KONDOO WA YESU WA KWELI HAWASIKILIZI SAUTI
ZA WAGENI
BWANA
YESU ASIFIWE!
Katika somo hili
ninafundisha wafuasi wa YESU wazidi kuimarika katika kumjua YESU wa kweli na
kuijua sauti yake kwa sababu yeye ndiye mchungaji wao, hivyo ni lazima waijue
sauti yake na wanapoijua sauti yake ni lazima kondoo hao hata wakisikia sauti
ya mgeni ni lazima watakataa na watamkimbia kwa sababu watajua siyo YEYE bali
ni mchungaji batili (fake) asiyejulikana.
Ukisoma katika kitabu cha
injili ya Yohana 10:2-6 inasema; “2Aingiaye mlangoni ni
mchungaji wa kondoo. 3 Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia
sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. 4
Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa
maana waijua sauti yake. 5 Mgeni hawatamfuata kabisa, bali
watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. 6 Mithali hiyo
YESU aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.”
Katika ule mstari wa 5, Biblia
inasema mgeni hawatamfuata kabisa bali watamkimbia. Mgeni ninayemzungumzia hapa
siyo wageni hawa wanadamu wanaotembeleana, mgeni ninayemzungumzia hapa ni neno
geni linalotumika katika injili kwa njia ya kuchanganya NENO la MUNGU na uongo.
Sauti ya mchungaji YESU ndilo hili NENO lilivyo bila kupunguzwa wala kuongezwa,
NENO linapoongezwa basi huitwa sauti ya wageni. Ukisoma katika kitabu cha
Ufunuo wa Yohana 22:18-19 imeonya isiongezwe maneno ya kitabu hiki wala
kuyapunguza, ikiwa ina maana kwamba kwa yule atakayesikia sauti ya NENO la
kweli kama lilivyo ndio sauti ya YESU, ambayo ndiyo ya kuwaongoza watu wote ili
siku moja wafike mbinguni. Ikiwa neno ambalo siyo la kweli watu wamelisikiliza
na kulifanyia kazi, basi kwa njia hiyo tayari unakuwa ni mfuasi wa kigeni na
siyo mwenyeji wa mbinguni.
Mwenyeji wa mbinguni ni
mtu yule ambaye anapokea wokovu wa kweli na NENO la kweli. Mgeni ni yule ambaye
yeye ni mwenyeji wa hapa duniani na kufanyika wenyeji wa hapa duniani sababu ya
kuchanganya neno la uongo, yaani hajui sauti ya YESU ni ipi na isiyo sauti ya
YESU haijui au kwa maana nyingine anaweza akawa ni mkristo lakini haijui kweli,
sawa sawa na NENO lisemavyo ishike kweli nayo kweli itakuweka huru kweli kweli.
BWANA YESU ASIFIWE!
YEYE yu karibu kurudi
kuwachukua kondoo wake ambaye siku zote wamesikiliza sauti Yake, kondoo hao
hawazitaki sauti za wageni ili wasije wakapotea.
Nitaelezea kwa ufupi
mifano ya sauti za wageni ambazo kondoo wengi wanazifuata wakijua anayewaongoza
ni sauti ya YESU na kumbe ni sauti za wageni; kwa mfano, katika Biblia
imeandikwa mtoto mdogo abarikiwe, cha ajabu sauti za wageni zimesikilizwa na
wakaamua watoto wadogo wabatizwe; imeandikwa mtu aokoke lakini wengine
hawaokoki na wanabakia kuwacheka waliookoka. Sauti ya YESU inasema uokoke wewe
hutaki kwa sababu nafsi yako imeisikia sauti ya wageni.
Imeandikwa mtaponywa bure,
hiyo ni sauti ya YESU, lakini baadhi ya watu wanatozwa pesa ili waombewe. Mchungaji
anayewatoza watu pesa za maombezi nataka uelewe huyo haongozwi na YESU wa kweli
na wala haisikilizi sauti ya YESU bali huyo ni mtumishi wa kigeni ndio maana
utasikia kuna miungu ya kigeni ni miungu isiyojulikana, hayo ni mafundisho
yasiyokuwepo katika Biblia. Unabatizwa kwa jina la mchungaji, kwenye kisima,
batizo hizo hazipo na Mchungaji wetu YESU alisema tuifuate njia yake, sasa je kubatizwa
kwa jina la mchungaji ndiyo njia yake? Hapana. Kubatizwa kwenye kisima siyo,
kubatizwa baharini siyo, kwa sababu sauti Yake inasema ubatizo ni mtoni katika maji
yanayotembea kama vile mto Yordani.
Wengine wanaabudu sanamu,
wanafanya matambiko, wamegeuza nyumba za ibada kuwa ni nyumba za michango.
Kumbuka YESU alivyokuwepo hapa duniani kimwili kipindi chake aliyakataa hayo
yote na kama sasa yanafanyika, basi uelewe sauti na maonyo yake YESU
aliyoyasema yanapuuzwa na wala hayasikilizwi, watu wangesikiliza sauti ya YESU
hakika wasingeyafuata mafundisho ya uongo na kuchanganya na NENO la kweli au
kupokea mapokeo. Nawaeleza alichonieleza YESU haijalishi wale wanaoipenda sauti
ya wageni watachukia ni bora YESU atukuzwe duniani kote kuliko sauti za uongo zikiendelea
kusambaa duniani kwa njia ya kutumia kanisa na jina lake kuwapoteza watu waende
jehanamu wakipelekwa na mawakala wa shetani. Wapo manabii, mitume, wachungaji,
wainjilisti, waalimu, maaskofu na wengineo ni hao ambao wameamua kusimamia
mafundisho ya uongo badala ya kusimamia kweli wakitumia jina la YESU kutafutia
pesa au biashara. Hukumu imekaribia sijui anayeyafanya hayo atajiteteaje.
YESU anarudi, nawasihi
watu wote wa mataifa yote mkatae sauti za kigeni mkimbie kabisa kwa sababu
unapoabudu mahali ambapo neno huchanganywa na uongo, tayari na wewe unakuwa upo
upande wa mchungaji asiyejulikana na wewe unakua siyo kondoo wa kweli wa YESU,
hii ni kiroho. Elimu ya kiroho ina uongo na kweli, hakuna ushirika kati ya nuru
na giza, ikatae giza ifuate nuru.
BWANA YESU naomba
unisamehe dhambi zangu zote uandike jina langu katika kitabu chako cha uzima wa
milele. Nifungue ufahamu na masikio yangu niijue sauti yako (neno la kweli).
Nalikataa neno la uongo, potea toka ndani yangu. YESU niongoze sasa, wewe ndiwe
mchungaji wangu, siwataki wachungaji wa kigeni tena, nimeijua sauti yako. Amen.
NABII HEBRON.