YESU
ALIMAANISHA NINI KWA KUSEMA, MBWA MWITU MJIEPUSHE NAO
BWANA YESU ASIFIWE. Katika Neno
hili alilolisema YESU, “mjiepushe na
mbwa mwitu”, MATHAYO 7:15. YESU hakumaanisha ni wale wanyama
wa porini ambao wanaitwa “wild dogs”
bali alimaanisha ni kiroho baada ya yeye kuondoka. Nitaelezea kwa ufupi kuhusu
tabia za huyu mnyama kwa sababu nimepata bahati ya kusoma elimu ya wildlife na nimewaona kwa macho na kujua
tabia zao vizuri. Huyu ni mbwa wa tofauti ni mkali kupita mbwa wanaotunzwa na
wanadamu, wanaitwa mbwa mwitu kwa sababu
wanadamu hawawezi kuwafuga. Nitaelezea kwa kifupi, wakiwa wanawinda mnyama hawa
mbwa mwitu humkimbiza mnyama wakiwa katika kundi (in group)
na kila mbwa mwitu hung’ata sehemu ya mnyama wanayemkimbiza na muda wote mbwa
mwitu hao wakiwa bado wanakimbia huendelea hivyo hivyo kung’ata na kula mpaka
pale mnyama anapoanguka chini. Mnyama huyo anapoanguka hubakia na sehemu kidogo
ya mwili wake au kwa maana nyingine hawa mbwa mwitu humla mnyama pasipo kumuua
kwanza, bali wakiwa katika kundi humla mnyama huyo akiwa bado mzima mpaka pale
atakapoishiwa nguvu na kuanguka chini na kufa, ni mbwa wakatili sana na kwa
kingereza wanaitwa wild dogs.
Sasa kwa nini YESU alisema angalieni
mbwa mwitu watakuja na kwa nini wasiwe hawa mbwa mwitu wa porini wakaja
makanisani? Badala yake hawa mbwa mwitu
wakawa ni watumishi wa kiroho katika
injili, na kama ni mbwa mwitu wako katika injili basi uelewe wanawinda wana wa
MUNGU wanaomtafuta au kumpenda YESU ili wauwawe kiroho na hata kutimia kimwili.
Neno hili nafikiri ni watu wengi hawalijui maana yake na inawezekana hata
unayesoma ujumbe huu pasipokujua au kwa kujua tayari umekuwa mbwa mwitu na siyo
mchungaji na kama ni mbwa mwitu basi siyo mchungaji aliyeitwa na Mungu bali ni
mchungaji jina tu. Ndio sababu YESU akasema kwa nje wamevaa ngozi ya kondoo ila
ndani yao ni mbwa mwitu, maana yake kwa nje anaitwa au kuonekana ni mchungaji
ila anayoyatenda na yaliyojaa ndani yake ni mbwa mwitu. Sasa kama unayotenda mambo
ya tabia za mbwa mwitu, hapo inakuhusu kuitwa na YESU wewe ni mbwa mwitu wa
kiroho. Ninaposema mbwa mwitu wa kiroho nina maana ni wale baadhi ya wachungaji
au watumishi ambao kwa nje au kwa majina wanaonekana au kuitwa ni watumishi wa
MUNGU ila ndani ya mioyo yao wana mipango tofauti na Roho Mtakatifu, haijalishi
jina la YESU linatajwa au Biblia kusomwa. Kumbuka YESU alisema watatumia jina
langu kuwateka hata wateule, yaani wale waliookoka, na ambao bado hawajaokoka
na ambao wapo njiani kumpokea YESU wakazuiliwa kutokuokoka.
Kazi ya mbwa mwitu katika
kanisa ni kuua kiroho au kuyaharibu yale ambayo YESU aliyaacha yafuatwe ili watu
waweze kuurithi uzima wa milele na kwenda mbinguni. Shetani akaingiza roho
mbaya ndani ya baadhi ya wachungaji waliomsaliti YESU na wale wengine
waliojiita na wengine wale ambao wamezaliwa kiroho na shetani japo ni wanadamu,
hivyo ile roho ya shetani ndiyo itendayo kazi, roho ya mbwa mwitu, roho ya kuua
roho za wanadamu, roho ya kula pesa za waumini kwa kuwadai pesa za maombezi
wakati neno linasema nimekupa bure, toa bure. Endapo mtumishi ataanza kuwatoza
watu pesa, tayari yeye anaitwa ni mbwa
mwitu na siyo mchungaji kwa sababu hili analolifanya siyo mapenzi ya MUNGU
aliye Mbinguni, bali ni mapenzi ya baba yao ambaye ni joka kuu aliye kuzimu. Haijalishi
anajua au hajui. MUNGU analiangalia Neno lake. Swali, je kutoza watu pesa ni la
Mbinguni? Jibu siyo la Mbinguni, hivyo basi mchungaji anapofanya hivyo tayari
yeye anaitwa mbwa mwitu na hata hao
anao waongoza kiroho hawawezi kuwa kondoo wa YESU, bali watakuwa na wao ni
watoto wa mbwa mwitu. Biblia inasema, jinsi alivyo mchungaji ndiyo taswira ya
waumini wake, hivyo usipende kuwa mtoto wa mbwa mwitu wakati wewe unapenda kuwa
kondoo wa YESU.
Nitaelezea kwa ufupi na
ulimwengu wote uelewe hata na wayahudi kwa sababu baadhi mnapenda kwenda
mbinguni, lakini tambua ya kwamba mbwa mwitu hakufikishi mbinguni bali
anakuamgamiza kiroho na kukunyang’anya mali zako kwa kutumia jina la YESU au
hata kukubatiza ubatizo ambao ni tofauti, ubatizo usiojulikana ulipotoka na
kumfanya mtu apokee ubatizo wa uongo na kwa njia hiyo hupokea kibali cha
kutengwa na YESU pasipo kujua. Ndiyo sababu YESU akasema ubatizwe ili uwe mwanafunzi
wake. Sasa jiulize umeupokea ubatizo alioupokea YESU, ambaye yeye ndie njia? Basi
endapo umepokea tofauti na ubatizo alioupokea YESU, yakupasa kujua kwamba katika
ulimwengu wa roho upo katika njia ambayo siyo Yake, unatembea katika njia
ambayo siyo yake, unatembea katika njia ya mpinga kristo, japo haupendi au
unajua. YESU amenituma niwaeleze ili mbadilike, hiki ni kipindi cha neema, yeye
anarudi na atawachukua wale wenye kibali chake au kiapo cha ubatizo wake.
NI
JINSI GANI MCHUNGAJI ANAWEZA AKAGEUKA AKAWA MBWA MWITU
1.
Akianza kuwadai watu pesa za maombezi.
2.
Akibatiza tofauti na ubatizo aliobatizwa YESU wa
maji mengi yanayotembea na yasiwe hata ni ya kisima au ubatizo wa maji ya
kikombe au hata wa maji mengi yanayotembea halafu ukabatizwa kwa jina la
mchungaji; mchungaji huyo mbele za YESU na mbingu anakuwa ni mbwa mwitu, iwe
anajua au hajui kuwa hayo ni makosa, na anakuwa ameivunja amri ya MUNGU au
kuipindua, soma Ufunuo 22: 18-19.
3.
Anapofanya maombezi ya kupanga kiwango fulani
cha kutoa au hata kupanga viti maalum katika ibada au mtumishi anayetangaza
kwamba atawawekea mikono wale tu watakao toa labda dola 1000, wao watapewa
sehemu maalum ya kukaa, hivyo lipia mapema ili ukutane na MUNGU au muujiza
wako. Nakueleza wewe uliyelipia na utakayoendelea kulipia bado hautakutana na
MUNGU kabisa bali unajitolea sadaka kwa mashetani pasipo wewe kujua, ila huyo
mchungaji anajua anachokifanya na mpaka afanye hivyo ameshakua sugu kabisa,
amejawa na ujasiri wa shetani, hivyo unakuwa umekutana na mbwa mwitu na wamekula
pesa zako au kukunyang’anya mali zako wakitumia jina la YESU. Ndugu kama
ulishakutana na jambo kama hilo uelewe ulikwenda kwa mbwa mwitu na siyo
mchungaji wa YESU, na zaidi unapotoa pesa katika ulimwengu wa roho ambao kiuhalisia
ni wa giza, wanatumia mapepo na majini kukuharibia vitu vyako na matokeo yake wewe
unajua ulitoa pesa ili ujibiwe na MUNGU lakini hauoni majibu, na hali inazidi
kuwa mbaya, tambua ya kwamba mapepo mbwa mwitu yanaendelea kula vitu vyako
ukiwa hai huku unatembea ila haujielewi na kama si Neema ya MUNGU ikakutana na
wewe hautapona, utaangamia kabisa, kwa sababu picha halisi ya mtu kwenda Mbinguni
inahusiana na uhusiano wake mzuri alionao na MUNGU wakati akiwa hai, ukiona uhusiano
na MUNGU ni mbaya basi utaenda kwa wabaya na kama hutajitoa au kujitenga na
kutoshirikiana kabisa na mbwa mwitu kiroho pamoja na ibada zao, basi unakuwa umefanana
na mwana wa mbwa mwitu na wewe utafuatana nao siku ile ya mwisho. Tafuta mahali ambapo yupo mchungaji wa kweli
wa MUNGU na siyo mchungaji mbwa mwitu. Kama nilivyoelezea kuhusu tabia za mbwa
mwitu (wild dogs) kimwili na kiroho wana
tabia hizo hizo; za kuua kila kitu hata karama uliyonayo au vipaji au maono au
mipango mizuri aliyokupangia mwenyezi MUNGU hapa ulimwenguni.
4.
Anapofanya harambee au minada ya masoko katika
nyumba ya MUNGU, tendo hilo YESU alilikataa na aliwafukuza, soma Marko 11: 15-18. Sasa mbwa mwitu wa
kiroho wamerejesha biashara katika nyumba za ibada na matokeo yake watu hawamwoni
MUNGU bali ni mateso na dhiki tupu kwa sababu mbwa mwitu haleti baraka hata
siku moja na wala haleti uzima bali huleta kifo cha kiroho tu. Watu wengi sasa
katika ulimwengu wapo makanisani lakini wameshakufa kiroho, wapo wapo tu,
wanakwenda kanisani kama vile mazoea tu au sheria hauoni mabadiliko yoyote,
hiyo ni dalili hapo ulipo siyo sahihi kwako, ondoka pana ukame wa kiroho, hapo
pana masika ya kiroho ya shetani.
Hata kudaiwa pesa ndipo
ukamwone mchungaji ili akuombee sio sahihi, usitoe kwa sababu huyo anayekudai kwa
kutumia jina la YESU katika moyo wake yupo pepo mbwa mwitu na hao ndio mbwa
mwitu aliowasema YESU.
Mtumishi ambaye anawachagua
watu na kuwaita partners wake na
anawapa daraja la jina la kitu cha thamani sawa sawa na jinsi mtu anavyotoa kwa
ajili ya huduma hiyo mfano gold, diamond (almasi), tanzanite
na mengine mengi, uelewe huyo ndio aina ya hawa mbwa mwitu aliowasema YESU na
mtawajuaje, mtawajua kwa matendo yao ya kuwatesa wanadamu kwa kuwatawala na
elimu ya mapokeo ya shetani. Na zaidi mambo hayo hupewa baadhi ya watumishi
wayafanye ili wafanikiwe kujenga ufalme wa shetani au mpinga kristo hapa
duniani. Kwa njia ya kuiba kwa kisaikolojia. Nawaeleza wote hakuna baraka
utapata kutoka mbinguni, kwa sababu huyo anayefanya hayo ndio mbwa mwitu wa
kiroho anayewachagua kondoo wale walionona na kuwaacha wale kondoo waliokonda.
Wenye uwezo kifedha ndio wanono na maskini ni kondoo waliokonda.
YESU alikuja kwa ajili ya watu
wa jinsia zote. Hakuja kuangalia wenye mafanikio tu, watu wote ni wake na wala hana
tabaka. Amenituma niwaeleze ili utakayependa utafunguka na uchukiaye ukweli
utabakia kuangamia na kuteseka. Enyi watumishi wa jinsi hiyo, someni Biblia na
maelekezo ya YESU, ameyakataza mambo hayo kabisa, ukiyakifuata tu inakuwa ni
kumfuata mbwa mwitu. Na kama unamfuata mbwa mwitu basi unakuwa tayari ni
mawindo yao na kukufanya kuwa umeshawindwa na kutekwa na shetani kupitia wao.
Kulazimisha au kuwaomba waumini
walipie kiasi fulani kama sheria iliyopitishwa na kanisa na endapo muumini
atashindwa kulipa hiyo pesa basi endapo atapata msiba au tatizo kanisa
halitashughulika na yeye. Kitendo hicho kinafanya mchungaji huyo kuitwa mbwa
mwitu na YESU kabisa kwa sababu hayo siyo ya Mbinguni. Kazi ya kanisa ni
kuhubiri injili, watu waonyeshwe njia nzuri apendayo YESU na kumfuata YESU na
siyo kufanya mambo ya kaisari kanisani au kutembelea waumini katika nyumba zao
na kudai pesa. YESU hayupo hivyo, na ndiyo sababu alisema muwe makini naondoka
naenda Mbinguni, mbwa mwitu watakuja na hata sasa wamejaa wakiwauma baadhi ya wakristo
katika ulimwengu wote.
Kama ulipewa risiti baada ya
kutoa sadaka yako au kupewa cheti cha shukrani (congratulations) eti ya kwamba umekuwa mtoaji mwaminifu basi uelewe
huyo siyo mchungaji wa YESU bali huyo amekuwa tayari mbwa mwitu. Yapo mambo
mengi ila nitaelezea machache kwa leo ili mpate kuwaelewa mbwa mwitu ambao YESU
alisema, ili muwajue wakoje na mtawajuaje. Na vile vile uweze kujua utajilindaje
nao ili usije ukang’atwa na mbwa mwitu wa kiroho. Najua hata wengi mnaosoma
mmeelewa, zaidi na wengine mpo katika mabanda yao kwa sababu mwokozi YESU yeye
anajenga kanisa na katika kanisa mambo hayo hayataki anaumia roho yake kwa sababu
anampenda BABA yake, tena bila unafiki na je kwa nini mtumishi asimpende YESU
bila unafiki mpaka unaamua kuwa jangili au mwizi wa kufoji Neno la MUNGU
ukidanganya watu kwa kuchanganya na uongo kwa sababu hawalijui Neno.
Amenituma mimi Nabii Hebron
niwaeleze yote hayo. Mpo wengi mnalia na mmekata tamaa na MUNGU kwa sababu mbwa
mwitu wamewang’ata kiroho mmebakia hoi. Sasa mtapona mtakapoachana nao mje
kwake YESU wa kweli na Yeye atawaweka huru. Mbwa mwitu ndio hao watumishi ambao
wanalitumia jina la YESU kufanyia biashara. Mtu mmoja alikuja kushtaki kwangu ana
matatizo mengi, alienda aombewe lakini matatizo yapo pale pale. Na kuna siku mmoja
akawa anasikiliza redio, mtumishi mmoja akatoa namba zake mwenye kuhitaji
msaada zaidi ampigie, na yeye kijana akafanya hivyo akamweleza tatizo lake huyo
mchungaji naye akasema MUNGU amesema tatizo lake ni kubwa sana hivyo atume
sadaka kubwa, kijana akaogopa akachanganyikiwa akamwambia mimi sina sadaka
kubwa, mchungaji akamuuliza anayo ngapi, kijana akamwambia ninayo TSh. 20,000/=
akamwabia hiyo ni ndogo kijana akaomba apunguziwe (bargain) sadaka ya kutoa (jamani hii ni aibu, mchungaji ana bargain
sadaka ya mtu), akamwambia MUNGU anataka utoe TSh. 60,000/=, kijana akamwambia
sina kiasi hicho akiamini MUNGU anataka, akaongeza ikafika TSh. 30,000/= akampigia
mchungaji, mchungaji akasema ni ndogo akakata simu. Sasa cha kushangaza baada
ya kijana kukatiwa simu na yeye akaamua kuwa kimya, baada ya muda mchungaji akampigia
simu kijana akamwambia haya tuma sasa hiyo TSh. 30,000/= kijana akajibu situmi
tena, MUNGU gani huyu kigeugeu nilimpa TSh. 20,000/= akakataa, nikampa TSh.
30,000/= akakataa, akamwambia sitaki situmi tena, wewe siyo mtumishi wa MUNGU.
Huu ni ushuhuda mfupi zipo shuhuda nyingi za jinsi hiyo, ingia katika website
yangu www.prophethebron.or.tz
katika link ya YouTube utayaona mengi na utaujua ukweli zaidi. Mwisho kijana alikuja
nikamwombea akapona na alipopona akatoa ushuhuda akimfurahia MUNGU aliyemponya
bila malipo yoyote. Sasa unaona, kijana huyu alikutana na mbwa mwitu na siyo
mchungaji na labda hata na wewe umeshakutana nao, nakupa pole katika jina la
YESU ila nakuombea uwekwe huru na usitumikishwe wala kutapeliwa.
Ukisoma Neno la MUNGU linasema
mtumishi wangu unapopata tatizo usijisumbue wewe rudi kwangu niombe nitafanya. Sasa ni aibu tupu kama kuna sehemu roho za
ukoma au omba omba ya mahitaji zimejaa katika baadhi ya makanisa na kama hizo
roho za shida ndizo zipo, sasa hauoni YESU hayupo hapo. YESU aliwaweka huru watu
wote wenye mateso, shida na vifungo
mbali mbali bila malipo yoyote.
Angalizo:
Kwa
ufupi, uwatumie ujumbe huu na wengine wakatae kuongozwa na mbwa mwitu au mpinga
kristo, kwa sababu hao ndio mbwa mwitu aliowasema YESU. Najua maelfu hamkuelewa
maana ya fumbo hili, nina amini kwa sasa mmelijua na baadhi ya watumishi wengi
baba zao wa kiroho pasipo kujua na wengine wakijua wamewaingiza katika mtego
huu, sasa tubu, ili uwe kondoo mzuri wa YESU na utengwe na kundi la mbwa mwitu
wa kiroho. Sema najitenga na mbwa mwitu wote wa kiroho katika jina la YESU.
Amen.
NABII
HEBRON.
USISAHAU KUSUBSCRIBE YOUTUBE CHANNEL
YETU YA PROPHET HEBRON KWA KUBONYEZA LINK HII https://www.youtube.com/prophethebron?sub_confirmation=1 KUTAZAMA
VIDEO ZAIDI