Pages

Monday, June 6, 2016

NENO LA MUNGU NI KWELI NA LIKIBADILISHWA LINAKUWA SIYO NENO LA KWELI BALI NI LA MIUNGU!

BWANA YESU ASIFIWE, katika makala hii nitaelezea kwa nini neno la MUNGU ni kweli na pia ni kwa nini tena neno hili linaloitwa neno la MUNGU likawa tena ni neno la uongo. Katika ulimwengu wote watu wengi wanajua kuwa neno la MUNGU ni kweli na ndiyo sababu wanalifuata na kulipenda sababu kupitia hiyo kweli inawapa uhakika wa kumfikia MUNGU mbinguni na kuurithi ufalme wa MUNGU. Lakini nyakati hizi na hata enzi za mitume wa MUNGU wa kweli waliotangulia akiwemo na YESU; wao walishajua kuwa neno la MUNGU huko mbeleni litabadilishwa na kutoka katika kweli na kuletwa injili ya namna nyingine ambayo siyo ya kweli na mtu anapoipokea tu na yeye anakuwa yeye siyo wa imani ya kweli tena, anakuwa ni wa imani ya injili ya namna nyingine; soma Wagalatia 1:6-7.


YESU NI MKWELI NA YEYE SIYO MUONGO.

Yohana 14:6;
6 YESU akamwambia, mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi.”

Yohana 17:17
“17Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.”

Ufunuo wa Yohana 22:18-20
18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, mtu yeyote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. 19 na mtu yeyote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki. 20 Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amen; na uje BWANA YESU.”

Katika masomo hayo yote yanakuelezea uhalisi wa ukweli kabisa kuwa neno la MUNGU ni kweli. Jinsi ya kujua neno la MUNGU ni kweli wewe fuata biblia ilivyoandikwa na uifuate kama ilivyo na endapo utaichanganya na mambo ambayo hayapo basi hapo tayari hilo neno linakuwa siyo la kweli na MUNGU haonekani hapo sababu ameingia katika nafasi hiyo mungu wa uongo na hapo ndipo na wewe unakuwa unaongozwa na mungu wa uongo kwa kujua au kutokujua; ila idadi kubwa ya watu wengi wanaona wapo katika kweli kumbe wapo katika uongo hivyo utakapo ujua ukweli uchukue hatua kufuata ukweli na ujitenge na uongo wa injili kiroho na kimwili ili upone kabisa.

Nitaelezea kwa ufupi ila zaidi utaendelea kusoma katika website yangu www.prophethebron.org yapo masomo ya kukutosha kukufundisha ufunguke kabisa kama atakavyo MUNGU wa kweli. Hili jina la YESU lina uthamani ambao hakuna kiumbe chochote chenye uthamani huo au hata mitume na manabii waiopita na watakaokuja; hivyo shetani alijua kuwa watu watamkimbilia yeye sababu jina la shetani halina uthamani wowote, ni ovyo kuliko vitu vyote hapa ulimwenguni. 

Alichokifanya huyo shetani, yeye akajipenyeza kwa wanadamu na akawapa utumishi na akawapa mafundisho yake wayachanganye na biblia pasipo watu kujua na hapo ndipo uongo ukachanganywa na neno la MUNGU na watu wakalishika neno la MUNGU likiwa limeunganishwa na uongo; na wote mnajua kuwa giza na nuru hazikai pamoja hivyo ndiyo ilivyo neno la MUNGU la kweli halichangamani na uongo au injili yeyote ila itokeapo popote tofauti na katiba ya MUNGU alivyoitoa kwa wanadamu yaani biblia.

UKRISTO UNAKUWA NI WA UONGO KWA JINSI HII;

1.     Ukristo unakuwa ni wa uongo pale tu mkristo anapojiita yeye ni mkristo lakini hapo hapo hataki wokovu na utashangaa hata kanisa linakataza mkristo asiokoke. Ukiangalia hapa utaona upo upinzani wa kukataa kweli na kushikilia uongo na mkristo anapojiita mkristo yeye anajifariji tu kuwa yupo na YESU lakini nataka uelewe upo na yesu wa uongo ambaye yeye ukristo wake ni wa uongo na wokovu kiimani na kimatendo.

2.     Mifano ya ubatizo yote ya uongo, ukianzia zote ambazo hazipo katika neno la MUNGU hizo ndizo injili za namna nyingine watu wanaletewa na wanazipokea wasipojijua na wengine wakijua na kwa jinsi hiyo unakuwa unapata kiapo cha kuwa mkristo wa uongo wa miungu badala ya kuwa mkristo wa kweli wa MUNGU.
a)    Ubatizo wa maji ya kikombe.
b)    Ubatizo wa kisima.
c)     Ubatizo wa kubatizwa kwa jina la mchungaji.
Na nyinginezo zote tofauti na ubatizo wa maji mengi yanayotembea kama yale alivyobatizwa nayo YESU Yordani huo ndiyo wa ukweli. Hivyo nawaeleza mataifa yote mrejee mkapate kiapo cha ubatizo wa kweli na kuliondoa kiapo cha uongo ambacho katika ulimwengu wa roho wewe unaonekana siyo mkristo mwenye alama ya neno la kweli yaani MUNGU bali unayo ya uongo na kumfanye shetani awe anao uhalali na wewe kabisa; sasa maamuzi ni yako. YESU anarudi na wengi wanakufa na alama hizo za uongo wala YESU hawatambui pamoja na ukristo wao. Sasa kataa huo uongo na zaidi muulize aliyekubatiza je hili ndilo neno la kweli aliloagiza YESU? Hata jibu.

3.     Ukisoma imeandikwa “nimekupa bure toa bure”, haya ni maneno ya YESU aliyoamuru yafuatwe; sasa unapoambiwa utoe pesa ndiyo uombewe au ndipo ufanyiwe huduma ya kiroho nataka uelewe hapo hakuna roho wa MUNGU wa kweli sababu hayo anayokueleza siyo maneno ya kweli ni ya uongo; hivyo ukienda kwa mungu wa uongo yeye ndiye anayechaji watu pesa mfano waganga wa kienyeji, mizimu na makafara au unakuta mtumishi anatumia jina la YESU kwa kuchaji watu pesa ndiyo uweze kuonana na yeye au ili akuwekee mkono anataja kiasi fulani ulipe ndipo akuwekee mikono. 

      Ukiona hivyo au kusikia elewa hilo silo neno la kweli lililotokea kwa YESU wa kweli bali ni neno la uongo na miungu ndiyo inayomuongoza huyo mtumishi bali watu wanafikiriia ni YESU yupo ndani yake; ni pepo la unyang’anyi ndilo lipo ndani yake wala siyo roho wa MUNGU wa kweli, bali ni roho wa uongo wa miungu.

4.     Sadaka zote ambazo zinaandikwa majina na kupewa risiti au kutangazwa kanisani na kupewa cheti cha hongera unakuwa ni mtoaji mzuri au unakuwa rekodi zako za sadaka halafu usipotoa fungu la kumi baadaye unaambiwa unadaiwa sadaka ya MUNGU ya mwezi fulani. Huu ni uongo silo neno lisemavyo; neno la kweli linasema ukitoa asijue mtu yeyote yule na endapo akijua iyo thawabu yako inabakia kwa watu na MUNGU haupati thawabu yake sababu unafuata ya uongo na hiyo madhabahu inakuwa ni ya uongo na siyo ya kweli, hiyo ni dalili inaongozwa roho ya uongo ila mnapigwa upofu mnaona mpo na MUNGU wa kweli kumbe upo na mapepo ya injili ya namna nyingine. Neno la kweli linasema sadaka ni siri yako kati yako na MUNGU, sasa huu uongo wa neno hili linatokea wapi? Hivyo sadaka zako haziendagi kwa MUNGU zinaenda katika ufalme wa uongo na mwishowe isipokupitia neema ya MUNGU wa kweli na wewe utaenda huko ulipopelekewa sadaka zako na utakuta taji lako la mauti ya milele jehanamu utavikwa.


Zipo sadaka za kukanyagiwa miguuni, sadaka za kuchangisha, sadaka za kutoa ndiyo utamkiwe unabii, hizi zote ni sadaka za uongo za unyang’anyi wala hazina ushirikiano kati ya ibada yako na MUNGU wa kweli yeye anaangalia kweli ndiyo ashiriki ibada yako ikiwa inauongo anakuja mungu wa uongo kushirikia ibada hiyo.

5.     Kuhusu makanisa au watumishi wa MUNGU wa kweli hawaruhusiwi kuchangisha katika neno la kweli linasema “wewe mtumishi wangu usifikirie utakula nini, na mengineyo, kama nanyeshea maua je wewe siyo bora zaidi yao.” Utaona sasa wengi hawafuati neno la kweli na hii ni sababu wapo waliojiita, waliomsaliti YESU, wapo wa mshahara, wapo wachawi, wapo freemason. Sasa mataifa yote msishangae mnapo yaona hayo yakifanyika na yataendelea kufanyika hiyo ndiyo dalili kubwa ya kujua hawafuati neno la kweli la MUNGU bali wanafuata uongo wa injili ya namna nyingine na hii injili ya namna nyingine inatokea kwa huyo mungu asiyejulikana ambaye yeye hana lolote katika dunia hii mfano hajaumba hata mtu wala mdudu; injili zake ni lazima michango na hata kukopa benki. 

      Neno linasema usichaji riba sasa iweje yeye kanisa ni lake lilipe riba? silo lake, au kwenye radio au tv au crusade, ukiona mtumishi anaomba pesa za kufanyia hiyo kazi uelewe hana neno la kweli ndani yake na ndiyo sababu ahadi za kweli za MUNGU hazionekani kwake. Zaidi MUNGU akimtuma mtumishi anamfanyia njia mwenyewe na siyo ajiaibishe kuwa anayo matatizo haiwezekani bila wewe. Neno linasema amtegemeaye mwanadamu amelaaniwa, je ni wangapi leo hii wamelaaniwa?

6.     Kuhusu hekalu; unajua ni mahali patakatifu na haparuhusiwi hata kufanyika michango. Angalia picha ya leo sehemu nyingi siyo hekalu tena ni soko. Yeye aliwafukuza hekaluni leo yamerudishwa, ndiyo injili aliyoikataa YESU ya namna nyingine ikifanyika yeye haitaki haya; wanadamu baadhi ndiyo wanayoitaka. Sasa huko ndiko kumkubali shetani na kumfukuza YESU; hilo ndilo neno la kweli la MUNGU na yapo mengi roho mtakatifu asemaye kweli azidi kukufundisha ukweli ili hata imani yako kweli kwa YESU imfuate YESU wa kweli na isimfuate tena yesu wa unafiki ambaye hajulikani. Utaujua kwa kufuata neno la MUNGU bila kuchanganywa na uongo au unongezwa zaidi ya MUNGU alivyopiga mhuri kitabu chake kitakatifu.

NOTE:

Kwa mataifa yote muwe makini sana kwa kulifuata neno la kweli ukiona linachanganywa na uongo hapo MUNGU wa kweli hayupo, hata kama utang’ang’ania kukaa hapo utakuwa umekaa kwa shetani na unamwabudu pasipokujua au kwa kujua, ipo mifano mingi ninayoelezea kwa YouTube, blog, vitabu pia; na maneno ya kweli alivyonieleza YESU asemaye kweli, ambaye ni mwana wa pekee wa MUNGU wa kweli.

Nataka uelewe yupo mwana wa pekee wa mungu wa uongo, ndiye aliyechanganya neno la MUNGU wa uongo na watu wakafuata na kutekwa na shetani. Japo wapo watumishi wanadamu kabisa walioingia mkataba na shetani wa kuleta injili ya uongo; hao yapo mambo yatawapata ambayo atayafanya MUNGU peke yake na kwa wengine ameshaanza  kazi hiyo. Myaonapo msishangae! Zile OLE za neno la kweli juu ya wanaodanganya watu zitaanza kuonekana kimwili kabisa na ndipo macho ya watu yatashangaa imekuwaje apatwe na hiki au yale? Mwenye akili na ajue asema BWANA MUNGU WA MAJESHI asemaye kweli na ndivyo ilivyo.

Rejeeni- BWANA YESU naomba unisamehe dhambi zangu kwa kufuata injili ya namna nyingine isiyo ya kweli. Uniandike jina langu katika kitabu chako cha uzima wa kweli, unitoe katika kitabu cha mauti ya milele. Amen.

UBARIKIWE.

NABII HEBRON.