Pages

Wednesday, December 7, 2016

HUU NI MCHEZO WA KAMARI NDANI YA KANISA NA SIYO KUTOA SADAKA!!!


BWANA YESU WA NAZARETI ALIYE HAI ASIFIWE, YESU anawapenda watu wote hata wale wanaomkimbia kwa sababu hawataki ukweli bali wanapenda uongo au giza, yeye ni nuru tu tena isiyozimika, yeye ndiye taa ya mataifa yote kwa atakayeifuata taa hiyo atafika mbinguni, itakuvusha katika giza.

Katika miaka mingi mamilioni ya watu wamekuwa wakicheza kamari katika nyumba za sala wakifikiri wanamtolea MUNGU sadaka, ukisoma katika kitabu cha Marko 11: 15-18 inaelezea vizuri na zaidi uelewe sadaka ni siri yako wewe na MUNGU, haitakiwi ijulikane. Sasa watu wanampenda MUNGU sana na wanapenda kumpa asante zao, ila baadhi inakuwa siyo sadaka bali ni “kamari” au “mchezo wa kamari”. Kamari hizi ni michango, kutoa sadaka na kuandika majina na kupewa risiti au kupewa vyeti vya hongera umekuwa mtoaji mzuri (huu ni ufisadi kabisa na ikifikia mpaka kuhani kutoa vyeti vya watoaji bora wa sadaka uelewe amefikia kiwango cha kishetani au fisadi). Hayo ni mambo ya shetani siyo ya MUNGU kabisa, utafilisika hapo.

Kamari nyingine ni harambee makanisani. Kama mtu anataka kumtolea MUNGU atoe siyo kwa kujionyesha mfano natoa kiasi fulani halafu anapigiwa makofi; hiyo siyo sadaka hiyo ni kamari. MUNGU hapokei kamari wala hachezi kamari na ukicheza kamari ni dhambi. Asili ya kamari ni kuzimu (unyang’anyi). Mfano, wewe kiongozi ukiombwa usimamie harambee kanisani au michango, na wewe unaonekana mbele za MUNGU ni kiongozi wa kusimamia unyang’anyi au kamari. Kama kazi ni ya MUNGU yeye atafanya njia ajuavyo yeye sababu yeye ni tajiri na siyo maskini.

Na zaidi wapo baadhi ya watumishi sehemu mbali mbali ambao wapo kipesa (kimaslahi) na kipepo, mtashangaa waumini wanaambiwa kila mtu aandike kiasi chake cha mshahara au kiasi cha kipato chake na taarifa zao zinawekwa kanisani. Huu siyo mpango wa YESU, unachokipata ni haki yako ni MUNGU anayekupa ndiye ajuaye kipato chako. Taarifa zako zikijulikana basi unashikiliwa ufahamu wako kipepo na matokeo yake unanyang’anywa katika ulimwengu wa roho, unakuwa unazitoa zote na unasahau maendeleo yako, familia na mengineyo, na unaanza kusikia misemo “huyo anafilisikia kanisani.”

Jiulize, imeandikwa ukitoa utapokea, sasa kwa nini haupokei? Natumaini jibu mmelipata, ulicheza kamari. Wengine wanashiriki kutoa katika kikapu cha mama mchungaji, hiyo siyo sadaka, hiyo ni kamari ( ni wizi).

Angalizo:
Hivi umeshajiuliza siku zote, je tajiri au mfalme hua anaenda kuomba msaada kwa masikini? Jibu ni dhahiri kwamba tajiri au mfalme wao ndio hupeleka misaada kwa masikini, hivyo MUNGU yeye siyo masikini, vitu vyote ni vyake. Akitaka jambo lake lifanyike anafanya njia na njia zake siyo za kamari.  Utasikia fulani simama umsaidie MUNGU, hiyo siyo sadaka na wala haitabarikiwa, na kazi zitakazofanyiwa hizo pesa hazitakuwa na baraka za MUNGU. Yeye siyo omba omba. MUNGU ainuliwe juu milele.

NABII HEBRON.