KONDOO WA
YESU WA KWELI HUZIKIMBIA SAUTI ZA WAGENI!
BWANA YESU ASIFIWE!
Tutasoma katika kitabu cha
injili ya Yohana 10:2-6, Neno la MUNGU linasema “2Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. 3
Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo
wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. 4 Naye huwatoapo nje kondoo
wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. 5
Mgeni hawatamfuata kabisa, bali, watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za
wageni. 6Mithali hiyo YESU aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na
mambo hayo aliyowaambia.”
BWANA YESU ASIFIWE. Neno hili
lina maana kubwa sana, unaweza ukawa mchungaji au mwinjilisti au nabii au
muumini ambaye yuko chini ya sauti za wageni.
Sauti za wageni ninazozungumzia
hapa ni kuhusu habari ya ufalme wa MUNGU, kwa nini tunaambiwa kwamba sauti za
wageni kondoo hawazisikii? Wewe ni mwenyeji wa mbinguni lakini hapa duniani ni
mgeni, sasa wewe mkristo umekuja hapa duniani unataka kusikiliza sauti za
wageni, pale inakufanya wewe kuwa chini ya mchungaji au mwinjilisti wa wageni hutaki
kusikiliza sauti za wenyeji, lakini wale ambao wanasikiliza sauti ya MUNGU aliye
hai wao hawataki kusikia kabisa sauti za wageni maana wanajua si za kwetu,
sijui mnanielewa? Mithali hii YESU aliwaambia lakini hawakuelewa, amenituma
nikwambie habari za ufalme wake, haleluya! Wewe ulitoka mbinguni unatakiwa
urudi mbinguni, kwa hiyo wewe si mgeni ni mwenyeji wa mbinguni, lakini
kitakachokufanya ubaki hapa duniani ni pale tu utakapokubali kusikia sauti za
wageni.
Unapokubali kupokea ubatizo wa
kikombe umepokea sauti za wageni, unataka kuombewa unaambiwa leta pesa umepokea
sauti za wageni, unapoabudu sanamu umesikia sauti za wageni lakini wale wa MUNGU
hawataki kusikia sauti za wageni, wao na mchungaji wao wanataka kusikia sauti ya
wenyeji wa mbinguni peke yake. Sasa wewe unayetaka kwenda mbinguni uhakikishe
kwamba husikilizi mafundisho ya waongo, hizo ni sauti za wageni zinafanya
maisha yako yawe ya kigeni, baraka zako ziwe za kigeni, wakati MUNGU amesema
utafanikiwa katika dunia hii, lakini wewe umechagua kuabudu sanamu hauwezi
kufanikiwa katika Neno la MUNGU, utatoa sadaka sana, mafungu ya kumi lakini
wewe umebatizwa kwa ubatizo wa kikombe, wewe unasikia sauti za wageni.
Sauti ya wageni haiko mbinguni
kwa hiyo usitegemee cha Mwenyezi MUNGU, rudi kwake. Utaomba mpaka utapasuka
mdomo lakini hamna kitu, mimi nazikataa sauti za wageni. Mimi nashangaa sana, nawaeleza
watu habari za ufalme wa MUNGU, utashangaa watu wengine wanasema “tunaomba
tunampinga Hebron” hamnipingi mimi bali mnampinga MUNGU. Mimi nataka usikie
sauti ya mbinguni na wale ambao wanasikia sauti ya mbinguni wataongozwa na
mchungaji wa mbinguni, kwa hiyo sasa ni kukataa watumishi wa sauti za uongo,
kataa. Biblia inasema hivi wala hawakubali sauti za kigeni, wewe unataka
kubatizwa unaambiwa utoe ada, kataa hiyo sauti kwa jina la YESU.
Unapokubali kwamba mimi si
mwenyeji wa mbinguni, maisha yako yanaharibika, njia zako zinaharibika lakini
wewe huna kosa bali ni mafundisho uliyopokea toka madhabahu za mafundisho
kigeni.
BWANA YESU ASIFIWE, wewe
unakuja kubarikiwa unaambiwa leta pesa ndio ubarikiwe, leta kiwango fulani au
kiasi fulani MUNGU ndio anataka. Soma Biblia, sauti ya wenyeji inasema “nimekupa
bure toa bure”, sasa wengi wanapenda sauti za kuambiwa wale wa elfu elfu, laki laki,
amka, hapa sizitaki sauti za wageni na wewe sema sizitaki, zipotee katika
maisha yangu katika jina la YESU.
Zile sauti zikikufuata na
zikikaa ndani yako zitakuhubiria na kushika maisha yako, vitu vingine si uchawi
ni sauti za wageni. BWANA YESU asifiwe, sijui mnanielewa, utaenda kwenye ibada
ya maombezi, mikutano hiyo ndiyo sauti za wageni, utasikia wakisema “tumemaliza
mkutano chukua bahasha ya sadaka ya kesho, hizo ni sauti za wageni, MUNGU hakutuma
watumishi wake ambao amewatoa mbinguni kuja kutafuta pesa hapa.
Nitawaambia ukweli anayekataa akatae
na akasirike ninakwambia sauti ya mbinguni, ndio maana watu wanahangaika, ndio
maana watu wanateketea wakin’gan’gania njia ya YESU kumbe ni njia ya yesu wa
wageni, tabia za wageni hatuzitaki tunataka tabia ambazo ziko kwenye biblia na
Neno la MUNGU kama lilivyo! Haleluya!
YESU alisema watakuja nyakati
zile za mwisho watachanganya Biblia na uongo, watakusomea Biblia lakini ana
ubatizo wa kikombe, huyo siyo mwenyeji wa mbinguni nina uhakika ninachokwambia,
umenielewa? Uko nabii wa ugeni, mtume (apostle) wa ugeni, mwinjilisti wa ugeni,
mchungaji wa ugeni, mwalimu wa ugeni, askofu wa ugeni, shemasi wa ugeni,
utamjuaje, anayoyafanya hayako kwa Mwenyezi MUNGU, kwa hiyo yeye ni mgeni hayo
ya ugeni umeyatoa wapi, ni kwa mungu asiyejulikana, sasa na wewe unavyoongozwa
hata kama unaabudu hapo umekwenda! MUNGU hakujui, siku ile utasema “BWANA mimi
nimeokoka” umeokoka katika miungu ya wageni, unakubali kusikia sauti ya wageni
unabatizwa kwenye kisima YESU alibatizwa wapi? “mtoni” lakini sauti ya wageni inabatiza
katika “kisima” sasa kuna watu wanataka baraka za MUNGU halafu hawataki kuja kwa
sauti ya wenyeji wa mbinguni, tii, amua, haijalishi watakucheka, haijalishi
watakukataa wewe geuka twende tusonge mbele, kataa sauti za wageni.
BWANA YESU asifiwe, ukitoa
sadaka zako kwa sauti ya wageni usitegemee baraka, ukiimba tu toeni sadaka ya
kwaya, hiyo ni sauti ya wageni. Sasa unashangaa watu wanasubiri sadaka ya
kwaya, sadaka ya pambio, sadaka ya somo la utangulizi, sadaka ya shuhuda,
wanarudi wanakaa baadae sadaka ya mke wa mchungaji, baadae ya kodi ya mchungaji.
Je hapo hamjawa masikini? Je hapo hujarudi nyumbani kwa miguu? Kumtolea MUNGU ni
nzuri lakini unaweza ukamtolea MUNGU katika sauti za wageni ndio maana huoni
kitu.
BWANA YESU asifiwe, na wewe
unaweza ukawa umefanya vitu vingi lakini huoni MUNGU, haya umetoa matofali kwa
wageni unategemea ujenzi uendelee hapo? Lakini MUNGU anasema wale walio wangu
wanaisikia sauti yangu na mchungaji wao hawaitaki sauti ya wageni, kwa hiyo
nakutia moyo mtu anayekukataa angalia anafuata sauti ya nani? sauti ya wageni
wanakukataa sababu wao wanataka kuwa wa michango, wanataka kukanyagiwa sadaka
na bahasha zao wanataka kuombewa kwa viwango vyao walete pesa zao, hizo siyo
sauti za mbinguni, hizo ni sauti za miungu (wageni) maana MUNGU wako ni
anayejulikana, aliyekuumba si mungu mgeni, sasa na wewe imani yako imekuwa ya
wageni, sauti ya wageni ikishaingia kwenye moyo wako hautaki ukweli na ukisoma
biblia inasema kweli ila huitaki.
Fungua masikio yako, sema sauti
za wageni sizitaki tena, toka kwenye nyumba yangu na maisha yangu, mwambie mimi
naijua sauti ya mchungaji wangu namjua na MUNGU, mimi siijui miungu. Utasema
umeokoka, unafunga lakini kumbe uko kwa wageni, unaimba kwaya ya wageni. BWANA
YESU asifiwe, YESU atasema sikujui sikujui, YESU anarudi, ile siku ya mwisho
watu watalia na kusaga meno, YESU atasema wewe ulikuwa kwa kikombe sikujui
sikujui, hiyo siyo sauti yangu nenda mtoni ukabatizwe, mimi ni mkristo lakini sijaokoka
atakuambia sikujui sikujui hiyo siyo sauti ya MUNGU, sasa watu wengi wako
kwenye sauti za wageni na wanaona wako sawa kabisa, nitapiga kelele sauti ya MUNGU
iingie ndani yao ibadilishe watu.
Sauti za wageni zimekaa mpaka
kwenye mifuko ya watu, hapana! Hapana! Baraka zako zina sauti za wageni, unaambiwa
andika jina, namba za simu katika sadaka, hizo ni sauti za wageni. MUNGU mwenyeji
anasema sadaka ni siri yako, sasa wewe unakuja kumlilia MUNGU mbona hunibariki,
waambie wageni waachie mali zako. Sema, mapepo na mafundisho ya uongo siyataki.
Mimi Hebron nilipozaliwa tu
nikawekewa sauti ya mgeni mwanamke huku mwanamume huku wananisimamia ubatizo wa
kikombe, je! YESU alisimamiwa na mtu, sasa hapo wewe haujawa mgeni? Unaonekana
si mwenyeji wa mbinguni, wachawi watakushughulikia wanavyotaka, pesa yenyewe
itakuwa ni mgeni wakati wewe unatakiwa kuwa mwenyeji mwenye baraka, sasa baraka
zinaondoka wakati tumeambiwa, tutatawala, tutashikilia, sasa ziko wapi? Unabaki
na roho ya kilokole, tutakuwa kichwa mbona tumekua mikia? Kama Baba yako yeye
ni kichwa na wewe utakuwa kichwa twende tusonge mbele, sikiliza sauti ya mchungaji
wako ambayo ni ya MUNGU lakini sauti za miungu (wageni) sizitaki, sijui kikapu
cha mama mchungaji, hizo ni sauti za wageni zikatae, ukija kanisani wewe uwe
mwenyeji wa kwenda mbinguni.
MUNGU atakufungua na ukitaka
kumbariki unambariki wewe mwenyewe kwa kupenda siyo kutengenezewa tengenezewa
mazingira ya kutoa mali na madeni, acha kulipa madeni, kama mchungaji amekopa
yeye amefuata sauti ya wageni, MUNGU amesema hivi, mchungaji wangu aniulize
mimi asiumize kichwa, sasa kuna injili za sauti za wageni. BWANA YESU asifiwe,
mtaambiwa pokea, utapokea za wageni, pokea maisha mazuri maisha ya wageni nuksi
balaa na mikosi lakini kwa sauti ya mdomoni umeambiwa pokea mazuri, yeye
anachangisha pesa ndani yake kumejaa nini? Simama imara, unapopokea tofauti na
Mwenyezi MUNGU tayari na wewe unakuwa wa wageni. Mpaka sasa hivi hutaki kuokoka
wewe si mwenyeji wa mbinguni ni mgeni kwa hiyo unataka tu kubakibaki hapa
duniani eti unasema nina dini ya mama yangu watanielewaje? wakatae wageni na
wewe uamue ndani yako mwenyewe, sema nakataa, kwa sababu mimi nikikwambia kataa
kama wewe mwenyewe unasema nawapenda ni kazi bure. Tumeharibiwa dunia nzima,
asilimia kubwa tunafanywa kuwa wenyeji wa dunia hii siyo wenyeji wa mbinguni.
Amenituma niwaeleze habari
njema, mimi Hebron situmwi na wanadamu na hata wao ambao wanawapeleka watu
kuwaletea sauti za wageni, OLE wao watakutana na Mwenyezi MUNGU, MUNGU anawapenda
watoto wake, ndio maana hamfanikiwi mnateseka wakati YESU ameleta watumishi
wake wa kweli na wale wa kweli nao wanakanyagwa, hawasikii, sasa hivi watumishi
wa kigeni ndio wamejaa, mafundisho ya kigeni, mapokeo ya kigeni yamejaa, sasa
wewe umeshamjua BWANA YESU ni wakati wa kuyakataa mafundisho ya kigeni ama sivyo
watakurudisha nyuma uwe mgeni wa jehanamu, mwambie mimi sitaki, mimi ni
mwenyeji wa mbinguni.
Watoto wako unapeleka kwa
wageni, wanaenda kubatiza watoto wadogo, mtoe huko kwa maombi, wewe umesikia
sauti ya MUNGU Neno la kweli limekutoa huko, piga sauti ya wageni, mimi nakueleza
unaweza ukazunguka Arusha nzima au Tanzania ukakuta makanisa ya kweli labda ni
arobaini (40) tu, tena haya makanisa makubwa makubwa baadhi yao ndiyo hayafai
kabisa, mimi ninawaambia ukweli, ninauhakika na ninachokisema, ninajua
wanachokifanya lakini mwisho wao siyo mrefu na kazi hiyo imeanza anaifanya YESU
peke yake ili kweli inyanyuke, maana Mwenyezi MUNGU anataka watoto wake, dini
imekuwa ni biashara na michango, hayo ni mambo ya wageni, hata kama atakuja
askofu na mashuka yake na kusema tunatoa mchango hapa, hayo ni ya wageni, halafu
unategemea baraka zako zije hapo, haziji, ndio maana unachanganyikwa, rejea
uokoke twende mbele, kataa mafundisho ya uongo haijalishi watakukataa,
haijalishi watakuchukia, sema sawa tu mimi ninakwenda mbinguni.
Unajua kile kilichomjaa mtu
ndicho kimtokacho, atakurudisha nyuma usiende mbele atakuambia nifuate mimi
usisikilize sauti ya kweli mwambie wewe ni mgeni sitaki sauti ya wageni, haya
utasema nataka nibarikiwe, mgeni unategemea baraka za MUNGU? Njooni bwana kwa
mfalme upate mambo yako.
Inawezekana mume naye tayari
kuna sauti ya wageni au mke au watoto, vitu haviendi, sasa ni kuvunja hizo
sauti za wageni na uzichome moto katika ulimwengu wa roho, MUNGU amesema
nimekupa bure toa bure sasa mchungaji bila aibu tena anachangisha watu pesa,
huyo ni mlafi, nasema ni mwizi tena ni jangili kabisa. Ukisoma moja ya amri ya MUNGU
inasema “usiibe” sasa yeye mwenyewe mchungaji ni mwizi anachukua pesa za watu
pesa ndiyo awaombee wakati MUNGU anasema nimekupa bure toa bure, wewe hauoni
huyo ni mwizi mnabaki kusema tunapiga roho ya wizi wakati mchungaji (pastor)
mwenyewe ni mwizi. Nakuambia kweli ukichukia chukia mimi nasema kweli, wengi
watafunguka na watamjua MUNGU, wewe unaye n’gan’gania utabaki na baba yako
mwizi na madhabahu ya wizi na mapepo yatakuja kuiba kila kitu chako, sikiliza
sauti ya MUNGU na mchungaji wako anayekuongoza lakini ukiona mambo ya michango michango
ujue hapo hamna sauti ya MUNGU, tayari na nyie mmeshaharibikiwa, wewe utajiona
umesimama sawa lakini kumbe umeharibikiwa, haleluya!
BWANA YESU asifiwe, utaenda
kwenye maombi na hata redio unalala nayo ukisikiliza usiku kucha au TV kumbe
unasikiliza sauti ya wageni, wageni wa kipepo wanaingia kwako, mafundisho ya
uongo, maroho ya shetani yanaingia ndani yako, kataa, ndio maana hata baraka
kwako hazikai. Mungu ametuandalia Baraka uzao wa Ibrahimu, ziko wapi, kuna
wageni haijalishi watasema nimeokoka, wanatumia biblia, Yesu alisema watatumia
jina langu lakini Mimi sijawatuma. Nimetumwa niwaambie habari njema, kwa Mungu
wewe ni mtoto wa mfalme, sasa wewe nenda kwa wageni na useme mimi mtoto wa
mfalme kumbe ni mtoto wa mgeni. Mimi Hebron nataka uwe mwenyeji wa mbinguni,
nataka uyashikilie maneno haya, nataka yakusaidie utaona unanyanyuka, utaona
unasonga mbele, siyo kwenye sanamu kidogo, kwenye kadhalika kidogo, utashangaa
umepotea. Sema hata madhabahu za kigeni siendi, kwa maana unapoingia tu pale,
anayoyazungumza mchungaji na wewe tayari umeshaisikia sauti ya wageni tayari umetekwa,
hata useme sadaka yangu siandiki jina haijalishi roho ni ile ile, uchumi wako
wenyewe utakuwa ni wakigeni, baraka zako hazikukubali, sasa ukija kwenye sauti
ya Mungu inasema “mtakanyaga, mtamiliki, mtashika” iko wapi? Makosa siyo ya
kwako na wala hautendi dhambi, ni sauti za kigeni.
Haleluya! Ukiwa mwenyeji wa
mbinguni hakuna pepo litakusogelea wala mchawi, lakini kwenye sauti za wageni
wachawi ndiyo watakutesa, sikiliza sauti ya wenyeji, mimi Hebron mchungaji
wangu ni Yesu siwezi shindwa, na wewe twende pamoja hauwezi shindwa, haleluya!
Sikiliza sauti ya mchungaji wako ambayo ni sauti ya mbinguni utanyanyuka, sasa
wewe kama ukitaka kusikiliza sauti ya mchungaji wako mambo ya elfuelfu,
michango, ubatizo wa ajabuajabu, nakuambia wewe ni wa hapa hapa, fanya uamuzi
wako sasa na ubadilike, umrejee Yesu.
Unaweza ukawa wa yesu wa kigeni
lakini haupendi, kwa nini watu wanachukia ukweli? Mimi Hebron kabla sijaanza
kuhubiri habari za Yesu wa kweli kila mtu alinipenda lakini nilipoanza kusema
ukweli hata wachungaji walinichukia na kuanza kuniambia sina adabu, mimi nina mheshimu
Mungu, sitaki pesa za watu, mimi siyo mwizi lazima sauti ya Mungu niisikie ”nimekupa
bure toa bure”, hao wanaochukua pesa za watu wameshakuwa wachawi, unaweza
kusema unaenda kumuona mchungaji kumbe unaenda kumuona mganga na anakupigia
simu akisema “Bwana ananiambia usipotuma pesa haraka utaangamia” na wewe
ukisikia hivyo unaogopa na kuanza kutafuta pesa popote na hata kukopa ili
upeleke sadaka mimi nakuambia hiyo siyo sadaka ni pesa ya mkopo anayodaiwa
mahali anataka akalipe, usikubali kufanywa chuma ulete, akafagie hata barabara ili
apate pesa na siyo kuwanyan’ganya watoto wa Mungu pesa zao, nakuambia ukweli,
mimi Hebron sina ushirika na wapuuzi na watu wa namna hiyo maana Biblia inasema
niwapumbavu na wewe kataa, Yesu alikataa sauti za wageni leo ni mwenyeji wa
mbinguni.
Utasikia baadhi ya watumishi wakisema Bwana Yesu asifiwe ukafikiri ni
sauti za mbinguni hizi Bwana Yesu asifiwe hizi hata shetani ni aina ya bwana
hata wewe na bwana wako ni bwana kuna bwana shamba, kuna bwana afya wote hao ni
mabwana lakini huyu Yesu ni Bwana tofauti, kataa sauti za kigeni, huyo yesu
anayeangalia mifuko yako, nakwambia huyo siyo Yesu wa mbinguni, nakwambia
ukweli, hili ni kanisa la wenyeji wa mbinguni na mimi Hebron ni mchungaji
nimeletwa kutoka mbinguni sasa sikiliza twende kwa wenyeji wa mbinguni.
Yesu aliwaambia mithali hii
hawakuelewa sasa wewe uelewe, usipoteze muda wako kwa wageni wa hapa duniani.
Bwana Yesu asifiwe, unayetaka kupona upone, mbinguni wanakwenda wenyeji, wewe
usitake kwenda na ugeni wa shetani kule mbinguni, nembo ya ubatizo wa kikombe,
ubatizo wa kisima wanakuambia maji tele, wapi? Kama ni kubatiza kwenye visima
angebatiza Yohana maana jagwani kuna visima vingi lakini alienda mtoni kama
alivyoonyeshwa na wenyeji wa mbinguni maana mbinguni upo ubatizo wa mtoni,
huwezi kubarikiwa ukiwa ni wa wageni, nataka uwe mwenyeji, na unapokuwa
mwenyeji wa mbinguni usifikiri wale ambao hawataki mambo ya mbinguni watakupenda,
hawatakupenda kwa sababu ndani yao iko roho ya hapahapa ya kuwapeleka kuzimu,
imeruhusiwa kwa mwanadamu anayetaka kuwa mwenyeji wa mbinguni sawa anayetaka
kuwa mgeni sawa, ndiyo maana Biblia inasema katika mstari wa tano Yohana 10:5,
inasema hivi “mgeni hawatamfuata kabisa
bali watamkimbia kwa maana hawazijui sauti za wageni.”
Hata mimi Hebron mgeni simtaki
kabisa, hayo ni mapepo, mafundisho ya uongo siyataki kabisa, nimewakimbia maana
namjua mchungaji wangu ni Yesu wa mbinguni asiyebatiza kwa kikombe, asiyeombea
watu kwa pesa, ambaye hana ubaguzi, ambaye hana sadaka ya mama mchungaji,
ambaye nyumba yake yeye haina mambo ya kigeni, sijui harambee, mara amekuja
Raisi, sijui Katibu, sijui askofu hayo ni mambo ya sauti za wageni mtakuwa na
makanisa ya kigeni, kataa, nataka kanisa la wenyeji wa mbinguni pale ndipo Yesu
alipo, Biblia inasema “pale unapoabudu
ndipo na maisha yako yalipo”. Kuna watu wanabudu mahali penye madhabahu za
kigeni maisha yao yanabaki kwa wageni, yatoke katika Jina la Yesu, haijalishi
watakushauri kwamba umepotea, waambie mimi ni mwenyeji nyie ni wageni, mimi
Hebron nilichukiwa, nilikataliwa lakini nimewasamehe wote walionikataa maana
wao wamekuwa ni wageni hawataki habari za mbinguni, achana na sauti za wageni
zikatae twende mbele, Mwenyezi MUNGU awabariki sana.
APOSTLE
HEBRON.