo wezi
wa kiroho ambao wanatumia Jina la YESU kuibia watu vitu vyao na mali zao
wakijua ni YESU anavitaka na kuvichukua kumbe ni wanadamu ambao wameanza kuwa wezi
wa kiroho wakitumia jina la YESU.
Ukisoma katika kitabu cha
Yohana 10: 10, 14-15, “10 Mwivi haji ila aibe na
kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. 14
Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua
mimi; 15 kama vile BABA anijuavyo, nami nimjuavyo BABA. Nami nautoa
uhai wangu kwa ajili ya kondoo.”
YESU anakiri yeye siyo mwizi
bali yeye ni mleta uzima, sasa kupitia uzima aliouleta anazo sheria zake, Yeye
anautoa uzima wake bure na amekataza mtu anapoombewa uzima wake asilipie malipo
yeyote yale kwa njia ya kutozwa pesa ili aombewe. Sasa inapokuwa hivyo, mtu
ambaye anatumia jina la YESU kutoza pesa
watu naomba ieleweke wazi huyu mwana wa
MUNGU wa pekee siyo anayekuchaji pesa bali anayekuchaji pesa yeye ndiye mwizi
wa kiroho, YESU asitambulishwe katika wizi huo, sababu hayo siyo yake wala si ya
mwenyezi MUNGU bali ni ya mwanadamu anayejiita mtumishi wa wizi wa kutumia jina
la YESU. Hapo mwanadamu yeye ndiye mwizi, hivyo ni wakati wa kupinga kabisa huu
wizi au ujangili wa kutumia jina la YESU kuwatoza watu gharama ya maombezi wakisingizia
kuwa ni ya YESU. Sasa kwa njia hii YESU anakuwa analaumiwa sana na wanadamu kuwa
amechukua pesa zao, mali zao, wakati hawaoni uponyaji. Nataka muelewe Yeye
alishasema mmepotea kwa sababu ya kutokulijua Neno lake na sheria zake zilivyo.
Sasa nikuulize swali wewe
hauoni katika kitabu cha sheria za MUNGU imeandikwa mtumishi nimekupa bure, toa
bure? Sasa wewe kwa nini unakubali kudaiwa pesa ikaitwa ni sadaka au kwa nini
unapewa risiti katika sadaka na unaandika jina; je, hizi ni sheria za MUNGU wa
mbinguni? Jibu ni hapana; basi hapo uliyafuata mapokeo ya mafundisho ya wanadamu
na kama unayafuata mafundisho ya mapokeo ya wanadamu katika kumtafuta MUNGU wa
kweli, wewe unakuwa ni mfuasi wa wanadamu hata kama unajitia moyo sababu imani
inaendana na matendo. Je, imani yako wewe inafuata sheria za mbinguni au za
wanadamu? Na hata anayeendeleza hayo mapokeo ya wanadamu akikufundisha uyafute,
wewe usikubali sababu katika ufalme wa MUNGU unakuwa hauna nafasi bali unakuwa
unayo nafasi katika mapokeo ya wanadamu.
Ukisoma katika injili ya
Mathayo 21:13 inaelezea vizuri tena utaona YESU akiwa na hasira juu ya wizi na
biashara zinazofanyika katika nyumba za sala. Sasa badala ya nyumba ziwe za
sala ya MUNGU zinakuwa za sala za wanadamu kwa miungu. Na ukisoma Luka 4:12, “12 YESU
akamjibu akamwambia, usimjaribu BWANA MUNGU wako.”
Utaona imeandikwa usimjaribu
MUNGU, sasa angalia katika dunia yote MUNGU anavyojaribiwa na baadhi ya watumishi wakitoza watu pesa, hata wewe unayetoa pesa ili
upate uponyaji na wewe unaunganishwa katika kumjaribu MUNGU. Sasa YESU alitegwa
na shetani ila yeye alikuwa anazijua sheria, akasema imeandikwa usimjairbu
MUNGU na dhambi ya kumjaribu MUNGU au kuvunja sheria zake ni hukumu na moto wa
jehanamu. Natumaini mpaka hapa utakuwa umeelewa ukweli zaidi na moyo wako
kufurahi bali wezi hawafurahi bali watachukia sababu yaliyofanyika katika giza sasa yamewekwa wazi (peupe), haijalishi
na wachukie kabisa, ni bora MUNGU afurahi kuliko shetani kufurahi na mawakala
wake wa kuibia watu pesa wakitumia jina la YESU; kumbuka alikataa mwenyewe
alivyokuwepo hapa ulimwenguni hivyo ni lazima msimame imara.
Waliandika mambo yote yatapita
lakini NENO lake litasimama imara na kusimama imara ni kusema ukweli na siyo
kulichanganya NENO la MUNGU na uongo. Hivyo namtetea YESU yeye siyo
mnyang’anyi, wala siyo mwizi wala hanyang’anyi watu mali zao ili awaponye, yeye
siyo kama hospitali za hapa duniani, alishalipa damu yake pale msalabani, hivyo
kila mtu anayempenda YESU kikweli asikubali kutozwa pesa, nataka uelewe hata
mimi nikitoza watu pesa ili niwaombee tayari nimekuwa ni mwizi au jangili la kiroho
na anayeendelea ajielewe yeye ndiye mwizi kwa jina lake kwa sababu ndani yake
ipo ile roho ya wizi na siyo ROHO MTAKATIFU sababu Roho Mtakatifu angekuwepo
ndani yake angemkataza kuchukua pesa za watu au kupigia watu simu eti MUNGU
kasema tuma pesa haraka kiasi fulani utapatwa na mabaya fanya haraka.
Nawaeleza MUNGU siyo wa matisho
yeye ni wa amani, hao ni wezi. Hivyo basi msimlalamikie YESU bali walalamikieni
hao wezi wanadamu kwa majina yao tena warudishe vitu vya watu katika jina la
YESU.
BWANA YESU AINULIWE JUU SANA.
NABII
HEBRON.