MBEGU MBAYA
MBEGU NZURI HUZAA MBEGU NZURI NA MBEGU MBAYA HUZAA MBEGU MBAYA
BWANA YESU ASIFIWE! Basi ikiwa na maana kwamba
siku zote mbegu mbaya haiwezi kuzaa tunda zuri, wala mbegu nzuri haiwezi ikazaa
tunda baya, maneno haya aliyasema Yesu lakini ni kama fumbo.
Ukisoma Neno la Mungu kutoka katika
kitabu cha Mathayo 13:36-43; Neno la Mungu linasema 36Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani, wanafunzi wake
wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. 37Akawajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa
Adamu; 38lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni
wana wa Ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; 39yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na
wale wavunao ni malaika. 40Basi,
kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika
mwisho wa dunia. 41Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao
watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, 42na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na
kusaga meno. 43Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika
ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie.
Bwana Yesu asifiwe, mfano huu Bwana Yesu
alioutoa una maana kubwa sana, siyo kwamba Bwana Yesu ni mkulima wa shamba la
mahindi au maharage, mbegu ambayo aliyokuwa anaongea hapa Bwana Yesu ni yake
mwenyewe ambayo anaipanda yeye na hii mbegu ni yeye mwenyewe, lakini nataka
ujue kuna mbegu mbili, katika hizi mbegu mbili na pia zina wakulima wake, Yesu
ana mbegu nzuri, shetani ana mbegu mbaya, lakini mashamba ya kupanda hizi mbegu
ni wapi? Ni kwa wanadamu. Achana na mfano ule tunaojua wa haya mashamba ya
kawaida tunayoyalima, huu ni wa kiroho, ndiyo maana Yeye mwenyewe alitoka
mbinguni akaja hapa duniani, Yeye akaonyesha njia, namna ya kupanda mbegu, sasa
ukipanda mbegu nzuri utavuna mazuri, ukipanda mbegu mbaya utavuna mabaya, ni
kama vile kwenye mashamba ya kawaida ukipanda mbegu mbovu haupati kitu na hata
siku moja haiwezekani hapa duniani wewe uwe na shamba lako halafu mazao yameiva
ukaenda kuvuna kwa mwingine, ndivyo itakavyokuwa ile siku ya mwisho, wewe
ambaye Yesu amependa mbegu ndani yako ndiye atakaye kuvuna, kama ni shetani
amepanda yeye ndiye atakuvuna, kwa hiyo nataka mnielewe, hizi mbegu
zinavyopandwa, mbegu zinapandwa kupitia watumishi pale unapoongozwa sala ya
toba, kama mtumishi amejiita au yeye ni mtafuta pesa au ni wa mazingaombwe basi
unapokiri ile sala ya toba tu ndivyo ndani yako hiyo mbegu inapandwa.
Bwana Yesu asifiwe, wewe ndiyo shamba,
lakini tu ukikutana na yule mtumishi wa Mungu wa kweli; pale unapokiri ile sala
ya toba, mbegu nzuri inaingia ndani yako, sasa inakuja shida na unaanza
kujiuliza “nimeokoka mbona mambo yangu hayaendi?” je ni mbegu mbaya imepandwa
au ni nzuri? Bila shaka ni mbaya, nadhani mnanielewa, na utakuta mwingine
anaokoka, anakutana na mbegu nzuri anafanikiwa kwa haraka, sasa kosa haliko
kwako unabaki na wewe kufundishwa kufa na shida zako, mimi nasema hakuna kufa
na shida hapa, hata mimi Hebron mbegu mbaya nimeshaipitia, niliongozwa sala
ya toba na huyu na yule, nakiri, aidha nikisikia kwenye redio au kwenye TV
nakiri mpaka nalala chini ya TV naambiwa kiri hapa kumbe mimi nakiri sala ya
toba ya mchawi, mbegu mbaya inaingia ndani.
Bwana Yesu asifiwe, hilo shamba ni wewe
lakini hili shamba pia na shetani analitaka. Mungu ana wivu ili apande mbegu
kwako akapate kuona utukufu wake kupitia maisha yako. Shetani naye hivyo hivyo anavizia
na watatumia hata jina la Yesu, ni somo refu kidogo lakini nitakufundisha kwa ufupi
ili ukapate kuelewa kwa sababu kuna mambo mengi ya kufundisha. Ukisoma mstari
wa 43 unasema hivi, ”Ndipo wenye haki
watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie”.
Sasa unaweza ukasema mimi nakwenda mbinguni lakini mbegu ilyopandwa na baba
yako wa kiroho kumbe yeye ni mwovu, na hizi mbegu zinapandwa na
makuhani, ina maana kama mimi hapa Hebron mimi ni mtumishi, mimi ni kuhani,
kama mimi ni mbegu mbaya na hao wengine wote nitakao waongoza sala ya toba wote
watakuwa wamepotea, lakini kama kuhani yeye amesimama katika kweli ya Mungu,
mkiongozwa sala ya toba mambo yote yanakuwa safi.
Bwana Yesu asifiwe, sasa kuna shida, kuna
mbegu ya Mungu imeingia ndani lakini pia kuna mbegu ya shetani, siku zote mmea
wa muhindi ukiwa na gugu, gugu lazima litakuwa linanyonya ule mmea wa muhindi usikue,
sasa nataka hii mbegu ing’oke ili ibaki mbegu ya Mungu halisi (original) peke yake na hapa itakuwa ni
mwisho wa kusikia mbona sibadiliki, mbona nafunga sana lakini niko kituo
kimoja, mbona naomba sana nachoka naishiwa nguvu za rohoni. Hautendi dhambi,
kumbe gugu linakunyonya hapo, ndio mambo ya kiroho yalivyo lakini ni somo zito
sana. Mimi mwenyewe Hebron katika maisha yangu sikuwahi kufundishwa hili
nilikuwa nikimsikiliza Mungu ninatetemeka, sikutaka hata mtu asogee karibu
yangu nilijifungia, niliandika tu na kusikiliza, lakini nitakufundisha kwa
kiwango kile ambacho kinatakiwa kwako mengine ni ya kwangu, maana mimi amenituma
kupanda shamba lake na kung’oa mashamba ya shetani, ndio maana Biblia
inasema “kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang’olewa”. Unaweza
ukamkuta mtu anahangaika, unamuombea na anampenda Mungu sana lakini kuna
magugu, jua kwamba na magugu nayo huwa yanaomba na yanafunga.
Bwana Yesu asifiwe, ukisoma katika kitabu
cha Mathayo 7:16-21, Neno la Mungu
linasema 16Mtawatambua kwa
matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? 17Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda
mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. 18Mti
mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. 19Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa
ukatupwa motoni. 20Ndiposa kwa matunda
yao mtawatambua. 21Si kila mtu aniambiaye,
Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaje
mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
Nikuulize kitu, wewe una mbegu mbaya
imepandwa ndani yako na shetani halafu unataka baraka za Mungu je! Inawezekana?
Je, umeshawahi kuona mnazi unazaa maembe? Mwenye akili na aelewe, ndiyo wewe
sasa kuna baraka za mbinguni zimeandaliwa kwa ajili yako lakini unakuta
wewe ni mnazi sijui mnanielewa, kosa siyo la kwako ndivyo shetani anavyofanya
kazi ya kuporomosha watoto wa Mungu, lakini mwisho wake umepita, sasa ni wakati
wa kumpinduapindua, kama vile Mungu anavyonituma mimi na wale watumishi wa
Mungu wanaosema kweli kupanda mbegu zake ili watu wabadilike, sasa watu
watang’olewa huko ili wasonge mbele. Shetani amepanda hizi mbegu muda mrefu
sana, haiwezekani mbegu ya Mungu iwe hivyo.
Bwana Yesu asifiwe, ukisoma Mathayo 7:19, Neno la Mungu linaseama “Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa
ukatupwa motoni”, sasa mti huu unaozungumzwa hapa ni wewe au ni mwingine,
kama umeshafunguliwa ukawa mti mzuri mshukuru Mungu maana unaweza ukajiona wewe
uko sawasawa kabisa unaenda mbinguni lakini kumbe wewe ni mti mbaya umebatizwa
kwa kisima, utakatwa. Nilikuwa nikijiuliza sana inakuwaje siku ile Yesu aseme
sikujui, sikujui, hata wewe ukiambiwa Yesu anasema sikujui, sikujui siku ile ya
mwisho wakati wewe umekuwa ukilala na kukesha kanisani, unasema umekoka, halafu
anasema sikujui, sikujui! Sasa unaanza kuelewa? Haya umewekwa kwenye
ubatizo wa kikombe, mwisho wake utakatwa! Eeh siyo mbegu yake, Yesu mwenyewe kabla
ya kuja hapa duniani alitangulizwa Yohana, Yohana akaja akaweka mbegu ileile
aliyopewa na Baba yake mbinguni, hakuipindisha, wala hakuigeuza, akasema
muifuate vile ilivyo. Mimi mwenyewe Hebron ni mmoja wa mkristo aliyekuwa anaitwa
kwa jina la dini ya mtu fulani badala ya kuitwa mwana wa Mungu, lakini yeye
anamuitwa kama vile muhebron, na mimi nasema ndiyo dini yangu. Wanikome, mimi
ni Yesu tu sitaki mbegu za majina ya watu, mfano mimi eti nakufa halafu useme
mimi ni muhebron, mimi ni wa kanisa la muhebron, wapi wewe, sasa hiyo
mbegu ni nzuri au ni mbaya? Bila shaka hiyo ni mbegu mbaya, basi ndivyo
itakavyokuwa.
Ukisoma Mathayo 7:20-21, Neno la
Mungu linasema “20Ndiposa kwa matunda
yao mtawatambua. 21Si kila mtu aniambiaye,
Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaje
mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.” Unaona Biblia inavyoelezea wazi? Sasa wengi ni mbegu mbaya, Bwana
anasema hivi “siyo wote waniambiayo vile vile wataurithi ufalme wangu”,
sawasawa? Sasa mimi sitaki mtu aje akatwe pembeni, mbegu mbaya, tunaichambua
Biblia ikae kichwani ili uelewe, unaweza ukasoma mistari, lakini kama hamna
mafunuo ni kazi bure.
Bwana Yesu asifiwe, ukisoma Mathayo 7:26-27, Neno la Mungu linasema “26Na kila asikiaye hayo maneno yangu
asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga,
27mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo
zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko likawa kubwa”. Biblia iko wazi lakini jambo ninalotaka
kulielezea kwa undani hapa ni “mbegu
mbaya”, nani anataka kuwa mbegu mbaya? Bila shaka hakuna, lakini
tulishakuwa mbegu mbaya, kwa kujua au kwa kutokujua. Ukisoma Mathayo
15:13-14, Neno la Mungu linasema “13Akajibu, akasema kila pando asilolipanda
Baba yangu wa mbinguni litang’olewa. 14Waacheni
hao ni viongozi vipofu, Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia
shimoni wote wawili”.
Bwana Yesu asifiwe, Biblia inazidi
kuelezea acheni viongozi wa vipofu, tunaongozwa, tunapandiwa mbegu na tunatii
huku tukiambiwa ni habari ya Mungu. Bwana Yesu asifiwe, wengine tunaabudu
sanamu na tunajiaminisha kwamba tunaabudu habari ya Yesu, kumbe ni mbegu
nyingine, lakini nataka nikuambie, alisema watakuja watatumia jina lake na
ndivyo ilivyo sasa maana shetani na yeye anatumia jina la Yesu kupanda mbegu
zake. Mbegu hizi ni makanisa, unaweza ukaona makanisa mengi sana duniani, lakini
kila moja lina mkulima wake, liko kanisa ambalo Yesu amepanda mbegu na liko kanisa
ambalo shetani amepanda, sijui mnanielewa? Na unapokaa hapo na wewe unakwenda;
kama ni kwa Mungu umekuwa mbegu ya Mungu na kama ni kwa shetani na wewe
umekuwa mbegu ya shetani; hiyo imeruhusiwa. Ile siku ya mwisho watakuja Malaika
wa Mungu kukuchukuwa, na hiyo siku ya mwisho nataka ujue watakuja malaika wa
shetani kukuchukuwa vilevile maana aliye asi yuko na wafuasi wake. Siku hiyo
Yesu ataangalia shamba lake, je ni wewe, “twende”. Wako watakaosema, Bwana Yesu
mimi ni mkristo, Yesu atasema “hapana
mbegu ya kikombe hiyo, ya miujiza ya kutoa mawe hiyo, mbegu ya kisima hiyo,
mbegu ya harambee hiyo, siyo yangu”
Tunarudi kwenye somo, mbegu nzuri huzaa
mbegu nzuri, mbegu mbaya huzaa mbegu mbaya, mimi hapa Hebron najijua, wewe nichunguze
utajua je ni mbegu mbaya au nzuri, ndiyo maana hii mbegu iliyopandwa na
Yesu ni ya Yesu mwenyewe, hujasikia hata siku moja nikimtoza mtu pesa,
hujasikia hata siku moja mie natamka wale wa elfu, elfu wasimame hapa,
hujasikia nabatiza kwa jina la mchungaji, hujasikia hata siku moja mimi nikiomba
michango kwenye redio na TV. Mbegu nzuri ni sawasawa na Neno lake “nimekupa bure toa bure”, sasa wewe
unaweza ukaona unamfanyia Bwana kumbe wewe uko kwenye mbegu ya shetani,
umepoteza pesa, utafundishwa habari za kutoa fungu la kumi vizuri sana, sasa
wewe unabaki kusema “mbona Mungu hajibu na mie nimepanda” hivi mkulima akipanda
si huwa anavuna? Sasa mavuno yamekuwa ni ukame, baraka hakuna, ni mikosi tu.
Bwana Yesu asifiwe, siku zote nataka
nikuambie kusema kweli ni vita, ukiwa unasema uongo unakuwa rafiki, mimi sitaki
urafiki na mashetani; sitaki na wewe sema sitaki, utamalizwa. Kwenda mbinguni
siyo kufungwa kamba miguuni jamani, ni Neno la MUNGU pekee, lakini sasa Neno
linabadilishwa, kuna mbegu imechanganywa ukweli na uongo; unataja kuna Pasaka,
lakini kuna sanamu, hiyo ni mbegu mbaya, kwa hiyo mbegu mbaya anayeipanda ni
mbaya, ni shetani. Kwa hiyo shetani ataichukuwa mbegu yake, wewe unasema mimi
nitakufa na dini ya mama yangu na baba yangu hiyo ni mbegu, utakwenda huko huko,
toa watoto wako kwenye mbegu mbaya, ndiyo maana hii mbegu mbaya ukimkuta mtu
anayo anajiita ni mkristo lakini haongelei habari ya wokovu, ukimweleza habari
ya wokovu hakuelewi anakuzungusha au siyo jamani, kama nyie ni mbegu moja mtaelewana.
Ndiyo maana mwingine atakwambia kama umeokoka wewe umechanganyikiwa lakini yeye
anajiita mkristo na anabeba Biblia anasema Baba yetu uliye mbinguni, kumbe ni
mbegu mbaya, sasa unaelewa?
Bwana Yesu asifiwe, nakutia moyo,
inawezekana watu wamekukataa, wamekuchukia, haijalishi, wewe shukuru Mungu,
wewe ni mbegu nzuri, mbegu mbaya haikukubali lakini hiyo mbegu itafika wakati
itakwama, itakwama mpaka itanywea na itakuacha na watu wataanza kukukubali na
wengine watatoka huko wawe mbegu nzuri ili tusonge mbele. Unaweza ukawa ni
mchungaji, mwinjilisti lakini wewe ni mtumishi wa kupanda mbegu mbaya tu. Mimi
nawaambia kama ni watu watakao hukumiwa zaidi, ni watu wanoitwa watumishi kwa sababu
wao ndio wanaofanya watu wapone, waende mbinguni, lakini sasa wao ndio
wanaofanya watu wapelekwe jehanamu, lakini wapo pia watumishi wamejaa mbegu
mbaya wanaokwenda vituo mbalimbali vya maombi dunia nzima na anayeipanda ni
baba yao shetani. Mwingine alikuwa ni mbegu ya Mungu, alianza na Mungu lakini
akaondoka akamkataa Mungu na shetani akapanda mbegu mbaya juu yake; mtawajuaje,
kwa matendo yao.
Jambo jingine si kwa kutumia uchawi bali
ni shetani na nguvu zake anafanya kazi ndani ya kanisa, mtumishi kutenda kwake
ni kama kwa shetani, ananena, anaimba kwaya na mengine, si alisema watatumia
jina langu? Unafikiri bila kufanya hivyo watakupata wapi wewe, kwa njia hizo
hizo wanapanda mbegu mbaya wakati wewe unataka amani, mbegu nzuri ni amani.
Unatakiwa kukaa kwenye kiti kanisani kwa amani hakuna mambo ya michango, siyo
ibada inakaribia kwisha mnaambiwa wamama bakini wale wa elfu-elfu n.k, hiyo haitakiwi,
hiyo ni mbegu mbaya, peleka huko hatutaki mbegu mbaya. Unaweza ukaambiwa pokea
baraka, lakini anayekwambia pokea baraka yeye ni mbegu mbaya, na unaposema
amen, shetani anapiga muhuri katika ulimwengu wa roho, maana yake na iwe hivyo,
hapo ujue umebarikiwa na mbegu mbaya. Nataka uvunje ule utabiri wa mbegu mbaya.
Hii habari ya kuambiwa pokea, ukapokea mbegu mbaya, hiyo inazuia usipokee yale
ya mbegu nzuri ya mwenyezi Mungu. Kaa na mimi nikufundishe, nikuelekeze, kazi
hii ni ya kwake Mungu, hii sio kazi ya kwenda kusomea chuoni, kwani hakuna mtu
anayeweza kusomea kazi ya kumpeleka mtu mbinguni. Mwalimu wa kazi ya Mungu ni Roho
Mtakatifu mwenyewe.
Nataka uelewe, umewekewa mbegu mbaya, toka
ulipozaliwa tu ukawahiwa badala ya kuwekewa mbegu nzuri ili ukastawi katika
dunia ukawekewa mbegu mbaya, hata hawa watumishi wengine hawajui, wamesomea,
sijui wana shahada (degree) za wapi,
za ajabu ajabu na wenyewe wanaendeleza mbegu mbaya tu. Je mbegu mbaya inazaa
mbegu nzuri, kama wewe mkristo ni mbegu mbaya, je unategemea baraka? Hapo
tegemea mikosi, ndoa ina mbegu mbaya halafu wewe unataka mazuri, je mbegu mbaya
imetoka? Maana kazi ya shetani ni kuharibu. Kuna mbegu mbaya ya mizimu, majini
na mapepo. Nina ziamuru zote zitoke kwa Jina la Yesu.
Bwana Yesu asifiwe, nitaongelea mfano wa
kanisa ambalo ni mbegu mbaya, ukiingia kwenye nyumba ya mbegu mbaya na wewe umetekwa.
Aidha umetoa sadaka kwenye mbegu mbaya, mimi nakwambia utajiri hauji, mpaka wakuchomoe
huko kwa maombi halafu mbegu nzuri ijae, maana sadaka zako Bwana ameziona,
lakini sasa itashuka wapi? Kuna magugu, ambayo ni mbegu mbaya yamejaa hapo, ndio
maana akasema yang’olewe mapando mabaya? Kwa hiyo, shetani anakubana mahali ukubali
wewe mwenyewe usifanikiwe pasipo kujua au kupenda.
Bwana Yesu asifiwe, ziko mbegu za uchawi
pia, mtu anapokwenda kwa mchawi katika ulimwengu wa roho anakupandia mbegu ili
uumwe kichwa, anakupandia mbegu mwaka huu usifanikiwe na kweli unaona mwaka huo
haufanikiwi, mimi nakwambia ukiwa na Yesu yeye ambaye ni mbegu nzuri hakuna
mbegu ya uchawi itaingia ndani yako, maana mchawi kabla hajakuwekea mbegu mbaya
anakuchungulia kichawi, wakikuchungulia vitu vyako vinaharibika, unaweza kukuta
labda ni gari likishapandiwa mbegu ya kuharibika, kila siku gari litaharibika, vile
vile wachawi wanaweza kukuwekea mbegu mbaya, kila ukishika pesa wewe unazitoa
tu haufanyi kitu cha maana, hata shati hununui, aidha unaweza ukawekewa mbegu mbaya
wewe mwanamume au mwanamke unakaa tu haufanyi kazi yaani kila kitu hauwezi na
unakaa tu wakati Mungu amekuumba mbegu nzuri ikafanye kazi, ukafanikiwe ukawe
kichwa. Sisi tumeambiwa ni uzao wa Ibrahimu ambao ni wana wa baraka wa Yakobo
tuwe vichwa lakini inakuaje tumekuwa mbegu mbaya, mimi nakwambia utakuwa mkia
tu na ndio maana utaona kwenye kanisa wengine wanaingiwa na wivu na kuanza
kusema “mbona yeye anafanikiwa mimi sifanikiwi”. Sasa umeshajua siri, kama
mbegu mbaya haijatoka mimi nakwambia utakufa na mvi hata bati haununui, halafu
unasema kwa Baba yetu kuna kila kitu, angalia, kama kuna mbegu mbaya mimi nakwambia
Mungu hashushi kitu chake juu yako maana si shamba lake, wewe utapalilia shamba
la mtu uache kupalilia la kwako?
Bwana Yesu asifiwe, Mungu na shetani ni
maadui, Mungu na shetani hawana maelewano kabisa mimi nakwambia, ni mbaya,
mbaya; unaweza ukawekewa mbegu usizae. Hizi mbegu pia zina maagano yake, mbegu
mbaya ina agano lake, agano la kwanza ni la ubatizo wa kikombe hizi batizo za
ajabu, ajabu je umezitoa katika maisha yako? Utasikia mtu anasema mimi nakufa
na ubatizo wangu mimi nakwambia utazikwa na utaenda kwa shetani, Yesu
alivyokuja yeye agano lake alilolionyesha ni ubatizo wa maji mengi yanayotembea, hilo ndilo agano lake, sasa wewe
unaambiwa ubatizwe unasema mimi sitaki au unakuta mtumishi anakuhubiria wakati
yeye ana agano la mbegu mbaya; ubatizo wa kikombe, ubatizo wa kisima, ubatizo
wa jina la mchungaji, sasa mwenye kuelewa na aelewe.
Bwana Yesu asifiwe, Yesu alikuwa
anafundisha kwa mifano, na mimi nafundisha kwa mifano, wewe chunguza kwa faida
yako, mtu asikutikise imani yako maana unaweza ukatikiswa imani yako na mbegu
mbaya, utasema sisi watoto wa Baba mmoja, mimi sijui kama Yesu ana mbegu za
makanisa ya mashoga, mimi sijawahi ona, lakini nalo litaitwa kanisa, mimi
sijaona mbegu ya Yesu ya watu wanaabudu sanamu, mbegu ya Yesu, ukisoma Neno
lake watu wanaombewa bure, mimi sijaona Yesu akiwaambia watu wewe leta pesa
zako ili Mungu akuponye, mimi sijaona hiyo mbegu, mwenye akili na aelewe.
Utaona unanenewa kumbe watu wanamwagiwa mapepo, maana shetani yuko kazini na Mungu
yuko kazini, lakini Mungu mashamba yake ni machache, lakini mimi nakwambia utukufu
wa kanisa la mwisho Mungu atavuna kuliko shetani na unaenda kunyanyuka zaidi na
zaidi.
Bwana Yesu asifiwe, mimi nakwambia ingekuwa
ni mbegu za Mungu kila mahali, kweli ingekuwa hakuna uchawi, watu wangelala kwa
amani, hakuna wizi, hakuna watu kuvuta madawa ya kulevya; lakini sasa unakuta mchungaji
(pastor) au askofu (bishop) na yeye ndio kwanza anaingiza kontena
la madawa, sasa mnasema wanachafua kanisa, ndio wanachafua kanisa la kwao la
mbegu mbaya na si kanisa la Mungu wa kwetu. Madawa ya kulevya ni kitu kibaya
jamani, msije mkatumia, sijui eti bangi nibangue, acha hizo, haifai. Hiyo ni
mbegu mbaya ya kuharibu akili na maisha yako, utadumaa, hiyo nitafundisha
wakati mwingine.
Bwana Yesu asifiwe, natakueleza moja ya
maana ya mmea huu unaoitwa bangi (marijuana),
asili ya mbegu ya mmea huu ilitoka kuzimu, kuzimu kuna mimea ilitupwa duniani,
mmoja wapo ni mmea wa bangi, unaelewa? Unapovuta tu jini linaingia kwenye
kichwa, kama umevuta jini la kusoma utasoma sana, kama jini la kuimba mziki
utaimba sana, utacheza mpaka watasema anakipawa kumbe ni bangi nibangue,
Haleluya! Nina amuru kwa Jina la Yesu mbegu mbaya toka katika maisha yako. Kwa
nini wewe hujiulizi kuna mtu katika hali ya kwaida hawezi kuongea mpaka avute bangi,
acheni hiyo kitu kabisa haifai, wengi mmepuliza, uongo? Acheni hiyo
haifai.
Bwana Yesu asifiwe, mbegu mbaya kwenye
ubongo ni majini, mapepo, hazifai, ziko mbegu za mateso, mimi nakwambia utaona
mateso tu, ikitupwa kwa mtoto hamuelewani, wewe unamwambia hivi na yeye
anafanya vingine matokeo yake unamtandika, acha kumtandika, mlete kwa Mwenyezi
Mungu hiyo roho itolewe atabadilika tu. Amenituma kutengeneza, mimi neema ya
Mungu ilishanipitia, mbegu mbaya ikatoka, ikaondoka, nikiomba inakuwa,
nikitamka inakuwa, wakishindana wanashindwa, mbegu nzuri na itazunguka dunia
nzima.
Bwana Yesu asifiwe, mbegu mbaya unapewa
kiroho, ziko za kichawi, ziko za kimila, ziko za kiganga, ziko za kidunia;
sizitaki nataka ya Bwana Yesu wa kweli, ziko za mpinga Kristo, hizi zina
maagano yake ndio maana zinakuwa na masharti unasikia kama ulikuwa hutoi sadaka
hawakuziki, hayo ni maagano yao. Kuna watu wana mbegu mbaya mpaka
wamezikwa makanisani, jamani duniani kuna vituko sana, kanisani kabisa
patachimbwa na mtu anavalishwa na sanda analala akijua anampenda Mungu halafu
anakaa pale wanamzunguka halafu anatoka kumbe ndiyo amefanywa kafara. Sasa kama
kuna mbegu mbaya pia ujue kuna shamba baya, mbegu mbaya inapelekwa kwenye
shamba baya na mbegu nzuri inapelekwa kwenye shamba zuri yaani kuna kitu kizuri
cha Mungu kinaenda kwa watu wa Mungu na kitu cha shetani anapeleka kwa watu
wake lakini siri anakuwa nayo kuhani. Mafundisho ya uongo ni mbegu mbaya
unapoyaamini na kuyashughulikia kama vile kubusu mbao au sanamu na mambo
mengine ya ajabu, hutaki kuokoka unaambiwa wewe ni mkristo utaenda mbinguni
ukiokoka kata shauri, zote hizo ni mbegu mbaya, sema sitaki kwa jina la Yesu. Hiyo
mbegu mbaya kuna mtu anaye inyeshea ili ikue na inaombewa na katika ufalme
mwingine, inatolewa sadaka na wanafunga. Wanafundishwa madhabahuni na wanazidi
kukomaa namna wanavyotaka na ukishakomaa unatii yale ya kwao.
Bwana Yesu asifiwe, na ile mbegu ya Mungu
na yeye Mungu anainyeshea, anakufundisha, anakuombea, anakuinua na wewe
unashangaa unaanza kutii ya Mungu, mimi Mungu alivyoniita alinipanda yeye
ananinyeshea, ananikuza naendelea kunyanyuka na wewe hivyo hivyo nataka uwe
kama mimi, mbegu mbaya iwe mwisho. Mbegu mbaya ina utii wake, utaona kuhani
anakuangalia mara tu unaanza kutetemeka na unatoa kila kitu unamuachia,
utasikia akisema “bwana” anasema nyie wagumu sana lakini “baba” wasamehe
usiwauwe, na kwa sababu kuna mbegu mbaya ndani yako inatii ina muunganiko (connection). Mimi nakwambia huyo ni
mwongo, kwa sababu Mungu wetu hauwi watu ni Mungu anayeokoa. Wewe umeshasikia
wapi kuna hela ya kununua cheti cha kwenda Mbinguni? Mimi nilikuta kwenye
baadhi ya makanisa kuna mambo hayo sijui laki laki na kuna watu wamenunua, mimi
nakwambia cheti chako cha kwenda Mbinguni ni sala ya toba na utakatifu pekee. Damu
ya Yesu ilimaliza pale msalabani, hiyo ni mbegu nzuri, sasa wewe unatoa hela ya
cheti cha kwenda Mbinguni, ndio unapelekwa huko kuzimu. Utajiri wako unaharibika,
baraka zinaharibika, unapowekewa mikono na mtu mwenye mbegu mbaya ujue
umechukua matatizo na siyo baraka.
Bwana Yesu asifiwe, ziko mbegu mbaya za
chanjo, kujichanjachanja mwili, hizo ni mbegu mbaya, kwa nini Biblia ikasema
mapando yote yang’olewe? Mungu anajua hayo yapo, sasa badala ya kuwa kichwa
unakuwa mkia kwa sababu ya mbegu mbaya. Mbegu za kuwa mikia mimi sizitaki. Halafu
mtoe imani ya kila kitu ni kurogwa, mengine ni shetani mwenyewe, jiulize ni
mara ngapi umesema amen katika mbegu
mbaya? Maana yake unasema na iwe hivyo, Haleluya!
Sema Bwana Yesu, naomba unisamehe, dhambi
zangu zote nilizozifanya, hata pale ambapo niliongozwa sala ya toba nikapokea
sala ya toba na mbegu mbaya ikaingia ndani yangu, kwa idadi zake, naomba Bwana
kupitia Damu ya mwanao YESU KRISTO WA NAZARETI, hiyo mbegu itoke, nichunguze
Bwana, wewe wanijua, mimi sitaki kukataliwa ile siku ya mwisho, maana umesema
kwamba sio wote wasemao BWANA BWANA watakao urithi ufalme wako, Baba yamkini ni
mimi, wewe wanijua sijihesabii haki, mbegu mbaya itoke, iniachilie kabisa,
itoke kwenye baraka zangu, itoke kwenye imani yangu, itoke kwenye fahamu zangu,
itoke kwenye damu yangu, tena itoke na mizizi yake isibakie katika Jina la Yesu,
mizizi ya mbegu mbaya itoke, toka kabisa mbegu mbaya, ondoka, potea, katika Jina
la Yesu. Baba ninakushukuru, pokea sifa na utukufu, najua ya kwamba ule mwisho
Malaika wako wa Mbinguni Watakatifu watakapokuja kuvuna shamba lako na mimi
watanivuna, sitavunwa na mwovu, sitavunwa tena na shetani, naomba Baba
ukarejeshe maana shetani alinivuna, alinitumikisha, alinitesa mpaka nikaona
dunia hii haifai, nikaona maisha hayafai, imebaki ni vilio, nimebaki na
kuteseka, ni kwa Neema yako Mungu ninakushukuru Baba, katika Jina la Yesu,
Amen.
NABII HEBRON.