Umewahi
kujiuliza ndugu msomaji wa makala hii kwa nini wajane wanahangaika mahakamani
na kwenye mabaraza ya wazee wa ukoo kwa maswala ya haki zao? Na pengine
hawazipati? Ni kwa sababu viongozi wa kanisa (watumishi wa pesa au matumbo);
wenyewe wamekuwa wanyang’anyi wakubwa wa kudai pesa na kuchangisha pesa
makanisani ndiyo maana hiyo roho ya kupenda pesa na vitu imeenea hata kwenye
jamii na watu kukosa muelekeo, ndiyo kutumbukia kwenye roho hiyo hiyo ya
kunyang’anya na kudhulumu wajane wa MUNGU.
Tukiangalia
tangu enzi za wazee wetu wakina Ibrahimu mpaka Musa na Sulemani waliamua
maswala ya wajane kwa haki kabisa, lakini sasa hivi viongozi wa kanisa
wamesahau kuwa BWANA YESU mwenyewe ni MUME wa wajane, na kimbilio la wajane ni
kwenye kanisa. Lakini sasa hivi sivyo ilivyo. Viongozi wa kanisa wametekwa na
roho ya kupenda pesa na vitu. Jambo hili wanalifungia macho na kusahau wajibu
wao kama kanisa na kwenda kinyume na neno.
Hebu
tuone neno linasemaje kwanza kabisa. Kitabu cha Mwanzo 1: 26-29; MUNGU aliumba
mwanaume na mwanamke akawabarikia Baraka za kiroho na kimwili, akawaagiza
wakazae na kuongezeka na kumiliki vitu vyote (wote) wamiliki. Maana ya kutawala
na kumiliki ni kuvitiisha pamoja na vile wanavyovizaa na kuongezeka. MUNGU
hakuagiza kwa mwanamume tu ameagiza kwa mwanamume na mwanamke wote! Kisha
akawapa wote kila kitu, hapa maana yake mwanamume na mwanawake wanapounganishwa
kwa ndoa takatifu wanakua mwili mmoja na MUNGU anaachilia hivi vyote juu yao na
kila wanapozaa na kuongezeka MUNGU anazidi kubariki zaidi kwa Baraka za mwilini
na rohoni.
Kama
ndivyo basi inakuwaje anapotangulia mwanamume kufa, wanadamu wanasema hizo Baraka
ni za mwanamume kwa hiyo mwanamke aliyebaki hana haki? Ni mwanadamu anasema
hivyo. Je? Kanisa nalo linasema hivyo? Jibu ni ndiyo. Hawa ni viongozi na
watumishi vipofu, wamesahau wajibu wao, wamerudi duniani badala ya kuwaongoza
hata hao wasioelewa na kuwatoa kwenye anguko la jehanamu.
Yeyote
anayemuonea au kumdhulumu mjane jehanamu inamhusu. Hana njia ya uzima ndani
yake, wa kwanza kabisa ni hao viongozi vipofu, wasaliti wa BWANA YESU. Mimi
nawaita wasaliti! Kivipi NENO linasema katika kitabu cha Kumbukumbu La Torati
10:18 “Huwafanyia yatima na mjane hukumu ya haki, naye humpenda mgeni, akimpa
chakula na mavazi.”
Kama
ndivyo basi inakuaje wachungaji wamekuwa wa kwanza kunyang’anya pesa na mali ya
wajane kichawi kuwafanya ATM mashine zao, bila huruma.
Wanazini
na wajane na kuwapotosha kabisa badala ya kuziponya roho zao wanazielekeza
kwenye moto kabisa. Wajane wakimbilie wapi? kila mahali panawaka moto wa uovu
ndani ya kanisa hakufai, kwa jamii ndiyo balaa. Yuko wapi mtetezi wao? Yupo
YESU WA NAZARETI ALIYE HAI. Lakini aonekane wapi?! Aliyewaachia kutetea
wamemsaliti. YESU ni mwamuzi wa yatima na mtetezi wa wajane Zaburi 68:5.
Kama
wachungaji wa kondoo wanafanya dhuluma kwa wajane unadhani jamii itafanyaje?
Jibu, itafanya hivyo hivyo kuwanyanyasa na kuwagandamiza wajane kosa ni la
nani? Kosa ni la wachungaji na viongozi wa kanisa siyo la jamii maana kanisa
linatakiwa kuonyesha mfano mzuri kwa jamii lakini siyo hivyo, na shetani
amepewa nafasi kubwa ndani ya kanisa akaweka makao.
Ndugu
msomaji uliyetangulia kusoma makala za Mtume na Nabii Hebron umejua kuwa kanisa
limetekwa 98% ndiyo maana hakuna haki ndani ya jamii. Itoke wapi ikiwa hakuna
haki ndani ya kanisa? Kivipi?! Kwa ukweli huu:
Viongozi
wa kanisa wanashiriki sherehe za mila na matambiko na kufanya (misa) za wafuu,
kubariki mbesi, sendoff, matanga na mengine mengi yanayofanana na hayo. Hii
yote ni ibada ya sanamu na katika kufanya hayo yote ni kumtukuza shetani na
kuzidi kuwapiga upofu hata wasijue kuwa MUNGU aliye hai ndiye MUME wa wajane.
Lakini shetani anajua hayo toka mwanzo kuwa MUNGU ndiye mtetezi wa wajane
akaliteka kanisa na kulipiga upofu.
ANGUKO
Mwanzo
3: 1-19; uharibifu ulitokea hapa mahali ambapo Adam na Eva walimuasi MUNGU,
shetani akakamata ndoa toka mwanzo mpaka mwisho utaona kwamba hata baada ya
mwanamume kufariki kikao cha kwanza kabisa cha kufanya maamuzi ya maisha ya
mjane inaanza kwa usimamizi wa wazee wa ukoo, badala ya viongozi wa kanisa,
wachungaji. Kama ndoa hiyo ilifungwa kanisani, umejiuliza kwa nini maamuzi ya
ndoa hiyo iliyofungwa ndani ya kanisa linaloitwa kanisa la YESU, maamuzi na
mashauri yafanyike ndani ya ukoo? Jibu ni kwamba toka mwanzo watu hao wawili
walianzia kwa wazee kabla ya kupelekwa madhabahuni.
Inavyokuwa
ni hivi; kijana akimpata binti anampeleka kwao na wazee humpokea kwa sherehe za
kimila. Je nikuulize ndugu msomaji, hapo aliyepewa kipao mbele ni nani? Kama
siyo shetani (mizimu) na siku ile ya kikao baada ya mazishi unadhani ni nani
atakayetawala hicho kikao? Jibu, ni shetani, ndiyo maana kunakuwa na mvutano
mkubwa sana baina ya ukoo na mjane. Kwa hiyo ndugu msomaji wa makala hii
ninavyo kwambia kwamba kanisa limeacha kutetea wajane ni viongozi na wachungaji
wametekwa na shetani 98% hata hawajui wajibu wao kwa kuwa wamemsaliti YESU na
YESU amewaacha wabaki na upumbavu wao.
UKWELI
Ukweli
ni kwamba mwanzilishi wa ndoa ni MUNGU mwenyewe, na ikitokea mmoja wa wanandoa
hawa ametangulia kufa anayebaki pamoja na familia hiyo wakabidhiwe ndani ya
uongozi wa kanisa ili kuzungumzia swala hilo, kwa kuwa neno linasema, YESU
KRISTO WA NAZARETI ndiyo mwamuzi wa yatima na wajane. Na mtumishi ambaye
anatumiwa na YESU wa kweli, hufuata taratibu na uongozi wa neno la MUNGU na
kuangalia hizo roho zisipotee bali zipone. Je? Nikuulize ndivyo inavyofanyika
ndani ya kanisa? Jibu ni hapana.
Kitu
cha kwanza kabisa viongozi wa kanisa huwashauri wafiwa; mjane na watoto ni
kuwakazania kufanya ibada ya wafu, misa ya kumbukumbu. Je? Nikuulize ndugu
msomaji, mtu aliyekufa kumbukumbu lake halijasahaulika? Jibu, limesahaulika
Soma Mhubiri 9: 3-5; hana ijara maana yake ni asikumbukwe kabisa siyo
wakuzungumziwa tena wala kutajwa haisaidii lolote.
Kinachotakiwa
ni kuwashikilia waliohai roho zao zisipotee kwa kuwaongoza vizuri wavuke
washinde, wasonge mbele kuangalia mahali YESU aliyefufuka alipo siyo mahali
wafu walipo. Shtuka mwana wa MUNGU unazidi kuunganishwa na huo ufalme katika
kila hatua ya maisha yako ili usione NURU. Hii ni janja ya shetani na himaya
yake kubwa sana kwa sasa ni kanisa!
Kwa
wewe mjane na yatima, tafuta kanisa ambalo YESU wa kweli yupo akutetee.
UBARIKIWE
SANA. AMEN.
MCHUNGAJI
DORCAS SAMUEL MDEE.