Pages

Thursday, March 17, 2016

JINSI MBINGUNI PALIVYO


Halleluyah!

Karibu tena katika kipindi hiki, lakini ngoja kwanza nikuombee; BABA katika jina la YESU ninawakomboa watoto wako, nawafungua fahamu zao, ninavunja kila aina ya upinzani katika jina la YESU, wakuelewe MUNGU katika habari njema wanayokwenda kuipata kuhusu mbinguni palivyo, nami na kwenda kusema na mataifa yote maana wengine wanajua hamna mbingu ulinionyesha, ulinipeleka na sasa nafanya kazi yako, na sasa nakwenda kuwafundisha watoto wako, kile ambacho unataka kwa utukufu wako, Amen.

BWANA YESU asifiwe, karibuni tena siku ya leo, nakwenda kueleza habari za jinsi mbinguni palivyo, ninajua kuna wengine wanajua hamna mbingu,  lakini mbinguni pako, nitakuelezea kwa ufupi sawa na MUNGU atakavyo niruhusu , amenipeleka mimi huko, nijue alipo yeye na siku moja, nitafika kimwili kabisa, na wewe ufike huko. Akaniambia Hebron, uwaongoze watoto wangu mpaka wafike hapa, BABA yako YESU alitoka hapa, alikwenda duniani amerudi hapa na wewe nimekuleta upaone.

BWANA YESU asifiwe, kwanza kabisa nataka kuwaeleza MUNGU yupo. Wanaosema MUNGU hayupo watubu, sio wao ni roho ya shetani inayokaa ndani yao kuwaambia kuwa MUNGU hayupo ili wapate dhambi ili wahukumiwe na wabaki hapa hapa, na siku moja wasiende mbinguni, kwa sababu wameshakataa kwa kinywa chao, kwamba hamna MUNGU, aidha kwa kujua au kutokujua.

Haleluya! Nilipopelekwa mbinguni nikiwa hapa hapa duniani, nilikaa kwa muda wa miaka mitatu, mwaka mmoja ulikuwa ni wa MUNGU, mwaka wa pili ulikuwa ni wa BWANA YESU, mwaka wa tatu ulikuwa ni wa Roho Mtakatifu. Miaka yote nilikuwa nikifundishwa lakini nikiwa hapa duniani lakini watu hawakuelewa sikuwepo bali ni mwili tu ndio ulikuwepo duniani. Nilipomaliza ndio wakanirudisha, sasa nimeanza kazi yake, na mimi nakueleza habari za mbinguni maana amenifundisha yeye.

Kwanza kabisa nataka niwaeleze katika dunia hii tunaambiwa kuna sayari kubwa inaitwa Jupita, kubwa kuliko sayari zote, sasa mimi nataka kuwaambia hivi, sayari zote zikikusanywa ukubwa wake na nyingine hazijulikani bado hazifikii robo ya ukubwa wa mbinguni, mbinguni ni pakubwa sana, mbinguni ni pazuri sana, kama hizi sayari zote zikichanganywa bado hazifikii robo ya mbinguni.

Tazama hii dunia ilivyo kwanza ukubwa wake watu wanazunguka lakini watu hawamalizi, sasa zidisha ukubwa wote huo mara tisa (9) bado hazifikii ukubwa wa robo ya mbinguni, ni pakubwa sana, mbinguni kuna bahari, kuna maziwa (there are rivers), kuna samaki, kuna wanyama (simba, pundamilia, n.k) kama hapa duniani palivyo, na mbinguni ndivyo palivyo. Kuna bustani nzuri sana, kuna milima mizuri sana, kuna maofisi mazuri sana, hata nilienda kwenye ofisi ya BWANA YESU, na ofisi yake ni moja ya ikulu, MUNGU na yeye ana ikulu yake mwenyewe. Hapa duniani tulikuwa tunajua kwamba YESU labda anakaa hivi, labda anashikwa mkononi, ni kweli yupo karibu na MUNGU sana, lakini siyo kwamba amekaa mkononi mwake MUNGU na yupo hapo karibu.

Nilishangaa sana kuna ndege za kuruka angani, kuna magari mazuri sana, hakuna giza, hakuna usiku, kuna vinywaji vizuri sana, kuna hekalu zuri sana, ambalo ni la MUNGU peke yake, malaika na serikali ya mbinguni wote wanaabudu hapo. Na wanamtolea MUNGU sadaka vile vile, lakini leo nitaeleza kidogo.

Haleluya! Bwana YESU asifiwe, na viwanja vya kule mbinguni, kwa hapa duniani inaitwa ploti, kwa mbinguni ploti ya mtu ya kujenga nyumba, kwa mfano wa huku duniani ni sawa na kama heka 2000 au 1000, hiyo ni  nyumba ya mtu mmoja wale wanaoishi mbinguni ndivyo nilivyoona. Kuna siku moja, nakumbuka tulikuwa kwenye nyumba ya Musa, yule ambaye aliwavusha wana wa Israel. Nyumba yake ilikuwa ni kubwa sana tulikunywa chai, tulikula pale, tuliongea, alinifundisha kama mgeni, akaniambia sisi tumepita na wewe hakikisha unafika. Lakini nilifungwa mdomo muda mrefu nisiyaseme haya.

Siku chache zilizopita ndipo nikasikia eleza habari hizi halafu nikakumbushwa, maana MUNGU kama MUNGU akikuonyesha kitu chake kama sio wakati wake huwezi kukisema, mpaka atoe kibali yeye.

Haleluya! Mbinguni kuna malaika wengi sana. Umekwisha kusoma katika Biblia wameandika kwamba, malaika wengi kama mchanga wa baharini, ina maana wako wengi sana, kama nilipokwisha kukuambia ya kuwa sayari zote tisa (9) zikiunganishwa hazifikii robo ya ukubwa wa mbinguni, sasa nikuulize wewe unafikiri ni wangapi watakaa huko, malaika ni wangapi?

Haleluya! Lakini usiogope! Pia kuna mji wa malaika Mikaeli maana yeye ndiyo mkubwa wa vita dunia nzima, ni malaika mkuu wa MUNGU na pia anayesimamia vita vya wana wa MUNGU hapa duniani wanaokwenda mbinguni.

Bwana YESU asifiwe, na katika wakati nilipokuwa mbinguni kuna sayari ambayo haijajulikana hapa duniani na haitajulikana, na hiyo sayari kuna watu wanaishi na malaika. Bwana YESU asifiwe, unajua kuna vitu vingine mwanadamu anafuatilia, lakini MUNGU hawezi kufuatiliwa mpaka MUNGU aamue mwenyewe, lakini hiyo haitakaa ijulikane, haleluya!

Bwana YESU asifiwe, mbinguni ni pazuri sana, kuna barabara nzuri sana na barabara za kule ni za madini, na ni kubwa, upana wake ni kama kilometa tano, hiyo ni barabara moja tu. Magari ni makubwa. Bwana YESU asifiwe, kuna viwanda vya magari, kuna viwanda vya silaha, kuna viwanda vya nguo. Kule mbinguni wanavaa mavazi mazuri sana, mimi kwa akili yangu hapa duniani kabla ya kumjua MUNGU nilikua najua wanavaa mashuka kama zile nguo za kiyahudi, kumbe wanavaa mavazi mazuri sana, na viatu vingine ni vya dhahabu tu, na mavazi mengine ni ya madini ya gharama kubwa sana yanayojulikana hapa duniani. MUNGU ni tajiri sana. Na ni BABA yako anakuhitaji.

Pia kuna chuo cha kufundisha watumishi wa MUNGU, ambapo Roho Mtakatifu ndio msimamizi wake, Roho Mtakatifu siyo njiwa kama mnavyoambiwa, ni mtu kama vile YESU alivyoonekana hapa duniani, na ile siku ya mwisho utamwona, haleluya! Roho Mtakatifu ndiye anayeongozo injili ya kweli. Bwana YESU asifiwe, kuna mashamba, haleluya! Umeshajiuliza wanakula nini? Wana kila kitu,  niliona mpaka meli za uvuvi katika bahari. Haleluya! Wako malaika wa kitengo cha uvuvi.

Haleluya, katika chuo nilicho kiona mbinguni, ambacho mimi pia nilisoma pale, waalimu wake ni wale Wazee 24, Bwana YESU mwenyewe na Roho Mtakatifu na mara nyingine pia MUNGU alikuwa ananifundisha. Nilichokishangaa sana, yale niliyofundishwa kule Mbinguni nilipokuja hapa duniani ni tofauti na ambayo naona watumishi wengi wanayafundisha. Unajua ni kwa nini YESU alichukiwa na mafarisayo? Alifundishwa na BABA yake mbinguni, na alikifanya kile alichofundishwa mbinguni. Sasa hapa duniani, nimeshangaa watu wanachangisha pesa. Nimeshangaa watu wanabatiza watu kwa ubatizo wa kikombe, kwa majina ya wachungaji, kwa vumbi, kwa kutumia maji ya tenki na mengine mabaya kabisa.

Hao wafanyao hayo hawajafundishwa na MUNGU, hiyo ni elimu ya shetani, nilishangaa sana na niliogopa, MUNGU aliniambia Hebron nimekuita  nikufundishe ndio maana mwaka 2009, nilipokuita ukiwa Serengeti nilikuambia usiende chuo chochote, maana uliniuliza sana nitafanyaje kazi yako, mimi nilikuangalia tu, lakini nilijua nitakachokifanya, nimekufundisha, umemaliza, umefika kiwango nilichotaka, sasa angalia dunia  ilivyopotea. Nakutuma sasa.

Amenituma na ndiyo maana nawaeleza ukweli MUNGU anawahitaji watoto wake, anahitaji uende mbinguni ,mafundisho ya uongo hayakupeleki mbinguni, usijitie moyo kwamba utakwenda mbinguni wakati unafundishwa uongo, mbinguni kuna wokovu, mbinguni wameokoka, sijawahi kuona mtu ana hasira kule, ni upendo tu, sijawahi kuona mambo ya hapa duniani, hakuna magonjwa, hakuna shida, ni furaha tu waliooko mbinguni wana miji yao, wana maisha mazuri, lakini maisha yao kule mbinguni kila mmoja ana madaraka yake. Tuchukulie mfano wa mfumo wa uongozi hapa duniani katika nchi nyingi, labda tuseme Rais au Mfalme ndio Bwana YESU, Waziri Mkuu ni Roho Mtakatifu. Bwana YESU asifiwe, wako wale wenye madaraka kama mawaziri, wapo wengine ni mameneja, wapo wasimamizi (supervisors) na watendaji kazi mbali mbali, ndio maana unaambiwa, mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA, si utapiga makofi tu halleluya pamoja na kumwabudu.

Bwana YESU asifiwe, kuna maaskari mbinguni, kuna silaha mbinguni, kuna mabomu ya kila aina ambayo hapa duniani hakuna, kuna ulinzi ambao haupo hapa duniani, na MUNGU anazungukwa kule mbinguni analindwa, kumsogelea MUNGU aah si kitu rahisi, wapo watu wa chini yake, hata kumsogelea YESU ni vigumu kama kumsogelea Rais, hata Rais inaweza kuwa rahisi kumuona ukilinganisha na kumsogelea YESU. Wanadamu mmepewa neema ya kumpokea yeye tu na anakuja mara moja, lakini unakataa, unasema bado wakati wake, kwa kufanya hivyo wewe unakua ni mtu wa shetani, badilika.

Bwana YESU asifiwe, na kule mbinguni, YESU huwa anapanda ndege hata malaika wote wana ndege zao, YESU akitoka labda anaenda mji mwingine kutembea anakuwa na msafara mkubwa zaidi ya ndege 2000 zikiwa zinamtangulia na kumlinda na mahali popote anapokwenda lazima anakuwa yuko na malaika Mikaeli  na anakuwa na msafara mkubwa sana. Bwana YESU asifiwe, na kuna viwanja vya ndege vizuri sana, sasa nikuulize hapa duniani mtu gani anasafiri anasindikizwa na ndege 2000 na wakati mwingine zinazidi. Hapa duniani tunaona ndege kubwa lakini mbinguni hizo ndege tunazoona ni kubwa hapa duniani, mbinguni vile ni vidogo kabisa yaani hizo ndege ni ndogo sana ni kama, hizi za watu wawili au watatu, Halleluyah.

Na wewe ukienda mbinguni ziko ndege zinakusubiri. Mbinguni nyumba za watu ni kama nyumba ya Eliya, nyumbani kwake niliona kuna viwanja vya ndege na siyo ndege moja, kwenda ofisini kuna uwanja wa ndege ni tofauti na hapa.

Haleluya, Bwana YESU asifiwe, na MUNGU huwa anawalipa mishahara, ndio maana nao wanatoa sadaka, wewe ulifikiri wanatoa nini? Bwana YESU asifiwe, ipo benki kule mbinguni, hayo nitaeleza wakati mwingine, MUNGU ana pesa, lakini nashangaa hapa duniani watu wengine wanaambiwa wakatae pesa. Nikuulize swali, yule samaki aliyemtemea pesa Bwana YESU kwenye ziwa, ile pesa iliitoa wapi? Yule samaki alitoka mbinguni, kama nilivyowaambia mbinguni kuna samaki, pia, akaja kwenye ziwa pale akamlipia Bwana YESU, na wewe bwana YESU atakulipia.

Kama nilivyokwisha kuwaambia, mbinguni kuna wanyama, umeshawahi kujiuliza kipindi kile Musa alivyokuwa jangwani wana wa Israel walidondoshewa mikate na kunguru, wale kunguru walitoka wapi, walitoka Mbinguni, wakagawa mikate, wakashushiwa chini walipomaliza walirudi mbinguni, hii inakuthibitishia kuwa mbinguni kuna wanyama. Kuna wakati mwingine wana wa Israeli walishushiwa kware wakiwa jangwani, wakala. Unafikiri kware walitoka wapi, jibu walitoka mbinguni. Mbinguni ni pazuri sana, pazuri sana. Haleluya! Kuna sehemu ya muziki, nyimbo za kumsifu MUNGU na vile vile mbinguni watu wanaenda baharini kutembea, wanaogelea lakini bahari ya mbinguni haijachafuka, hizi hapa zina wachawi zimechafuka, zinavinyesi. Bwana YESU asifiwe, na makafara  na vitu vingi vya ajabu.

Haleluya, Bwana YESU asifiwe kama nilivyokwisha kuwaambia hapa duniani, watu wanatoka nchi moja kwenda nchi nyingine kuangalia wanyama na vivutio vingine. Haleluya! Na mbinguni ni hivyo hivyo kuna sehemu kuna wanyama maeneo fulani, lakini haiwezi kuelezeka. Ndio maana shetani amechukia kwa kufukuzwa huko kwa maana ni pazuri, anakuonea wivu na wewe anakuzuia usiokoke. Akachafua ukristo, akawateka watumishi ambao wamemkubali yeye ili kuendeleza mabaya ili wewe usiende mbinguni.

Bwana YESU asifiwe, leo nakuomba utubu. Mbinguni wana simu nzuri sana, wana miziki mizuri sana, wana camera nzuri sana, wana vitanda vizuri sana, mimi nilifikiri wana lala chini. Kama MUNGU yeye ndiye ameumba vitu vyote hapa duniani na bado havifikii robo ya ukubwa wa mbingu, Je Yeye anaishi mahali gani?

Haleluya! Jambo jingine, tulifundishwa katika physics na chemistry, maji yanaganda angani alafu yananyesha, ninachoowambia, ndiyo hiyo tumefundishwa kuna ukweli wake. Lakini kuna mara nyingine bahari ya mbinguni inafunguliwa maji kunyeshea dunia. Pale MUNGU anapotaka kuadhibu wanadamu, kuna maji yanayofunguliwa kutoka mbinguni kama nilivyokwisha kuwaeleza, tokea Desemba 2015, MUNGU ameanza ishara za kujulisha mwanae anarudi. Niliwaambia kuna mvua za ajabu zitanyesha, zinatoka mbinguni, umeshawahi kujiuliza, radi inatoka wapi nilishangaa sana wakati nikifundishwa mbinguni. Mbinguni kuna umeme, wakati mvua inanyeesha kuna malaika wa kitengo cha mvua kunyesha dunia wanatumia nguvu ya umeme ya kiungu kuamuru ile mvue iende mahali fulani ambayo ni nguvu haielezeki, ndio maana wakati mwingine unasikia inaunguruma.

Bwana YESU asifiwe, MUNGU ana nguvu sana, usishangae  sana ukaona kuna mafuriko ya ajabu, ni kweli inaonekana mvua inanyesha hapa lakini kuna maji mengi yanatoka mbinguni kunyeshea, na MUNGU akitaka kuwaadhibu wanadamu hutumia njia hiyo, maana kuna upepo mbinguni, ule upepo umaamuliwa kuja kupiga duniani, kwahiyo MUNGU anasema kuwa atafanya maajabu na kuipindua pindua dunia mwishoni, kule mbinguni niliona aina mbalimbali (stock) za mapigo, Bwana YESU asifiwe, na  kama nilivyokwisha kusema ardhi itakuwa inagawanyika, yeye anajua msingi wa dunia ulivyoo anajua mwanzo wake na mwisho wake, na siku moja wakati ananifundisha, nilikuwa naongea na MUNGU alisema Hebron wanadamu wananiudhi sana, mimi sioni hasara hata nikiangamiza dunia nzima, naweza nikaangamiza na kutengeneza  nyingine na nikaumba watu wengine, niliogopa sana akaniambia kipindi cha Nuhu niliua yote na sasa hivi wamejaa tena, ninakueleza wewe Hebron sitafanya hivyo lakini maana nilishtuka aliniambia wewe ni rafiki yangu tuongee hata manabii wa zamani, nilipotaka kuwapiga waliomba, nami nakusikiliza kwa sababu mtoto mzuri baba yake humsikiliza yakaishia hapo, akaniambia waeleze habari zangu, waambie ila wengine watakupinga, usiogope utashinda tu, wale walio wa kwangu watakuja na nitatenda, kwa siku ya leo niishie hapo nitaendelea wakati mwingine tena, ninasikia sauti kutoka mbinguni “today that is enough” na yanakatika na yanafutwa kwenye macho yangu. Halleluyah!

Sema, Bwana YESU, naomba unisamehe dhambi zangu zote, nilizozifanya kwa kujua au kutokujua, naomba  Bwana YESU na mimi unipokee, na siku moja nifike mbinguni, ninafurahi kujua habari za mbinguni nakushukuru.

NABII HEBRON.