Pages

Saturday, December 7, 2013

NINI MAANA YA FATHER CHRISTMAS? 



Ndugu msomaji wa makala ya Nabii Hebron, leo napenda kuwafundisha watu wote wa ulimwengu huu kuhusu neno FATHER CHRISTMAS ni nini na chanzo chake, maana watu wengi hata mimi nyumbani kwangu wakati wa Krismasi nilinunuaga huyo mdoli anayeitwa Father Christmas pasipo kujua maana yake mpaka YESU WA NAZARETI aliponifunulia siri hii.

Akaniambia Hebron nikuulize swali?  Nikasema ndiyo BABA, akaniuliza hivi Krismasi ni sikukuu ya nini? Nikamjibu, ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwako, akasema sawa kabisa. Sasa kwa nini badala ya wanadamu kumkaribisha YESU yaani mimi katika nyumba zao na makanisa yao, wanampamba huyo anayeitwa Father Christmas. Nikashtuka. Akaniambia, je? Hebron, mimi ndiye huyo mdoli anayevalishwa nguo nyekundu na madevu? Nikajibu, siyo.

Akaniambia shetani amewateka wanadamu na wanafanya wasilolijua. Huyo Father Christmas asili yake na mpaka kufikia kuitwa hivyo na wanadamu waliomuasi MUNGU aliye hai. Akaniambia, asili yake ni mzimu, tena ni mwanadamu ambaye tayari ameshakufa miaka mingi iliyopita. Naye aliitwa Nicholas, huyu ni mturiki, aliachiwa mali nyingi na wazazi wake akiwa mdogo, ila alikuwa anawasaidia watu hata kuwalipia mahari wale waliokwama na hakupenda ajulikane ila yale aliyoyafanya watu waliyasema. Na baadaye akawa askofu na alijiita Saint Nicholas. Na hata alipokufa mifupa yake ikachukuliwa kwenda Italy katika bandari Bari, na watu wanabaharia pia huiabudu hiyo mifupa yake eti bahari itapoa na yeye ndiye anayeipooza bahari itulie mwaka mzima.


Akaniambia, wanadamu wakajipangia katika nchi za Ulaya wakamtungia jina wamuite Father Christmas. Sasa ndugu msomaji, nimeeleza kwa kifupi tu ili upate picha. Kumbe siku ya Krismasi ni siku ya BWANA YESU TU (Happy Birthday yake) sasa jiulize, kwa nini siku hiyo ambayo ni ya mfalme YESU WA NAZARETI ambaye ndiye mtoto wa MUNGU wa pekee, je? Ni halali siku hii kuiita na kumpa huyu Nicholas ndiye aitwe baba wa Krismasi? Jibu, siyo sawa. Ni dhambi na kumkufuru MUNGU aliyemuumba mtoto wake na akaifanya ni siku yake ya pekee na ndiyo maana siku ya Krismasi ni sherehe ya kukumbuka kuzaliwa kwake mkombozi wa ulimwengu huu.

Ila shetani ameingiza mchomeko wake hapo wakampa jina Nicholas eti ndiye Father Christmas. Embu fuguka ufahamu wako, je ni sahihi siku ya YESU kuzaliwa apewe mwanadamu yeyote aliye hai au aliye kufa? Sasa basi, kila anayeweka huyu mdoli au cartoon ya Father Christmas ajue kuwa anamuadhimisha Nicholas ambaye amekufa na hajafufuka. Na kama anaadhimishwa mtu aliyekufa inamaana hiyo ni mitambiko au ibada ya wafu. Watu wengi wameshiriki bila kujua na zaidi cha ajabu siku ya Krismasi utakuta huyo mdoli ya Father Christmas imepambwa makanisani, haifai kabisa.

Na mfano uliotumika kumpata Father Christmas ni sawa sawa tuu na wale viongozi  maarufu waliokufa halafu baadaye wanadamu waamue kumpa jina la Father Christmas, au kina Petro, Musa, Eliya, hawa walitenda mema zaidi kuliko watumishi wote waliopita lakini bado hawakuchukua utukufu wa MUNGU wajiite Father Christmas. Na sasa ulimwengu muwe macho msije mkashangaa wanadamu wakatafuta tena mtu yeyote wamuite Father Easter, huku ni kumuasi MUNGU na mnashiriki matendo  ya shetani.

Mpaka hapo umeelewa na kama makanisani na katika nyumba zenu mmeweka hiyo midoli ya Father Christmas, mjijue ni mzimu wa Nicholas ndio mnaouadhimisha na siyo YESU WA NAZARETI, hivyo na sikukuu hiyo imeharibika kwako na haujashiriki Krismasi safi ya YESU WA NAZARETI bali umeshiriki mzimu. Umeshajiuliza, imeandikwa katika biblia msiabudu sanamu, sasa hata kibinadamu nyie wakristo mkiangalia hauabudu sanamu? Na je dhambi haijakuotea? Fungukeni ufahamu shetani alibuni njia nyingi sana ili kuhakikisha tuu mmemkosea MUNGU aliye hai na mbakie mali yake. Na akajichomeka katika siku ya Krismasi na kuiharibu kwa kuwakamata fahamu wanadamu wamtafute mtu na wampe jina yeye ndiye Father Christmas.

Sasa nikuulize swali, yaani hata BABA yake YESU WA NAZARETI aliyemleta hapa duniani, amenyimwa utukufu huo na badala yake ni kumpa mzimu utukufu na midoli. Wanadamu, hizi elimu za uongo muwe makini sana, mtaangamia pasipo kujua, usishiriki kabisa kuweka hiyo midoli ya Father Christmas ni kumkufuru MUNGU.

MUNGU siyo mdoli, siyo sanamu, wala YESU siyo sanamu. Sanamu haina uhai, haiongei, haina akili. Sasa watu wametekwa na kuabudu sanamu ya Nicholas ambaye huyu ni mwanadamu kama wewe tuu, wala haikupaswa aitwe yeye ndiye BABA WA KRISMASI. Na kama siyo sahihi elewa umetenda dhambi umeabudu sanamu. Tazama sasa katika siku hiyo ya Krismasi kila mahali utaona midoli ya Father Christmas, mahotelini, makanisani baadhi na hata  kwenye nyumba za watu wanazoishi.

NOTE:
Ukimweka ndani huyo mdoli ujue umeweka sanamu ya Saint Nicholas na yeye siyo YESU. Na ni machukizo matupu mbele za MUNGU, msifanye hivyo. Ukisoma mueleze na mwenzako ili Krismasi yako isiwe na laana, ukawa umemwadhimisha mzimu. Kama ilivyo miaka yote watu hawajui na wanamuabudu sanamu siku hiyo na kuiweka itawale katika nyumba zenu.

Sasa umeujua ukweli na upone. Ili YESU WA NAZARETI peke yake na MUNGU aliyemleta aje hapa ulimwenguni ndiyo wainuliwe tuu na utukufu wa siku hiyo arudishiwe yeye peke yake maana ndiye anayestahili na siyo kumpa mwanadamu. Jina la Father Christmas life kabisa katika ulimwengu wote na hiyo roho iangamie kwa damu ya YESU WA NAZARETI na malaika wa mbinguni waiteketeze kabisa, abaki MUNGU wetu tuu arudishiwe utukufu katika kiti chake cha enzi.


NABII HEBRON.